Mke wa Mkubwa Fella afunguka kinachoendelea hali ya mumewe
Muktasari:
- Kwa mujibu wa taarifa zilizowahi kuripotiwa na Mwananchi, Mkubwa Fella alianza kusumbuliwa na presha pamoja na kupungua kwa nguvu mwilini, hali iliyomlazimu kupunguza shughuli zake za kila siku.
Dar es Salaam. Safari ya afya ya meneja wa wasanii wa muziki wa Bongo Fleva, Said Fella 'Mkubwa Fella' imeendelea kuvuta hisia baada ya mke wake kueleza maendeleo ya matibabu yake tangu alipoanza kuugua mwanzoni mwa mwaka 2025.
Kwa mujibu wa taarifa zilizowahi kuripotiwa na Mwananchi, Mkubwa Fella alianza kusumbuliwa na presha pamoja na kupungua kwa nguvu mwilini, hali iliyomlazimu kupunguza shughuli zake za kila siku.
Wakati huo taarifa mbalimbali zilienea mitandaoni zikieleza hali yake ilikuwa mbaya, jambo lililowatia wasiwasi mashabiki na wadau wa muziki.
Baadaye, Mkubwa Fella alithibitisha alikuwa mgonjwa lakini alianza kuona nafuu taratibu.
"Ninaumwa kweli, lakini naendelea vizuri kidogo tofauti na mwanzo. Namshukuru Mungu naona mabadiliko taratibu," alinukuliwa akisema.
Mke wake amesema mwanzo wa ugonjwa huo ulikuwa mgumu kutokana na dalili zilizojitokeza ghafla na kumfanya mumewe ashindwe kuendelea na majukumu yake kama kawaida.
Ameeleza kwa sasa hali yake imeimarika na bado anaendelea na matibabu chini ya uangalizi wa madaktari.
"Mwanzoni hali ilikuwa inatisha kidogo, lakini sasa tunaona tofauti kubwa. Anaendelea vizuri na kila siku kuna matumaini mapya," amesema.
Ameongeza familia imeendelea kuwa bega kwa bega katika kipindi chote cha matibabu, huku marafiki na wasanii mbalimbali wakimtembelea nyumbani kumtia moyo.
Mkubwa Fella alianza kuugua mapema mwaka 2025 na tangu wakati huo amekuwa akipunguza shughuli zake ili kuzingatia matibabu. Familia yake inasema anaendelea kupata nafuu hatua kwa hatua na wana imani ataendelea kuimarika kadri anavyoendelea na matibabu.