Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Master J afichua sababu kinafanya achukiwe

Muktasari:

  • Master J ambaye alianza uzalishaji muziki mwaka 1996 baada ya kumaliza masomo ya chuo kikuu ameliambia Mwananchi kitendo cha kuweka vyeti kabatini kilifanya asizungumze na baba yake kwa zaidi ya miaka minne

Dar es Salaam. Wanasema maisha ni kuchagua na hivyo ndivyo alivyofanya mzalishaji wa muziki mkongwe nchini na mwanzilishi wa MJ Production ‘MJ Records’, Joachim Marunda ‘Master J’ ambaye licha ya kupata Shahada ya Uhandisi wa Umeme chuo kikuu cha London aliamua kuweka kabatini vyeti vyake na kuutumikia muziki.

Master J ambaye alianza uzalishaji muziki mwaka 1996 baada ya kumaliza masomo ya chuo kikuu ameliambia Mwananchi kitendo cha kuweka vyeti kabatini kilifanya asizungumze na baba yake kwa zaidi ya miaka minne.

“Mzee hakufurahi hatukuongea kama miaka minne, mitano. Ilifika muda akanifukuza nyumbani haikuwa suala la kufurahia. Hakukuwa na biashara ya muziki, kwanza hata redio hazikuwapo.  

“Hata Radio One ilipoanza walikuwa hawapigi nyimbo za kwetu kwa sababu quality ilikuwa chini sana. Lakini alivyokuja Master T ndiyo akafosi sana ili waanze kupiga muziki yetu, ndiyo kidogo kidogo ikaanza kupigwa,” anasema.

Anasema kwa kuwa muziki haukuwa biashara kwa kipindi hicho ndiyo maana baba yake alichukizwa na alichofanya.

“Nimesoma mpaka Ulaya ilikuwa ngumu. Alilaumu lakini ndiyo ilikuwa passion yangu. Kusoma haikuwa passion yangu nilifanya tu kwa sababu mzee amelipia ada. Kipindi hicho kulikuwa hakuna hata kompyuta tulikuwa tunarekodia kwenye tepu mambo ya kompyuta yalikuja baadaye.

“Hali hiyo haikuwa tu Tanzania ni kote na hata Wakongo walikuwa wanaenda kurekodi Ufaransa, kwa ajili ya ubora. Kwetu sisi hakukuwa na mtaji wa kwenda,” anasema.

Mkali huyo ambaye vijana wa kileo wanamuita ‘Kifimbo Cheza’ anaongezea kwa kudai yeye ndiye alikuwa mtu wa kwanza  kutumia  kompyuta  kwenye kazi.

“Lakini kompyuta ilikuwa kwa ajili ya kutengeneza biti tu. Haikuwa na uwezo wa kurekodi sauti. Nilitoka nayo chuo Uingereza.  Mtu wa kwanza kuja kurekodi kwa kutumia kompyuta alikuwa Mzee Muta ambaye alimwajiri Miikka Mwamba mwaka 2001,” anasema. 

Utakumbuka awali Miikka alikuja nchini akitokea Finland  kwa ajili ya kufanya mafunzo kwa vitendo (field) baada ya kuhitimu Chuo Kikuu aliposomea sanaa. Akiwa hapa alifanya kazi kwa ukaribu na marehemu John Komba katika bendi ya TOT.

Wimbo wa Dully Sykes ‘Julieta’ ndio ulimtambulisha Miikka katika Bongofleva kisha wasanii wengine kama Daz Nundaz, Saida Karoli, Mad Ice, Dudu Baya, Banana Zorro, Hardmad n.k nao wakaenda kurekodi kwake na nyimbo zilizofanya vizuri.


Vita ya Gen Z na Master J

Hata hivyo kumekuwa na tabia kwa baadhi ya vijana wa kileo ‘Gen Z’ kumshushia maneno ya lawama, kejeli na matusi mkongwe huyo kila anapojaribu kutoa mitazamo yake kuhusu muziki. Akizungumzia hilo anasema sababu kuu ya  watu kumpinga ni chuki.

“Watu wana chuki na mimi kwa sababu nasema ukweli kuhusu wasanii wao. Hawapendi naongelea mpaka mapungufu lakini mimi siyo kama nachukia, naongea ili tuboreshe. Kwa hiyo kila msanii ambaye nitamuongelea kwenye mapungufu wanachukia na kutukana.

“Mimi nawasema mpaka Gen Z. Kwa hiyo hainisumbui nitaendelea kuongea ukweli sasa hivi imefika sehemu hata nikisema ‘maji’ kwa kiingereza yanaitwa ‘water’  watu watabisha. 
Nimefikia hapo wanasema huyu Master tahira hajui chochote. Ndiyo maana sikasiriki hata watu wakitukana, sifuti komenti kwa sababu naelewa,” anasema. 

