Huyo ndio Rais Samia wa wasanii Tanzania

Muktasari:

  • Rais Samia aliingia madarakani Machi 19,2021, akiwa ni mwanamke wa kwanza kushikilia wadhifa huo tangu nchi ilipopata uhuru mwaka 1961, utawala wake unatajwa na wengi kuleta neema kubwa upande wa sanaa na burudani.

Ikiwa inaelekea kutimia miaka mitatu tangu Rais Samia Suluhu Hassan kuingia madarakani, wasanii wa muziki na filamu nchini wamebainisha na kushukuru yale mazuri aliyoifanyia tasnia yao kwa kipindi hicho.

Rais Samia aliingia madarakani Machi 19,2021, akiwa ni mwanamke wa kwanza kushikilia wadhifa huo tangu nchi ilipopata uhuru mwaka 1961, utawala wake unatajwa na wengi kuleta neema kubwa upande wa sanaa na burudani.

Mathalani kurejesha tuzo za muziki Tanzania (TMA), ambazo zilikuwa zimesimama tangu mwaka 2015, ila tangu amekuwepo madarakani serikali imetia mkono kuwezesha utolewaji wa tuzo hizo ambazo sasa zinaenda msimu wa tatu.

Wakizungumza na gazeti hili, wasanii mbalimbali wamesema ndani ya muda mfupi Rais Samia amefanya mabadiliko makubwa ambayo moja kwa moja yameenda kuwagusa wao na sanaa yao na kuna matarajio ya mambo mazuri huko mbeleni.

Miongoni mwa waliopata fursa ya kuidaduvua miaka mitatu ya Rais Samia madarakani ni pamoja na Kala Jeremiah, Dude, Christian Bella, Shilole, Mwasiti na Jacob Stephen (JB).
 
 

Kala Jeremiah

Msanii wa Hip Hop, Kala Jeremiah amesema miaka mitatu ya Rais Samia madarakani imeonekana siyo kwa wasanii pekee, bali kwa wadau wote wanaofuatilia sanaa, kwani amehakikisha wasanii na sanaa yao vinakua kwa pamoja. 

“Kwa mara ya kwanza kumekuwa na mikopo ya wasanii, kwamba msanii anapokopeshwa ili aendeshe kazi zake za sanaa, haijawahi kutokea, ndiyo imetokea kwa mara ya kwanza chini ya uongozi wake, na pia tumeshuhudia ulipwaji wa mirabaha,” amesema.

                      

“Vilevile ni shabiki wa muziki, mara kadhaa ametaja hadharini nyimbo anazozipenda, hata mimi aliwahi kusema wimbo wangu ‘Kijana’ ni mzuri na nyimbo kama hizo ndizo zinahamasisha vijana kufanya kazi, ndiyo uzalendo wenyewe,” amesema Kala.

Kala amesema ukiona Rais anafuatilia kwa ukaribu namna hiyo na kujua wimbo gani umetoka na una maudhui gani, ina maana yupo karibu na sanaa, na huo ni uthibitisho kuwa anapambana kuhakikisha kazi zao zinakaa sehemu nzuri zaidi.

Kuhusu changamoto zao, Kala amesema changamoto kubwa ni uwekezaji katika sanaa, maana unakuta msanii ana kipaji kizuri au ana mradi anaotaka kuufanikisha, ila hana fedha, lakini kupitia mfuko wa sanaa ulioanzishwa na Rais Samia mambo yanaenda vizuri.

“Changamoto kubwa niliyokuwa naiona kwenye uendeshaji ni hiyo, ila sasa inaweza kutatuliwa kupitia mfuko wa sanaa,” amesema Kala na kuongeza

“Lakini pia mirabaha ambayo huko nyuma tulikuwa hatupati, sasa kuna utaratibu wa kukusanya mirabaha na inatufikia wasanii. Hizo ni fedha ambazo zamani nilikuwa najiuliza zinaenda wapi na kwa nini zilikuwa hasikusanywi?” amesema Kala.
 
