Kwa Barnaba ni kazi tu kama Burna Boy
Muktasari:
- Utakumbuka tangu Barnaba ametoka kimuziki chini ya Tanzania House Talent (THT) amekuwa akifanya vizuri na ametoa albamu tatu, Gold (2018), Refresh Mind (2020), Love Sounds Different (2022) pamoja na EP moja, Mapenzi Kitabu (2020).
Dar es Salaam, Staa wa Bongo Fleva, Barnaba amesema wasanii wa muziki huo bado wana nafasi kubwa ya kufanya vizuri kimataifa kama ilivyo kwa Burna Boy ikiwa kazi ndio zitaongeza zaidi na kuacha kulalamika kwa madai kuna wenzao wanapendelewa.
Utakumbuka tangu Barnaba ametoka kimuziki chini ya Tanzania House Talent (THT) amekuwa akifanya vizuri na ametoa albamu tatu, Gold (2018), Refresh Mind (2020), Love Sounds Different (2022) pamoja na EP moja, Mapenzi Kitabu (2020).
Muziki wake umempatia tuzo kadhaa za muziki Tanzania (TMA), miongoni mwa hizo ni Wimbo Bora wa Zouk/Rhumba (Nabembelezwa) 2011, Msanii Bora wa Kiume 2012 na Albamu Bora ya mwaka (Love Sounds Different) 2022.
Akizungumza na Mwananchi Barnaba amesema yeye hajafanikiwa kutajwa kwenye mambo mengi ya muziki Afrika lakini huwezi kumsikia akilalamika au kuvunjika moyo bali ndio anazidi kufanya kazi kwa bidii.
"Sijatokea sana kwenye tuzo kubwa za Afrika, vijatokea kwenye vitu vikubwa vya Afrika, sijawahi kutawala kwenye vitu vikubwa vya Afrika lakini ni moja ya wasanii wakubwa ambao nafuatiliwa, muziki una nguvu kuliko maneno." amesema Barnaba.
Amesema mshindi wa Grammy kutokea nchini Nigeria, Burna Boy ni mfano wa kuigwa kwa wasanii ambao wanataka kufika mbali kimataifa kwani licha ya kukataliwa bado aliweza kusimama na kuandika historia yake kimuziki.
"Ukifuatilia stori ya Burna Boy unaambiwa watu walimkataa huko kwao Nigeria, walikuwa wanamwambia anakoroma sio mwanamuziki mzuri lakini sasa hivi ndio namba moja Afrika." amesema na kuongeza.
"Ukizungumzia wasanii watatu wakubwa Afrika, Burna Boy namba moja, namba mbili Wizkid, namba tatu Diamond Platnumz, kwa hiyo dawa sio kulalamika, hata kama kuna changamoto ipo fursa ya kupenya." amesema Barnaba.
Ikumbukwe Burna Boy alianza kuvuma Afrika mwaka 2012 baada ya kuachia ngoma yake, Like to Party kutoka kwenye albamu yake, L.I.F.E (Leaving ana Impact for Eternity) iliyokuja kutoka Agosti 12, 2013.
Albamu yake ya tano, Twice As Tall (2020) ilishinda tuzo ya Grammy kama Albamu Bora ya Muziki Duniani, huku akiweka rekodi kama msanii kwanza Nigeria kuwania Grammy mara mbili mfululizo baada ya albamu yake, African Giant (2019) kufanya hivyo awali.
"Na ili kupenya sio maneno, ni kufanya kazi nzuri, kujaribu kubadili lugha na lafudhi kidogo, Kiswahili chetu kinaenda duniani sasa hivi lakini vizuri tuangalie ni jinsi gani tunaweza kufanya watu wengine wa duniani kutuelewa kwa haraka." amesema Barnaba.
Utakumbuka Barnaba ambaye ni mmiliki wa studio, High Table Sound ameshirikiana na wasanii wa kimataifa kama Jose Chameleone, Otile Brown, King Kaka, Khaligraph Jones n.k, huku akiwaandika nyimbo wasanii wa Bongofleva kama Lulu Diva, Ruby, Shilole, Linah, Recho, Vanessa Mdee n.k.