Mbinu inayompa Billnass mafanikio kimuziki

Muktasari:

  • Rapa huyo alitoka rasmi kimuziki na wimbo wake, Raha (2014) ambao aliwashirikisha TID na Naziz ambaye mwanachama wa kundi la Necessary Noize kutokea nchini Kenya, huku Rada Entertainment wakisimamia kazi hiyo

Akiwa na miaka 10 ndani ya Bongo Fleva tangu ametoka rasmi kimuziki, Billnass amesalia kuwa yule yule katika mtindo na mbinu za kutoa kazi zake kitu ambacho kimempa mafanikio kwa kuendelea kubaki masikioni mwa mashabiki wengi.

Rapa huyo alitoka rasmi kimuziki na wimbo wake, Raha (2014) ambao aliwashirikisha TID na Naziz ambaye mwanachama wa kundi la Necessary Noize kutokea nchini Kenya, huku Rada Entertainment wakisimamia kazi hiyo.

Hata hivyo, muda mfupi alikuja kuachana na Rada Entertainment kisha kufanya kazi na lebo nyingine kama L.F.L.G (Live First Live Good) na Rooftop Entertainment kabla ya kufungua yake, Mafioso Inc hapo mwaka 2021.

Ni wiki hii Billnass ameachia video ya wimbo wake mpya, Number One (2024) akiwa na Staa wa WCB Wasafi, Mbosso ukiwa ni wimbo wake wa kwanza kwa mwaka huu na wa pili tangu aliposhinda tuzo za muziki Tanzania (TMA) 2022.  

Utakumbuka kolabo hiyo inakuja baada wawili hao kupewa shavu na Whozu katika ngoma yake, Ameyatimba Remix (2023) ambayo video yake ilisababisha wasanii wote watatu kufungiwa na Baraza la Sanaa Taifa (Basata), kutokana na kukiuka maadili.

Kitendo cha Billnass ambaye anafanya Rap kumshirikisha Mbosso ni mwendelezo wa kuhakikisha nyimbo zake zinakuwa na mwimbaji mwenye ushawishi ndani ya Bongo Fleva kitu ambacho kimekuwa na matunda makubwa kwake kama ilivyokuwa kolabo yake na TID.

Nyimbo zake tatu za mwisho kuachia kabla ya huu, Number One (2024) ft. Mbosso, Billnass aliwashirikisha waimbaji wanaofanya vizuri, nyimbo hizo ni Unaonaje (2022) ft. Rayvanny, Puuh (2022) ft. Jay Melody na Maokoto (2023) ft. Marioo.

Kwa asilimia kubwa nyimbo hizo zimempa Billnass mafanikio, mathalani wimbo ‘Puuh’  ulimwezesha kushinda tuzo yake ya kwanza ya TMA, alishinda kama Msanii Bora wa Kiume wa Hip Hop 2022, akiwabwaga Kala Jeremiah, Country Boy, Fid Q na Joh Makini.

Ripoti ya Boomplay Music 2023 ilisema huu ndiyo wimbo wa Bongo Fleva uliosikilizwa zaidi katika jukwaa hilo mwaka uliopita ikiongoza chati kwa wiki sita na hadi sasa umesikilizwa mara milioni 51.9 ukiwa ni wimbo pekee wa Billnass kupata namba hizo.

Kutokana na mafanikio hayo, Billnass ataendelea kufanya kolabo na waimbaji wanaozipa thamani kazi zake, yeye binafsi anaamini mbinu hiyo ndiyo inampa mafanikio na hata alipoachia kolabo yake na Marioo, Julai 2023 iligusia hilo.

“Hii inaenda kuchukua tuzo ya wimbo bora mwaka 2023, wimbo bora wa kushirikiana, video bora ya mwaka 2023, wimbo bora Afrika Mashariki, huu wimbo unaenda kutoa prodyuza bora wa mwaka 2023, director bora wa video 2023” alisema Billnass.

Pengine kuona mbinu hii inampa mafanikio ndiyo sababu hadi sasa hajatoa albamu wala EP licha ya kuwepo kwenye muziki kwa miaka zaidi ya 10 sasa wakati mkewe Nandy aliyetoka miaka miwili baada yake na wimbo wake, Nagusagusa (2016) ameshafanya hivyo.

Nandy aliyefunga ndoa na Billnass mnamo Julai 2020, ameshatoa albamu moja, The African Princess (2018) pamoja na EP tatu, Wanibariki (2021), Taste (2021) na Maturity (2022).  

Msanii mwingine wa Bongo Fleva ambaye alinufaika sana na mbinu hii ni Shetta ambaye nyimbo zake zilizofanya vizuri ni zile alizowashirikisha waimbaji wakali kama Diamond Platnumz, Belle 9, Rich Mavoko, Jux, Tundaman, Dully Sykes, na Marioo.