Kilio cha wasanii kwa serikali

Muktasari:

  • Maboresho ya sera yatakayochochea kupanuka kwa masoko ya kazi zao na kuinua vipato vyao, ulinzi zaidi wa kazi zao, urahisi wa kukopesheka, mafunzo na miundombinu rafiki kwa sanaa yao, mambo wanayohitaji.

Dar es Salaam. Baadhi ya wasanii wa muziki na filamu nchini wameeleza yale wanayotaka yafanyike katika tasnia yao chini ya utawala wa Rais Samia Suluhu Hassan ambaye anaelekea kutimiza miaka mitatu madarakani.

Maboresho ya sera yatakayochochea kupanuka kwa masoko ya kazi zao na kuinua vipato vyao, ulinzi zaidi wa kazi zao, urahisi wa kukopesheka, mafunzo na miundombinu rafiki kwa sanaa yao, mambo wanayohitaji.

Utakumbuka Machi 2021, ndipo Rais Samia aliingia madarakani na ameweza kuigusa sanaa, machache kati ya mengi aliyofanya ni kurejesha tuzo za muziki na filamu, kuanzishwa kwa mfuko wa kukopesha wasanii pamoja na kulipwa mirabaha ya kazi zao.

Kwa nyakati tofauti wakizungumza na gazeti hili, wasanii hao wameshukuru mengi mazuri yaliyofanywa na Rais Samia katika miaka yake mitatu kama tulivyoripoti wiki iliyopita ila sasa wana maombi machache kwake.

Mwimbaji wa Bongo Fleva aliyetoka kimuziki chini ya Tanzania House of Talent (THT), Mwasiti Alimas amesema maboresho yafanyike katika mfuko wa wasanii ili wote waweze kupata mikopo kwa urahisi bila kuangalia ukubwa wao.

“Tukopesheke, sasa hivi msanii kukopesheka ni mtihani ndiyo maana wanaoweza kupata kwa ukubwa huo ni wale wasanii wakubwa wanaoonekana. Nasikia wamebadilisha mfumo wa kutoa mikopo, nafikiri waliona mfumo wa mwanzo labda kidogo una hitilafu,” amesema.

“Hiyo inaonyesha ni jinsi gani na sisi wasanii tunatakiwa kufanya muziki uwe kazi, yaani mtu akikuona aamini haya ndiyo maisha yako, hiyo itatusaidia na sisi huko ambako tunataka kukopa, basi tukopesheke kwa amani na upendo kabisa, yaani mtu anakupa mkopo anajua kabisa huyu anarudisha kwa sababu tunaona anachokifanya,” amesema Mwasiti.

Amesema mikopo isiwe kwa ajili ya wasanii wakubwa wanaoonekana bali iwe kwa yeyote kwa sababu hata msanii mdogo hiyo fedha anahitaji ili aweze kusoga mbele kisanaa kama hao wengine.

“Pengine naye anatamani video yake iwe kubwa lakini kwa mfano akiomba mkopo wa Sh5 milioni au Sh10 milioni, ukampa Sh1 milioni au Sh2 milioni, bado unakuwa hujamsaidia huyo kijana,” amesema Mwasiti.

Utakumbuka mwaka 2007, ndipo Mwasiti alishinda tuzo yake ya kwanza katika muziki, kutoka TMA kama Msanii Bora Chipukizi, ushindi huo ulikuja mwaka mmoja baada ya kuachia wimbo wake wa kwanza, Niambie (2006), uliofanya vizuri.

Kwa upande wake muigizaji mkongwe wa filamu, Jacob Steven (JB), amesema kiu yake chini ya utawala wa Rais Samia ni kuona masoko ya kazi zao yanaongezeka zaidi, lakini pia mitaji kwa wasanii iongezeke ili kuinua kazi na uchumi wao.

JB ameeleza hayo baada ya kukiri kuwa ndani ya miaka mitatu ya Rais Samia ameshuhudia ongezeko kubwa la masoko ya kazi zao na mitaji kwa wasanii kitu ambacho ni kizuri na ishara ya ukuaji wa tasnia ya filamu.

Staa huyo ambaye amekuwepo kwenye tasnia tangu mwishoni mwa miaka ya 1990, amecheza filamu maarufu kama Lost Adam, Off Side, Fair Decision, Senior Bachelor, Peace of Mind.

Naye Staa wa Bongo Fleva, Zuwena Mohammed ‘Shilole’ amesema tangu Rais Samia ameingia madarakani kwao wasanii imekuwa neema sana maana wameendelea kuaminika zaidi katika nafasi mbalimbali za kuitumia nchi yao.

Amesema kutokana na mazingira mazuri yaliyowekwa kwa kazi zao, taasisi nyingi zimekuwa zikiwaamini wasanii na kufanya nao kazi, haya ni maendeleo makubwa, hivyo anaomba sera zizidi kuboreshwa tu.

