Kuna nini kati ya Rushayna na Ndaro?
Muktasari:
- Tetesi zilizokuwa zikisambaa kwa miezi kadhaa sasa zimezidi kupata nguvu baada ya mwandishi wa Mwanaspoti kuwakuta wawili hao wakitoka kufanya manunuzi Mlimani City, Dar es Salaam.
Dar es Salaam. Zaidi ya miaka mitatu tangu kuvunjika kwa ndoa yake na aliyekuwa Ofisa Habari wa Simba na Yanga, Haji Manara, Rushayna ameibua tena gumzo baada ya kuonekana akiwa karibu na mchekeshaji maarufu, Ndaro.
Tetesi zilizokuwa zikisambaa kwa miezi kadhaa sasa zimezidi kupata nguvu baada ya mwandishi wa Mwananchi kuwakuta wawili hao wakitoka kufanya manunuzi Mlimani City, Dar es Salaam.
Walipoulizwa kama ukaribu wao umeishia kwenye urafiki au tayari umegeuka kuwa uhusiano wa kimapenzi, hakuna aliyetoa jibu la moja kwa moja. Badala yake, walionekana kucheka na kukwepa kulizungumzia kwa uwazi.
Hata hivyo, Ndaro hakuficha hisia zake kuhusu Rushayna.
"Hakuna ubaya kuwa na mwanamke kama Rushayna. Kama ni kweli, basi mimi nimebahatika kuwa naye," amesema huku akiongeza kuwa anampenda sana Rushayna.
Kwa upande wake, Rushayna hakukanusha wala kuthibitisha tetesi hizo.
"Ndaro ni mtu wangu wa karibu sana... nampenda sana," amesema kwa tabasamu.
BIRTHDAY YACHOCHEA
Dalili za ukaribu wa wawili hao zilianza kuonekana wazi Juni 17, 2026, Ndaro alipompongeza Rushayna katika siku yake ya kuzaliwa kupitia ukurasa wake wa Instagram.
Akiambatanisha ujumbe huo na video zilizowaonyesha wakiwa pamoja katika nyakati mbalimbali, aliandika: "Moja ya watu wanaonipinga kuwa na matumizi mabaya ya fedha kila siku, wanaopigania furaha yangu ya kila siku. Wanamuita Rushayna ila mimi nakuita Rundaro. Happy Birthday to you Queen."
Ujumbe huo uliibua maelfu ya maoni, huku wengi wakiamini kuwa ulikuwa ishara ya uhusiano wa zaidi ya urafiki.
Kwa sasa, watu wanaodaiwa kuwa karibu na wawili hao wanasema ukaribu wao umeongezeka kwa kasi, ingawa hakuna aliyethibitisha rasmi madai hayo.
KUTOKA YOGO BEATS HADI HAJI MANARA
Safari ya mapenzi ya Rushayna imekuwa ikivuta hisia za wadau wa burudani kwa miaka kadhaa.
Kabla ya ndoa yake, aliwahi kuwa kwenye uhusiano na mtayarishaji wa muziki, Yogo Beats.
Baadaye akawa kwenye uhusiano na Haji Manara, uliofanikisha ndoa iliyofungwa Septemba 26, 2022.
Hata hivyo, ndoa hiyo haikudumu kwa muda mrefu na kufikia Januari 2023 wawili hao walitengana baada ya Rushayna kupewa talaka.
Sasa, miaka mitatu baadaye, jina la Ndaro limeanza kuhusishwa na ukurasa mpya wa maisha yake ya mapenzi, huku mashabiki wakisubiri kuona kama safari hii tetesi hizo zitageuka kuwa uhusiano rasmi.