 

Dude

Muigizaji mkongwe, Dude amesema kitendo cha Rais Samia kushiriki katika filamu ya The Royal Tour, kimekuwa na athari chanya katika tasnia ya filamu nchini, kwani wanatarajia fursa nyingi za kimataifa.

“Kwa sisi wasanii tulikuwa tumeitafuta sana hiyo nafasi, hasa upande wa location, vitu vingi vilivyoonekana kule vitawavutia watengeneza filamu wengi duniani kuja kuangalia location na kuna ambao tayari wameshaanza kuja,” amesema.

“Hivyo sisi wasanii tuna nafasi kubwa ya kushirikishwa katika kazi zote ambazo zitakuja kufanyika hapa, watakapohitajika waigizaji au wasaidizi wa hizo kazi, basi tuna nafasi kubwa sisi kushiriki, hivyo Rais Samia kwa upande wetu katusogeza,” amesema Dude.

Amesema katika wizara ambazo zinaigusa moja kwa moja tasnia yao kama Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, na ile Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Rais Samia amewawekea watu ambao wanaijua na kuiweza kazi hiyo.


                      

“Rais ametuwekea watu ambao walikuwepo huku au wanaoijua tasnia kwa undani, mfano Nape Nnauye tuliwahi kuwa naye akaondoka, lakini bado tunafanya naye kazi, unajua Nape pia ni mwanamuziki, anapiga vyombo, anaimba, pia Mwana FA ni mwanamuziki na ni kiongozi,” amesema.

“Kwa hiyo kutuwekea mawaziri wanaojua sanaa, hapo Rais Samia amefanya kitu bora zaidi, ndiyo maana unaona wenzetu wa muziki wanazidi kupaa, hata sisi tunajikongoja, tunaleta waigizaji wa kimataifa tunafanya kazi,” amesema Dude.

Amesema kutokana na hilo, sasa tamthilia zimekuwa nyingi tena nzuri hadi zimerudisha mashabiki wa Kitanzania kutazama muvi zao, kwa hiyo Rais Samia anastahili kupongezwa, maana amefanikiwa kuwarudisha kwenye mstari ndani ya miaka mitatu hii. 
 

Christian Bella
Mwimbaji Christian Bella amesema kipindi cha uongozi wa Rais Samia wasanii wamekuwa karibu zaidi na Serikali kwa kualikwa kwenye matamasha waliyoyaratibu kwa ajili yao na pia kupewa mialiko ya kutumbuiza katika hafla mbalimbali.

“Na mara nyingi tunapata ushauri kutoka kwa Rais Samia ambaye amekuwa akituunga mkono, amejitahidi kutuletea watu sahihi kabisa ambao tunasikilizana vizuri kuanzia Baraza la Sanaa Taifa (Basata), hadi Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo,” amesema.


                     

“Pale wizarani ametuwekea Mwana FA ambaye alikuwa mwanamuziki na anajua changamoto gani tunapitia kama wasanii, imetusaidia sana kutatua matatizo madogo madogo ambayo tunayo,” amesema Bella.

Amesema kutokana na mazingira mazuri yaliyowekwa na Rais Samia, wasanii wamekuwa na vikao kuhusu uuzaji wa kazi zao, namna gani ya kupata haki zao, vikao ambavyo ziliwawezesha kuanza kupata mirabaha kama wasanii wa nchi nyingine zilizoendelea.

“Unajua zamani hii mirabaha ilikuwa hamna ila sasa ipo, ni hatua kubwa sana kwa sababu nchi nyingine walikuwa wanaipata ila sisi tu ndiyo ilikuwa bado, naona huko mbele mambo mazuri yanakuja,” amesema.

“Upande wa changamoto bado sijaona maana hana muda mrefu madarakani, unajua alipoingia kuna mifumo mingi ambayo ameianzisha upya, kwa hiyo alikuwa na kazi kubwa, hivyo tuzidi kumpa nafasi mambo mazuri zaidi yanakuja,” amesema Bella.
 