“Sera ziendelee kuboreshwa na kufanywa rafiki zaidi ili tuendelee kunufaika na kuitumikia nchi yetu, naamini jambo hili chini ya Mama Samia litapiga hatua,” amesema Shilole na kuongeza.

“Mimi naipenda nchini yangu, nampenda Rais wangu Mama Samia Suluhu Hassan, ndiyo maana tunamshukuru Mwenyezi Mungu tumepata Rais wa kwanza mwanamke, kwa hiyo ni lazima tujivunie kuwa naye,” amesema Shilole.

Ikumbukwe Shilole ni miongoni mwa mastaa wenye nguvu kubwa ya ushawishi kwenye mitandao ya kijamii akiwa ndiye msanii wa pili wa kike wa Bongo Fleva mwenye wafuasi (followers) wengi Instagram akiwa nao milioni 10.4.

Naye muigizaji Kulwa Kikumba ‘Dude’, amemuomba Rais Samia kuwasaidia wasanii kupata wakufunzi wenye uwezo mkubwa kutoka nje ambao watawapiga msasa na kufanya nao kazi ili waweze kupiga hatua katika soko la kimataifa.

“Mama aliahidi kuleta wakufunzi wa masuala ya sanaa hasa upande wa uigizaji. Nakumbuka kipindi cha uzinduzi wa filamu ya Tanzania: The Royal Tour’ pale Arusha nilikuwepo, yule Director Peter Greenberg, alisema kuna wakufunzi watakuja,” alisema.

“Kwa hiyo tunataka tumkumbushe Rais Samia kwamba kuna watu tayari walishajitoa,  kuja kufanya kazi hapa na wengine kutoa mafunzo, basi wale tunawahitaji kwa haraka waje watusaidia,” amesema Dude.

Dude ameendelea kwa kusema, “Tunatamani kwa muda wote wa Rais Samia uliobakia walau wasanii wachache kutoka hapa nchini wawe wamefanya kazi za kimataifa,”.

Utakumbuka Dude ndiye msanii pekee wa filamu Bongo aliyefanikiwa kufika kilele cha mlima Kilimanjaro Oktoba 2019, katika kampeni ya kutangaza utalii ‘Kili Challenge Twenzetu Kileleni’ iliyoandaliwa na Wizara ya Maliasili na  Utalii.

Kwa upande wake Staa wa Malaika Music Band, Christian Bella amesema anatamani kuona wasanii wanapata sehemu nzuri ya kufanya matamasha yao pamoja na haki zao ziendelee kulindwa.
“Tupate Arena nzuri ya kisasa ya kufanya maonesho yetu na haki za wasanii zipatikane na hiyo ni kwa upande wa filamu, sisi wanamuziki, watu wa ngoma, muziki wa asili ,” amesema Bella.

“Serikali ijaribu kuangalia upande huo kwa sababu kuna haki zetu tunazikosa, hata namna ya uuzaji wa kazi zetu, tusipopewa mwanga na serikali msanii atakufa akiwa masikini, tunahitaji msaada kutoka kwao, wasanii wawe wanapata haki zao inavyotakiwa,” amesema.

Bella kutokea DR Congo aliyefanya muziki nchini kwa miaka zaidi ya 10, aliingia rasmi kwenye muziki akiwa na umri wa miaka 15, ambapo alikuwa kiongozi wa bendi ya Chateau, iliyokuwa ikimilikiwa na Frank ambaye alikuwa mshirika wa karibu na Papa Wemba.

Naye Kala Jeremiah msanii wa Bongo Fleva, ambaye alishika nafasi ya nne katika shindano la Bongo Star Search (BSS), 2006 na mshindi wa tuzo tatu za TMA 2013, amesema wasanii wanatamani kuona Rais Samia akienda kwa mwendo huohuo wa sasa ambao umewanufaisha.

“Ni kuendelea tu kwenda na huu mwendo anaokwenda nao, sioni kama kuna sehemu ya kuboresha sana ni kwenda na mwendo huu wa kuzidi kuibeba sanaa yetu, kuwapenda wasanii na kuwathamini wao pamoja na mchango wao katika jamii, hivyo aendelee na moyo huo tu ndicho ninachoweza kusema,” amesema Kala.

Mwaka 2005, ndipo Kala Jeremiah alirekodi wimbo wake wa kwanza, ni katika studio ya Ujumbe Records iliyokuwa Mwanza Jengo la Chama cha Mapinduzi (CCM) na Prodyuza aliyesimamia kazi hiyo anaitwa Brother John. Wimbo wake, Dear God (2013) ndiyo ulimpa mafanikio makubwa zaidi katika sanaa yake.