Miaka 20 ya umaarufu wa Wema Sepetu kupitia Miss Tanzania
Muktasari:
- Miss Tanzania 2006 hadi sasa inapewa heshima kwa kuibua mastaa wenye majina makubwa katika tasnia ya burudani, mbali na Wema, kuna Jokate Mwegelo (mshindi wa pili), Lisa Jensen, Irene Uwoya, Aunty Ezekiel na kadhalika.
Dar es Salaam. Mwigizaji wa filamu Bongo, Wema Sepetu (37), mwaka huu anaadhimisha miaka 20 tangu alipotwaa taji la Miss Tanzania 2006 ambalo limempa umaarufu mkubwa na fursa kibao kwa miaka mingi.
Miss Tanzania 2006 hadi sasa inapewa heshima kwa kuibua mastaa wenye majina makubwa katika tasnia ya burudani, mbali na Wema, kuna Jokate Mwegelo (mshindi wa pili), Lisa Jensen, Irene Uwoya, Aunty Ezekiel na kadhalika.
Huyo Lisa ambaye naye alikuja kuingia katika uigizaji, mwaka 2012 aliteuliwa na kamati ya Miss Tanzania kupitia shindano maalumu (Miss World Second Chance) kushiriki Miss World.
Wema alipokea kijiti cha Miss Tanzania kutoka kwa Nancy Sumari aliyeshinda 2005, na pia alifanikiwa kutwaa taji la Miss World Africa (Continental Queen of Africa) 2005 na ndiye Mtanzania pekee aliyefanya hivyo hadi sasa.
Ikumbukwe mashindano la Miss Tanzania kwa mara ya kwanza lilifanyika mwaka 1967 huku Theresia Shayo akiwa mrembo wa kwanza kutwaa taji hilo, kisha yalisimama kwa muda mrefu na kurejea 1994 ambapo mshindi alikuwa ni Aina Maeda.
Waliofuatia ni Emily Adolf (1995), Shose Sinare (1996), Saida Kessy (1997), Basilla Mwanukuzi (1998), Hoyce Temu (1999), Jacqueline Ntuyabaliwe Mengi (2000), Millen Magese (2001) na Angela Damas (2002).
Wengine ni Sylvia Bahame (2003), Faraja Kotta Nyalandu (2004), Nancy Sumari (2005), kisha Wema Sepetu (2006) a.k.a Tanzania Sweetheart (Kipenzi cha Watanzania) ambaye tunamjadili kwa leo.
Hadi sasa, Wema ndiye anatajwa kuwa mrembo maarufu zaidi kutokea kwenye mashindano hayo ambapo kwa miaka amegonga vichwa vya habari kwa mambo mengi, kuanzia urembo na mitindo, filamu na hata mahusiano yake.
Baada ya kutwaa taji la Miss Tanzania, Wema alishiriki mashindano ya urembo ya dunia (Miss World) yaliyofanyika Warsal, Poland ila hakufanya vizuri ukilinganisha na mtangulizi wake, Nancy.
Miss World ndilo shindano la kimataifa kongwe zaidi la urembo duniani, lilianzishwa mwaka 1951 na Eric Morley nchini Uingereza, na Kiki Hakansson kutokea Sweden ndiye mrembo wa kwanza kutwaa taji hilo.
Baada ya kukabidhi taji la Miss Tanzania, Wema alielekea Malaysia alikosomea Biashara ya Kimataifa (International Business) katika Chuo Kikuu cha Limkokwing. Hata hivyo, hakumaliza masomo yake baada ya kunogewa na uigizaji wa filamu, kitu kilichokuja kumpata umaarufu mwingine baada ya Miss Tanzania.
Wakati yupo Malaysia ndipo filamu yake ya kwanza kucheza ilipotoka, A Point of No Return (2007) akitumia jina la Dina, alicheza na Marehemu Steve Kanumba ambaye ndiye mtu wa kwanza kumuigiza katika filamu.
Wema na Kanumba walicheza filamu nyingine maarufu kama Family Tears (2008), Red Valentine (2009) na White Maria (2010) ambazo ziliweka jina la mrembo huyo sehemu ya juu kabisa upande wa uigizaji.
Lakini ukweli ni kwamba uhusiano wao wa kimapenzi ndio uliomfungulia milango Wema upande wa filamu, kwani Kanumba ndiye alimwambia anaweza kuigiza na kumpa nafasi ya kufanya hivyo.
Wema alifanya vizuri zaidi kupitia filamu yake, Heaven Sent (2017) ambayo ilichaguliwa kuwania vipengele saba katika tuzo za Sinema Zetu International Film Festival Award (SZIFF) ambapo alishinda tuzo mbili. Hadi sasa amecheza filamu zaidi ya 25 akishirikiana na mastaa kama JB, Richie Richie, Lulu, Irene Uwoya, Kajala Masanja, Hemed PhD, Riyama Ally, Aunty Ezekiel, Jacqueline Wolper, Patcho Mwamba, Yusuph Mlela, Gabo na kadhalika.
Hata hivyo, huwezi kuzungumzia umaarufu wa Wema bila kugusia mahusiano yake na mastaa kama Mr. Blue, TID, Kanumba, Chaz Baba, Diamond Platnumz, Idris Sultan, na Whozu ambaye yupo naye kwa sasa.
Uhusiano wake na mwanamuziki Diamond ndio uliokuwa na drama nyingi zaidi licha ya kupendana, ila hilo haliondoi ukweli kwamba Wema alichangia kuiinua chapa ya Diamond akimpatia mashabiki wapya.
Wema alitokea kwenye video ya wimbo wa Diamond, Moyo Wangu (2011), huku Diamond akimtungia wimbo, Lala Salama (2012), na kwa ujumla Diamond amemtaja Wema katika nyimbo zake kama Nimpende Nani (2012), Kesho (2012) na Fire (2017).
Kwa kutambua mchango wake kwake, katika birthday ya Wema mwaka 2014, Diamond alimzawadia gari aina ya Nissan, wakati huo Diamond alikuwa akitamba na wimbo wake 'My Number One' uliomtambulisha kimataifa.
Mnamo Februari 2016, Wema alizindua kampuni yake, Endless Fame Film, na baadaye lebo ya muziki ambayo iliwasaini wasanii wawili, Mirror na Ally Luna.
Hayo na mengine mengi, yamemfanya Wema kuwa maarufu, huyu ndiye mwanamke wa kwanza Tanzania kufikisha wafuasi (followers) milioni 1 katika mtandao wa Instagram ambapo alifanya hivyo mwaka 2015 wakati mitandao ya kijamii ikianza kushika kasi.
Na baada ya miaka saba (2022), Wema akawa wa kwanza tena kufikisha wafuasi milioni 10 Instagram akiwa ni mwanamke wa pili Afrika Mashariki baada ya Zari The Bosslady (Uganda), waliomfuatia Wema ni Lupita Nyong'o (Kenya), Hamisa Mobetto na Shilole (Tanzania).