Mac Voice aanza ukurasa mpya kwenye Bongo Fleva
Muktasari:
- Mac ameachia wimbo huo jambo ambalo limeibua shangwe kwa mashabiki huku wakiipongeza menejimenti yake ya ‘YBL Music’, kwa kufanikisha msanii huyo kurudi tena katika anga za muziki.
Dar es Salaam. Hatimaye mwanamuziki wa Bongo Fleva, Mac Voice amerudi tena katika tasnia ya muziki ambapo ameachia wimbo wake mpya uitwao ‘Hawajui’, baada ya kuwa kimya kwa takribani miaka miwili akiwa chini ya lebo inayomilikiwa na msanii Rayvanny, Next Level Music (NLM).
Mac ameachia wimbo huo jambo ambalo limeibua shangwe kwa mashabiki huku wakiipongeza menejimenti yake ya ‘YBL Music’, kwa kufanikisha msanii huyo kurudi tena katika anga za muziki.
Utakumbuka, mwanzoni wa mwaka huu Mac alitemana na lebo iliyokuwa ikimsimamia ya Next Level Music (NLM) huku akiwema wazi kuwa kupishana kwake na Rayvanny kulitokana na masuala ya fedha tu, yeye aliona kuna kitu alistahili kupata kutokana na muziki wake lakini lebo ikawa inadai hajaingiza fedha.
Machi 2021, Rayvanny alitangaza kuanzisha NLM wakati huo akiwa bado yupo na WCB Wasafi, pia akiwa msanii wa kwanza kutoka katika lebo hiyo ya Diamond Platnumz kufanya hivyo.
Kufikia Septemba 2021, akamtambulisha msanii wa kwanza wa NLM ambaye ni Mac Voice aliyekuja na Extended Playlist (EP) yake, My Voice (2021) yenye nyimbo sita huku Rayvanny akishirikishwa katika nyimbo mbili.
Wimbo uliobeba zaidi EP hiyo na kuliweka jina la Mac Voice juu wakati huo, ni Nenda (2021) uliotayarishwa na Laizer Classic ambaye ametengeneza nyimbo nyingi kubwa chini ya Wasafi Records.
Nenda ni wimbo unaozungumzia maumivu ya kutendwa katika mapenzi na mwanamuziki huyo anaeleza amekubali yote aliyotendewa na mpenzi wake na yupo tayari kumuacha aende zake.
Video yake iliyoachiwa Septemba 29, 2021, imetazamwa zaidi ya mara milioni 20 YouTube na ndio video namba moja kwa Mac Voice katika mtandaoni, yaani iliyofanya vizuri zaidi kwa muda wote.
Kwa jumla EP yake ilipata mapokezi mazuri ikimtambulisha kwa staa mkubwa ajaye katika Bongo Fleva ambaye anaiwakilisha lebo changa ya mwanamuziki mkubwa aliyeamua kuwekeza kwa nguvu zote.
EP hiyo ndani ya mwezi mmoja tu ilisikilizwa (streams) zaidi ya mara milioni 1 katika mtandao wa Boomplay Music na hadi sasa imefikisha milioni 39.1. Ukija YouTube alipopata wafuasi (subscribers) 100,000 ndani ya muda huo, ilikisikilizwa mara milioni 4.
Kufuatia kufanya vizuri kwa EP hiyo, haikuchukua muda mrefu Mac Voice akawa amechaguliwa kuwania tuzo ya African Entertainment Awards USA (AEAUSA) kama Msanii Bora Chipukizi 2021, tuzo zinazofanyika Marekani.
Tangu hapo jina la Mac Voice limekuwa si ngeni tena katika kiwanda cha Bongo Fleva huku wasanii wakubwa akimtabiria makubwa siku za mbeleni.
Mmoja wapo ni Diamond ambaye alimwita 'Mjukuu wake' akiwa na maana kuwa Mac Voice ni tunda la msanii aliyemtoa chini ya WCB Wasafi ambaye ni Rayvanny.
Diamond alieleza kuikubali sana kolabo ya Mac Voice na Mbosso, Only You (2022) ambayo hadi sasa video yake imetazamwa YouTube mara milioni 6.9, ukiwa ni mradi wake namba mbili kupokelewa vizuri zaidi katika mtandao huo.
Baada ya mfululizo wa nyimbo kali na kolabo kadhaa, ghafla Mac Voice akawa kimya, si kimuziki tu hata kwenye mitandao ya kijamii, mathalani Instagram posti yake ya mwisho iliwekwa Juni 9, 2024.
Na wimbo wa mwisho kuachiaakiwa na lebo ya NLM ni Mapenzi na Pesa ulitoka Mei 19, 2024 akiwa amemshirikisha Meja Kunta, staa wa Singeli Bongo.
Wakati mashabiki wakijiuliza nini kimemkumba hadi kukaa zaidi ya mwaka mmoja bila kutoa kazi mpya, ndipo Machi 2025 akaonekana akifanya show za 'chaka to chaka' ambazo muda mwingi hufanyika hadi vijijini.
Lilikuwa jambo la kushangaza kwa sababu ya umaarufu wa lebo anayotokea, na ukizingatia mara nyingi show za aina hiyo hufanywa hasa na wale wasanii ambao tayari wamekubali muziki wao umeshuka.
Rayvanny alipoulizwa kuhusu jambo hilo, alisema atakaa na menejimenti yake na kutoa tamko lakini tayari tukio hilo lilishaonyesha kuwa wawili hao kila mmoja ameshika njia yake kibiashara.
Katika mahojiano yake mapya, Mac Voice anadai uamuzi huo ulitokana na NLM kutokuwa tayari kumhudumia kiuchumia hadi kufikia hatua ya kushindwa kumudu mahitaji yake ya msingi.
Ikumbukwe kabla ya kusaini NLM, Mac Voice tayari alikuwa ameshasikika kwenye Bongo Fleva kwa uchache sana, ni wakati akiwa chini ya usimamizi wa Chege, mwanachama TMK Wanaume Family.
Lakini kukua kwa jina lake, na hata kutoa kazi kubwa na maarufu, ni chini ya NLM na kusema kweli Rayvanny alionyesha dhamira kubwa ya kufanya kitu cha kipekee kama jina la lebo linavyojieleza.
Hadi Mac Voice anaipa kisogo NLM, tayari alikuwa amefanya kolabo tano na Boss wake huyo ambazo ni Tamu (2021), Bora Peke Yangu (2021), Pombe (2021), Muongeze (2022) na Mwambieni (2023).
Hata hivyo safari yake ilikuwa fupi katika lebo hiyo na kwasasa ameamua kuanza moja kwenye kila kitu kwani hata ile akaunti ya Youtube aliyokuwa akiimiliki akiwa NLM hayuko nayo tena na sasa amefungua akaunti mpya ijulikanayo kama ‘Mack Voice’.