Jiongeze: Marioo hakomi kwa mkwewe
Muktasari:
- Kuna muunganiko wa Harmo na Marioo tena. Huu ni wa kisanaa zaidi kwa Marioo kumpa shavu sana Harmo. Na kwenye ngoma zao kadhaa walizokwishafanya ni rahisi kujua mkwe na mkwewe ni yupi. Balaa lilianzia kule kwenye “Naogopa”.
Dar es Salaam. Kuna muunganiko wa Harmonize na Marioo. Kwanza ni kifamilia zaidi kwa maana ya Marioo wa Paula na Harmo wa Kajala. Toto Bad ni wa mtoto na Konde Boy ni wa mama mtu. Kimsingi ni familia ya mtu na mkwewe.
Kuna muunganiko wa Harmo na Marioo tena. Huu ni wa kisanaa zaidi kwa Marioo kumpa shavu sana Harmo. Na kwenye ngoma zao kadhaa walizokwishafanya ni rahisi kujua mkwe na mkwewe ni yupi. Balaa lilianzia kule kwenye “Naogopa”.
Mule ndani Konde kaua sana lile ‘vesi’ lake. Kuna utawala mkubwa kaufanya na kuliteka pini kibabe sana. Na haina maana Toto Bad aliishi kinyonge mule, Konde ni wazi kaonesha ukubwa na kwa kiasi flan ‘vesi’ ilikimbiza ‘striti’.
Kuna ngoma ya “Wangu”, na kuna hii ya juzi juzi “Pombe”. Hizi zote wamepiga ‘kolabo’ la kikatili sana wana familia hawa. Muunganiko huu unazalisha kitu kama Roma na Stamina na kutuletea ubunifu wao wa Rostam. Hii imeenda.
Kwa wasanii washamba, Marioo angeweza kumpotezea Konde katika ngoma zingine. Baada ya kuumizwa na ile Naogopa, ajabu Toto Bad akili mingi, ndo kwanza anakomaa na mkwewe wakitoa madude kila siku na yanaenda.
Jaribu kuwaza hii familia kubwa ilivyoamua kuungana kutafuta pesa. Jaribu kunusa harufu tamu ya pini la Konde Boy na Toto Bad. Kisha warembo wakatumia binti na mami yake? Yaani Paula na Marioo, Konde na Kajala. Oyaa!
Madogo kizazi hiki wapo mbele ya muda sana. Kila kitu kwao wanakigeuza fursa. Familia hii ni fursa kamili, na wanaenda kuwa wakubwa kama siyo kipesa basi kifamilia zaidi. Bahati nzuri hata mama na bintiye wajanja.
Hii iitwe “KAMA HAPA” yaani ni Kajala, Marioo, Konde, Paula. Au “KAMA KOPA”, Kajala, Marioo, Konde, Paula. Kila kitu ni fursa na kama hujui fursa ndo kama hivi nakuonesha juu ya familia hii ambayo ni fursa kama fursa. Unyama.