Mimi Mars atamtosa tena Vee Money?
Muktasari:
- Mimi Mars, mkali wa kibao cha Una (2019) akiwashirikisha Young Lunya na Marioo, hivi karibuni kupitia Vlog yake mpya amethibitisha ujio wa albamu hiyo akisema itakwenda kwa jina la 17.
Dar es Salaam. Mwimbaji wa Bongofleva, RnB na Pop, Mimi Mars (33), a.k.a Chugga Queen anatarajia kuachia albamu yake ya kwanza ndani ya mwaka huu 2026, ikiwa ni miaka takribani tisa tangu ametoka rasmi kimuziki
Mimi Mars, mkali wa kibao cha Una (2019) akiwashirikisha Young Lunya na Marioo, hivi karibuni kupitia Vlog yake mpya amethibitisha ujio wa albamu hiyo akisema itakwenda kwa jina la 17.
Hata hivyo, mwanamuziki huyo ambaye jina lake halisi ni Marianne Mdee, bado haijajulikana iwapo dada yake, Vanessa Mdee a.k.a Vee Money atakuwepo katika albamu hiyo.
Kwa mara ya kwanza Mimi Mars alisikika katika Bongofleva kupitia wimbo wake, Sugar (2017) uliotayarishwa na Dee Classic katika studio ya High Table Sound ambayo inamilikiwa na mwanamuziki Barnaba.
Mradi huu ulikuja muda mfupi baada ya kusainiwa katika lebo ya dada yake Vanessa, Mdee Music akiwa ndiye msanii wa kwanza kisha akaja kufuata Brian Simba.
Vee alimsaini Mimi Mars ikiwa ni baada ya kupata matokeo mazuri kupitia nyimbo zake zilizotoka mwaka 2015 - 2016, ambazo ni ‘Niroge’, ‘Hawajui’, ‘Never Ever’ na ‘Nobody But Me’ aliyomshirikisha K.O wa Afrika Kusini.
Sugar ni wimbo mtamu kama jina lake lilivyo ambapo Mimi Mars ameeleza jinsi anavyoufurahia uhusiano wa kimapenzi ambao unampa raha kiasi kwamba anaweza kuufananisha na sukari (sugar).
Video yake yenye rangi nzuri na mvuto mkubwa ilisimamiwa na Director Hanscana, huku ikipambwa na ushiriki wa mastaa wa Bongofleva kama Navy Kenzo, Rosa Ree, Wildad na Quick Rocka.
Mafanikio ya Sugar yaliwashawishi Coke Studio Africa kumpa nafasi ya kutumbuiza kama Msanii Chipukizi (Big Break Artist) 2018 na ikatazamiwa miaka michache mbeleni atakuja kuwa mwanamuziki mkubwa.
Hata hivyo, kabla ya kuachia wimbo wake huo, Mimi Mars tayari alishakuwa karibu na muziki kwa miaka mingi, mathalani alichangia uandishi katika wimbo wa Vanessa, Come Over (2014).
Na vilevile alionekana katika video ya wimbo wa kundi la Navy Kenzo ambao pia Vanessa alishirikishwa, Game (2015) iliyofanyika Afrika Kusini. Ni video ambayo pia marehemu Costa Titch alishiriki wakati huo akiwa kama dansa.
Ikiwa ni miaka zaidi ya minane imepita tangu wimbo wake huo kuachiwa, mwimbaji huyu mwenye sauti nzito na ya kuvutia. Tayari amejikusanyia mashabiki kutokana na uwezo wake wa kuimba kwa sauti laini.
Baada ya miaka mingi ya kuonyesha kile alichojaliwa katika muziki, mwaka huu Mimi Mars amepanga kuja na albamu ili kuwaburudisha mashabiki wake kwa mfululizo wa nyimbo nyingi kwa wakati mmoja.
Bado hajaweka wazi albamu hiyo iliyopewa jina la ‘17’ itakuwa na nyimbo ngapi na kina nani ni watashirikishwa katika mradi huu wa kipekee ila swali la wengi ni iwapo dada yake Vanessa atakuwepo au atamtosa tena?.
Ikumbukwe katika Extended Playlist (EP) yake ya kwanza, The Road (2018) yenye nyimbo sita hakufanya hivyo, na hivyo hivyo katika ile ya pili, Christmas with Mimi Mars (2021) yenye nyimbo nne.
Lakini katika albamu ya kwanza ya Vanessa, Money Mondays (2018) yenye nyimbo 17, hakuna wimbo hata mmoja ambao Mimi Mars alishirikishwa, hivyo hamna anayemdai mwenzake.
Kwa ujumla katika Bongofleva, wawili hao hawajawahi kuachia wimbo wa pamoja ila walishakutana kwenye nyimbo mbili za Injili, mmoja wapo ni Beautiful Jesus (2017) wakishirikiswa na dada yao, Nancy Hebron.
Hivyo pia kuna uwezekano mdogo wa Vanessa kusikika katika albamu hiyo ya Mimi Mars, na iwapo atasikika basi kitakuwa ni kitu kizuri hasa kwa mashabiki ambao hawajamsikia Vee kwa muda mrefu.
Utakumbuka mnamo Julai 2020, Vanessa alitangaza kuachana na muziki huku moja ya sababu alizotaja hadi kufikia uamuzi huo, ni muziki kutomlipa kulingana na uwekezaji na juhudi alizokuwa akizifanya.
Na kweli tangu wakati huo hajafanya tena muziki ingawa lebo yake (Mdee Music) iliendelea kufanya kazi kwa kusimamia miradi yote ya Mimi Mars anayetamba sasa na wimbo wake, Let Me Know (2026).
Mimi Mars anakuja na albamu wakati huo ambao ameweka nguvu zake zote katika muziki baada ya ‘kupumzika’ uigizaji kufuatia kuondoka katika tamthilia ya Jua Kali ambapo alifahamika kama Maria.
Katika uigizaji alishinda tuzo mbili, nazo ni The Orange Awards 2023 kama Mwigizaji Bora wa Kike, na Tanzania Film Festivals and Awards (TAFFA) 2021 kama Mwigizaji Bora wa Kike Chaguo la Watazamaji.
Na kwa upande wa muziki, Mimi Mars ameshinda tuzo moja, nayo ni kutokea Entertainment Arts Excellence Awards (EAEA) 2025 kama Mwimbaji Bora wa Kike.
Katika mtandao wa YouTube unaotumiwa na mashabiki wengi nchini kwa kufuatilia kazi za wasanii, huko kazi za Mimi Mars zimetazamwa zaidi ya mara milioni 21.7, huku Boomplay Music akifikisha milioni 13.8.