Lulu Diva afunguka kuacha muziki

KUOA ni sheria na kuzaa ni majaliwa yake Mungu, kila mwanamke anandoto ya kuwa mama.
Lakini sio wote wamekuwa wakipata hiyo baraka kama matarajio yao hadi hapo Mungu anapoamua kuwabariki watoto ama mtoto.

Mwananchi limepata nafasi ya kuzungumza na mwanadada anayefanya vizuri kwenye sanaa ya muziki na maigizo Lulu Diva, ambaye amefunguka mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuombewa heri ya kupata mwanaume wa kumuoa kabla hajaombewa kupata mtoto.


Kuzaa ni majaliwa

Kila mwanamke ana ndoto ya kuwa na mtoto lakini kumpata ni mipango ya Mungu kama anavyothibitisha Lulu Diva kuwa muda ukifika ataitwa mama kama wengine.
“Kama kuna watu au mtu ananiombea heri nipate mtoto basi naomba kwanza aniombee heri nipate mume mwenye huruma na mimi nimpate mtoto nikiwa na mume,” amesema na kuongeza;

“Kama ridhiki ya mwenyezi Mungu ameniandikia kuwa na mume basi nikimpata huyo na mtoto atapatikana mimi ni mtoto wa Kiislamu unaponishauri mtoto alafu nizae nje ya ndoa atakosa haki zake kama mimi nilivyozikosa au apitie maumivu kama niliyoyapitia mimi sipo tayari kwa hilo,” anasema na kuongeza:

“Hata mama yangu alikuwa ananiambia ‘sikulazimishi upate mtoto kwa sababu wewe ndio utamzaa na wewe ndio una utayari wa kufanya hivyo’ alikuwa ananiambia hivyo kutokana na matamanio ya kuona mjukuu wake kutoka kwangu,”anasema msanii huyo.


Kufanya upasuaji

Kumekuwa na trendi kubwa ya wanawake kutengeneza miili yao, wapo ambao wanakata utumbo ili kuwa na muonekano wa mwili mdogo, wengine wamekuwa wakiongeza makalio, wengine wanajaza vifua na kuongeza lips za midomo.

Unaambiwa mwanamke shepu, lakini kauli hii siyo kwa wanawake wote kwani Lulu Diva yeye anasema anajikubali jinsi alivyoumbwa.

“Kwanza najikubali namna nilivyo, nitafanya vitu vyote lakini sio kupasua midomo au kuharibu mwili wangu kwa lolote, napenda nywele lakini hata leo hii ukiniambia ninyoe nipo tayari ila sio kufanya upasuaji ili kuwa na mwili mdogo au mkubwa,” amesema na kuongeza;

“Hakuna raha kama kujikubali ulivyo, mabadiliko ya mwili kwa mwanadamu yana madhara yake, kitu ambacho naweza kukifanya kwenye mwili wangu licha ya kuniongezea urembo ni kunyoa tu lakini mambo mengine sioni sababu na haitakuja kutokea,” anasema msanii huyo anayetamba na wimbo wa Andazi uliotoka mwaka jana.


Mwanamitindo

Lulu amekuwa na muonekano wa tofauti kulingana na mazingira, basi unaambiwa sio mtu wa kununua sana nguo dukani, amekuwa ni mtu wa kudizaini mitindo yake na kwenda kwa fundi.

“Mimi naweza kudizaini mashono na nina fundi wangu ambaye amekuwa akifanya kazi hiyo, lakini mimi ndio nachagua nataka hiyo nguo iwe ya aina gani.
“Sio mimi tu natakiwa kushonewa na huyo  fundi nawakaribisha watu wanaotamani kuwa na muonekano wa mavazi kama yangu kuja kushona kwenye ofisi yetu.” anasema.


Kujiandaa saa nne

Kuna kauli kuwa mwanamke unatakiwa kumuambia safari saa mbili au tatu zaidi ukitaka kutoka naye hii imethibitishwa na Lulu Diva kuwa wala hawajakosea kwani hata kwa upande wake anaweza kuambiwa safari saa nne akaanza kujiandaa saa mbili na asitoboe huo muda.

“Napenda kujiandaa vizuri na nikitoka niwe smati na niwe na muonekano wa tofauti, hivyo nikikaa kwenye kabati la nguo naweza kushusha nguo zote na nikajaribu ni ipi itanikaa kwa kutumia zaidi ya saa mbili hadi nne.