 

Shilole

Mwanamuziki na muigizaji Zuwena Mohammed, maarufu kama Shilole, amesema tangu Rais Samia ameingia madarakani imekuwa neema kwa wasanii, kwani kwa sasa wanaaminika kufanya kazi kwenye taasisi mbalimbali.

“Tangu mama Samia ameingia madarakani imekuwa neema kwetu sisi wasanii,  maana tumeweza kuaminika zaidi katika nafasi mbalimbali kuitumikia nchi yetu, taasisi zinatuamini zaidi kufanya kazi, kwetu sisi haya ni maendeleo makubwa na tunaona kama fursa kwetu,”  amesema 

                       

Shilole amemalizia kwa kusema haoni changamoto, kwani kwa sasa fursa ni nyingi nchini, hasa za kiuchumi cha zaidi ni watu kuitumikia nchi.


Mwasiti

Mwanamuziki Mwasiti Almasi ( Kipepeo Mweusi),  kwa upande wake ameeleza kuwa katika miaka mitatu ya Rais Samia anaona mafanikio ni makubwa muziki ulipo ni tofauti na mwanzo kwa sababu serikali kwa sasa inaona muziki kama sehemu ya mapato.

 “Kwa wasanii kwa sasa kuna mafanikio yanayoonekana na yasiyoonekana, ambayo yanaonekana kuna ulipaji wa kodi kama wanavyokatwa wafanyakazi.

“Pia serikali inatuangalia, mwanzo kuna vitu tulikuwa hatuvielewi kwenye Basata na Cosota, lakini sasa ofisi hizo mbili zimekuwa zinafanya kazi mpaka wasanii tunashangaa,” amesema Mwasiti.

Hata hivyo, ameeleza kuwa mabadiliko hayo yanaonekana kutokana na awali ilikuwa msanii akiitwa Basata inakuwa ni kufungiwa wimbo, hivyo walipachukulia kama mahakamani, kwa sasa sehemu hiyo imekuwa ikiwaweka chini na kuwapatia elimu.

Mbali hayo, anasema amefurahishwa na kauli ya Rais Samia ya kujenga Arena kwa sababu itawasaidia katika kuburudisha watu wengi kwa pamoja.


                      

“Rais kasema anatuwekea Arena, itakuwa ni jambo kubwa sana, Tanzania hatuna sehemu kubwa ya kufanyia show ambayo itaweza kuingiza watu wengi, kutuletea Arena tutakuwa na uwezo wa kujaza ili watu wapate burudani kwa uhuru zaidi pamoja na sisi kujipatia kipato kama wasanii na serikali kujipatia mapato kupitia kodi,” amesema.

Upande wa changamoto, Mwasiti amesema bado wanapitia changamoto kwenye kupata uhuru wa kufanya kazi kama wasanii katika baadhi ya maeneo.

“Kuna changamoto ya kupatiwa uhuru kama msanii anataka kufanya kazi, kama vile sehemu ya jeshi,  mahakamani, kuomba sehemu ‘kushuti’ bado kuna changamoto,  wakiturahisishia kwa ukubwa hata ubunifu utakuwa mkubwa zaidi na hatuwezi kufanya hivyo bila ya kupewa uhuru zaidi,” amesema Kipepeo Mweusi.
 
 

Jacob Stephen (JB)


                     

Aidha muigizaji wa Bongo Movie, JB kwa upande wake ameeleza katika miaka mitatu ya Rais Samia mafanikio yapo, wasanii wanafanya kazi kwa amani kwa sababu nchi imetulia.

“Kwa sasa tunafanya kazi kwa amani kwa sababu nchi imetulia na mikopo ya mama wasanii wamepata, masoko yameongezeka, pia ni pongezi ya mama kwenye sinema aliyofanya imefungua milango kwa sababu kuna maongezi yaliyofanyika na kuna wasanii ambao watakuja kufungua studio,” amesema JB.