Mfahamu mchoraji wa picha maarufu ya Mona Lisa, The Last Supper

Muktasari:
- Ni ngumu kuwataja wachoraji mahiri waliowahi kutokea katika ulimwengu huu na kuacha kumtaja Leonardo da Vinci ambaye ndiye alichora picha ya 'Mona Lisa' kati ya mwaka 1503 na 1506 na 'The Last Supper' kati ya mwaka 1495 na 1498.
Italy, Katika historia ya sanaa, wachoraji wengi wameacha alama kupitia kazi zao maarufu walizowahi kuzichora. Hata wale waliofariki dunia bado picha hizo zimeendelea kuwa kumbukumbu kwa wanaozitazama katika ulimwengu wa sasa.
Ni ngumu kuwataja wachoraji mahiri waliowahi kutokea katika ulimwengu huu na kuacha kumtaja Leonardo da Vinci ambaye ndiye alichora picha ya 'Mona Lisa' kati ya mwaka 1503 na 1506 na 'The Last Supper' kati ya mwaka 1495 na 1498.
Leonardo da Vinci ni mmoja wa wachoraji wakubwa katika historia kwani mchoro wake wa 'Mona Lisa' yenye tabasamu la siri, inachukuliwa kuwa moja ya picha maarufu zaidi duniani. Aidha, 'The Last Supper' ni kazi ya sanaa aliyoifanya ikiwakilisha chakula cha mwisho cha Yesu Kristo na wanafunzi wake nayo imekuwa ikitumiwa karne hadi karne.

Picha ya The Last Supper
Licha ya kuwa mchoraji mzuri inaelezwa kuwa Leonardo da Vinci alikuwa pia mhandisi, mvumbuzi na mwanafizikia kutoka Italia ambaye alizaliwa Aprili 15, 1452 na kufariki dunia Mei 2, 1519.
Pia Da Vinci alifanya utafiti katika nyanja mbalimbali za sayansi. Alijishughulisha na anatomia ya binadamu na wanyama, akifanya chunguzi ambazo zilimsaidia kuelewa mwili wa binadamu kwa undani. Alijaribu kuchora picha za misuli, mifupa, na viungo vya ndani, kwa ajili ya kusaidia katika sayansi ya afya.
Alikuwa akiandika na kuchora maelezo mbalimbali katika vitabu vyake, huku akitumia lugha ya siri na alama ili kulinda mawazo yake. Kutokana na michoro na kazi zake zenye kuvutiwa bado zinaendelea kufuatiliwa na kuhamasisha wasanii mbalimbali duniani, hivyo anachukuliwa kama mfano wa wabunifu wa kuigwa.