Marioo karudia kwa Nameless alichofanya kwa AY, Mr Nice
Muktasari:
- Ni wazi kuwa Marioo ni kati ya wasanii wachache ambao wameendelea kukuza chapa yao bila kurudi nyuma tangu ulimwengu ulipowafahamu.
Dar es Salaam. Kwa sasa ana miaka nane kwenye gemu ya muziki. Tangu pale ulimwengu ulipomuamini alipoachia kibao chake 'Dar Kugumu' (2018). Ni Marioo aliyeanza kung'aa baada ya kurudia wimbo wa mwanamuziki Lameck Ditto 'Moyo Sukuma Damu' (2016) hadi kumfanya Ruge Mutahaba ampe nafasi ya kunoa kipaji chake pale THT.
Ni wazi kuwa Marioo ni kati ya wasanii wachache ambao wameendelea kukuza chapa yao bila kurudi nyuma tangu ulimwengu ulipowafahamu. Na hadi sasa mkali huyu tayari ana albamu mbili The Kid You Know (2022) na The Godson(2024) huku akiwa na ngoma nyingi zilizotikisa nchi.
Hata hivyo, msanii huyu ameendelea kuthibitisha kuwa ukuaji wake kimuziki haujaja kwa bahati mbaya. Bali ni matokeo ya kuwa na mikakati ya kibiashara ikiwemo kushirikiana na wasanii wakongwe waliotengeneza historia Afrika Mashariki.
Kama alivyofanya kwa AY katika wimbo wake 'Yule Remix' waliotoa pamoja mwaka 2024. Yule ni wimbo wa AY ambao ulitoka mwaka 2005, hata hivyo, Marioo aliona kuna haja ya kuongeza sauti kwenye wimbo huo ndipo aliposhirikishwa na AY katika remix yake.
Ikumbwe AY alifika Dar kwa mara ya kwanza mwaka 1999 kwa lengo la kuja kupambania kipaji chake cha muziki.
Marioo hakuishia hapo akatupia kionjo cha wimbo wa Mr Nice 'King'asti' kwenye wimbo wake 'Shisha'. King'asti uliotoka zaidi ya miaka 18 iliyopita, hivyo miaka miwili iliyopita Marioo akamvuta Mr Nice na kutupia mistari hiyo kwenye wimbo wake mpya.
Baada ya kufanya kazi na wakongwe hao, Marioo akavuka mipaka ambapo mapema mwaka huu akazama nchini Kenya na kutupia maneno yake kwenye wimbo wa Nameless 'Nasinzia'. Wimbo huo halisi ulitoka zaidi ya miaka 17 iliyopita lakini kwa sasa umerudiwa na kuwa mpya.
Kupitia kolabo hizi, Marioo anaendelea kujijengea heshima kwa mashabiki wa rika zote. Huku hatua hii ikimfanya kuwa miongoni mwa wasanii wanaoheshimu misingi ya muziki wa Bongo Fleva jambo linalozidi kuipanua chapa yake na kumuweka katika nafasi za juu zaidi kwenye soko la muziki.