“Napenda kuvaa vizuri na kuwa na muonekano wa tofauti mimi ni msichana na ni maarufu kukosolewa ni suala la kawaida, hivyo kukwepa hizo shida natamani kuona nimejiandaa vizuri na kuwapa maswali wakosoaji. Hivi nguo za kwenye kabati ni zile ambazo nakuwa nimezinunua lakini sijavaa hata siku moja,” anasema msanii huyo aliyezaliwa mwaka 1995 na kuongeza.

“Sipendi kurudia nguo mimi napenda nivae mpya na nafurahi nikiwa kwenye vazi ambalo ndio mara yangu ya kwanza kuvaa, ” anasema.


Viatu zaidi ya pea 40

Achana na suala la mavazi ambalo amekiri kuwa ndio ugonjwa wake kutokana na kutumia gharama kwa kuhakikisha anavaa vile anavyotaka lakini pia anavingatia sana suala la viatu .

“Viatu siwezi kutaja idadi kwa sababu ni vingi huwezi kuwa na nguo nyingi halafu ukawa na viatu pea mbili lazima viendane na wingi wa nguo zilizopo kabatini kwasababu nguo zinatakiwa kuendana na kiatu na navaa kwa kuangalia mguuni unataka nini.

“Kwa haraka haraka viatu vyangu ni zaidi ya pea 40 na kuhusu gharama ya kiatu changu ambacho nimenunua bei ghali mmh! sijui,” anasema.


Nywele, nguo hahofii gharama

Mrembo huyo ambaye amekuwa akionekana nadhifu kuanzia mavazi hadi nywele, amesema linapokuja suala la kupendeza huwa hana ubahili kwenye kutoa fedha kwani anapenda kuvaa vitu vizuri na vya gharama.

“Sitaki kuweka wazi ni kiasi gani huwa natumia lakini kwa wanaofahamu mavazi na nywele nzuri wakiniona wanatambua gharama ninazozitumia kuanzia mguuni hadi kichwani, sioni shida kutoa milioni kwa ajili ya nywele au kiatu,” anasema.


Anakumbuka kauli ya mama

Kila mwanadamu amekuwa akipitia mapito mbalimbali kulingana na mazingira anayoishi na changamoto na mafanikio vimekuwa vitu ambavyo vinajenga kumbukumbu kwenye maisha kama anavyofunguka Lulu Diva.

“Kumbukumbu mbaya na ya kuniumiza kwenye maisha yangu ni kauli kutoka kwa mama yangu ambayo bado inaishi kwenye maisha yangu  kwamba nisifananishe kifo na usingizi.

“Mama yangu Mungu aendelee kumpumzisha mahala pema peponi alikuwa na kauli yake hiyo na imekuwa ikiishi kwenye akili yangu hadi leo naikumbuka ,” anasema  Lulu.


Muziki Mmh!, maigizo fresh

Lulu Diva ambaye anafahamika zaidi kwenye nyimbo kama Utamu, Ona, Amezoea, Nilegeze na nyingine amesema anajuta kuchelewa kuingia kwenye sanaa ya maigizo kwani huko ndio kipaji chake halisi kilipo.

Anasema itafika muda ataachana na muziki ili kujikita zaidi kwenye kuigiza ili aweze kuonyesha uhalisia wa kipaji chake alichonacho.

“Ukweli kwa muda mfupi nilioanza kufanya tamthilia nikianza na Rebecca, nimegundua kuwa nilijichelewesha kuingia kwenye sanaa ya maigizo, huku ndio kwenye kipaji changu na nimepata mashabiki wengi sasa kuna Juakali nazidi kuwa bora, sijisifii ila nafurahia kazi nzuri ninayoifanya,” amesema na kuongeza;

“Kutokana na namna ninavyopokea pongezi na kuendelea kukubalika na waandaaji wa tamthilia naona kabisa itafika muda nitahamishia nguvu zangu zote kwenye sanaa na kuachana kabisa na muziki,” anasema.


Nandy muziki fresh

Kufanya kazi ya Mtaalamu ambayo amemshirikisha mwanadada anaefanya vizuri kwenye tasnia ya muziki, Faustina Charles Mfinanga ‘Nandy’ anafunguka kuwa ilikuwa ni ndoto yake.

“Kwenye sanaa ya muziki ndoto yangu ilikuwa ni kufanya kazi na Nandy cha ajabu basi nilivyomuambia natamani kufanya kazi na yeye haikuchukua ata siku nne akanipigia na kuniambia tukutane studio wimbo wa Mtaalam aliniandikia na kunipa na sasa unafanya vizuri nampenda sana,” anasema Lulu.