Aidha katika hilo hakuacha kugusia tamko la mkongwe wa muziki nchini Juma Nature ambaye hivi karibuni video zake zilisambaa akidai Master Jay hakuwa producer bali alikuwa na vifaa tu.

“Watu wanabisha kwamba sijawahi kuzalisha kazi inabidi nicheke kama Juma Nature, alibisha na Gen Z  wakamsapoti. Lakini naelewa kila mtu ana hasira zake,” anasema.

Master anasema hana mpango wa kuzalisha kazi yoyote ya muziki tena, kwani alishastaafu muziki tangu mwaka 2008. Lakini atafungua lebo ambayo itakuwa inaendeshwa na vijana kwa ajili ya wasanii. 


Pesa ya Sugu iliishia Bar

Anasema pesa kubwa aliyowahi kulipwa kwa kipindi hicho ilitoka kwa mkongwe wa muziki wa hip-hop  Sugu ambayo nayo iliishia kwenye starehe.

“Sugu alinilipa Sh10 elfu kwa kila wimbo. Albamu nzima ya ‘Ndani ya Bongo’ 1996 ilikuwa na nyimbo kumi akanipa laki. Lakini  tuliitumia yote ndani ya usiku mmoja kwenye starehe.

“Na albamu mpaka ikamilike tulikuwa tunatengeneza ndani ya miezi sita hela yote iliisha. Kuna sehemu moja tuliendea kwenye starehe nilikuwa na yeye Sugu kazi tulikuwa tunafanya kwa ajili ya mapenzi,” anasema.


Bongo Fleva baada ya miaka kumi

Master anasema anauona muziki wa Bongo mbali ukilinganishwa na walivyoanza wao.

“Tutafika tumetoka mbali, shida ni tunapenda kujilinganisha. Wakenya walikuwa tayari wametupita lakini sasa hivi tumeshawapiga bao. Vitu vimebadilika sasahivi tunawatafuta Wanigeria.

“Mwanzo ilikuwa tunapambana kuwa best East Afrika. Mimi naamini baada ya miaka kumi tutakuwa, sawa na Wanigeria. Mimi naangalia tulipotoka miaka ya 1990 maisha ni kupambana wanaenda vizuri,” anasema Master.


Haijui shida

Simulizi za wakili wengi kwenye kiwanda cha muziki. Zimejaa maisha ya shida walizowahi kuzipitia kabla ya kutoboa. Lakini hilo ni tofauti kwa Master ambaye anasema hajawahi kupitia shida kwenye maisha yake.

“Mimi na P Funk hatujakua kwenye shida. Tulizaliwa katika familia nzuri. Mimi baba yangu alikuwa Mkurugenzi Tanesco na mama yangu alikuwa Mkuu wa UNDP Southern Africa yote. Maisha ya shida sijawahi kupitia nisiwe muongo,”anasema.

Licha ya kutokuwa na kumbukizi za dhiki kama ilivyo kwa wengi, anakumbuka vioja alivyowahi kuvishuhudia enzi za uzalishaji muziki.

“Kwenye kurekodi bendi utaona mengi. Mtu anataka kurekodi mara anaanza kulia kama mbuzi, mwingine kila akijaribu kuimba anakohoa mara anatoa panzi. Hayo ni mambo nilikutana nayo nikasema muziki wa Bongo ni mgumu.

“Kwenye studio yangu ya MJ Record, nilikuwa na studio tatu ya kurekodi bendi, kwaya na taarab, nimeona vitu vingi sana  huyo mtu aliyekohoa panzi sitaki hata kumtaja jina. Lakini akisika atacheka,  baadaye alikaa sawa. Na wimbo wake ulifanya vizuri balaa,” anasema .

Anasema anamshukuru sana mama yake kwa sababu alikuwa anampa simulizi za changamoto ambazo alipata. Hivyo kwake hakuna kigeni ambacho kinaweza kumyumbisha kwa sababu mengi amejifunza kutoka kwa mama yake.

“Watu wasionisikiliza waendelee hivyo hivyo. Lazima uishi maisha ukosee ujifunze. Waendelee kupambania ndoto zao kuna sehemu watakosea, wajifunze wasikate tamaa tuachane na mitazamo ya kuangukia pua,” anamaliza Master.

Licha ya hayo yote Master anasema hajawahi kufanya kazi inayoendana na taaluma yake ya umeme ambayo alisomea Ulaya. Aidha mbali na biashara zake binafsi anazofanya  ni jaji katika shindano la kutafuta vipaji vya wasanii wa muziki nchini maarufu kama Bongo Star Search.