Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mtazamo wa Sugu kuhusu usanii, atoa tahadhari-2

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Nyasa, Joseph Mbilinyi maarufu Sugu akizungumza wakati wa mahojiano maalumu na Mwananchi.

Muktasari:

  • Asisitiza kuwa muziki wake umemfikisha kisiasa, jukumu la waasisi ni kuilinda sanaa, na vijana wanapaswa kuiheshimu. Pia aeleza asili ya neno anautumia mitandaoni.



Dar es Salaam. Wakati mjadala kuhusu nafasi ya wasanii katika masuala ya kijamii na kisiasa unaendelea, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Nyasa, Joseph Mbilinyi maarufu Sugu, amesema msanii anapokuwa maarufu anakuwa mali ya wananchi, hivyo hawezi kujitenga na hisia, maumivu na matarajio yao.

Sugu, ambaye pia ni msanii kwa zaidi ya miaka 30, anaeleza kwamba sanaa ya muziki ndiyo aliyoitumia kama daraja la kumvusha na kumfikisha katika nafasi na hadhi ya kisiasa aliyonayo sasa.

Mjadala kuhusu wananchi kususia kazi za wasanii uliibuka mapema baada ya maandamano yaliyozaa vurugu Oktoba 29, mwaka jana. Baadhi ya watu walipoteza maisha, wengine mali zao kuharibiwa, sambamba na miundombinu ya umma.

Mijadala iliibuka katika mitandao ya kijamii, baadhi ya wananchi wakihoji kwanini wasanii hawajitokezi kuomboleza na kutoa pole kwa watu waliopoteza maisha. Mjadala huo ukasababisha baadhi ya wananchi wahoji kwanini wasanii hawatungi nyimbo zinazokemea matendo maovu nchini.

Miongoni mwa mambo ambayo wananchi walitaka yakemewe na wasanii kupitia muziki wao ni matukio ya kupotea kwa watu, ufisadi, demokrasia na mfumo wa siasa kwa ujumla nchini.

Hatua hiyo ikaibua shinikizo kutoka kwa baadhi ya wananchi wakiwataka wasanii waombe radhi. Wapo waliofanya hivyo, lakini wengine waligoma na walijibu katika mitandao yao ya kijamii wakisema hawataomba radhi kwa kuwa hakuna walilokosea.

Mjadala huo pia uliwahi kumuibua Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, aliyewatetea wasanii kwa kufanya kazi na Chama cha Mapinduzi (CCM), akisema wanafanya hivyo kama sehemu ya ajira zao.

Akiwa ziarani mkoani Songwe, Desemba 17, mwaka jana, Dk Mwigulu alisema wasanii wanaimba kwenye majukwaa ya CCM kutafuta fedha na haimaanishi wao ni wanachama wa chama hicho.

“Nani kawaambia hao ni wanachama? Nani kawaambia wanaenda kuimba kwa kadi? Nani kawaambieni nyimbo za kwaya zinatengenezwa kwenye studio ya walokole? Yule aliyetengeneza nyimbo hizo nani kawaambia kaokoka? Hawa wana akili au kamasi, mnakataa watu wasifanye kazi,” alihoji huku akisisitiza wataendelea kuwaunga mkono.


Wasanii vs Wananchi

Akizungumza katika mahojiano maalum mjini Dar es Salaam, Sugu anasema sanaa inapaswa kuwa sauti ya watu na wasanii wanatakiwa kujua kuwa umaarufu wao umetokana na mashabiki ambao ni wananchi.

“Kama wewe ni msanii na umekuwa maarufu, basi wewe ni wa watu, unamilikiwa na watu na watu wanakudai. Mara zote kumbuka watu, uwe na kiasi, uwe na busara za kupima hiki nachotaka kutoa kitawavutia watu kiasi gani,” anasema.

Anasema umma unaonekana kususia kazi za wasanii wa Tanzania na hadi sasa idadi ya matamasha ya wasanii wa Bongoflava imepungua.

“Waliozinguana na wananchi watumie busara na ushauri tuliowapa, kama wanaweza waombe radhi, kama wanaona haifai, wananchi wasiwe na wasiwasi, sisi tutapigania burudani hii na wapya watakuja tu,” anasema Sugu, aliyewahi kuwa Mbunge wa Mbeya Mjini kupitia Chadema kwa miaka kumi mfululizo (2010–2020).

Anasema jukumu la waasisi ni kuwafundisha wasanii kuwa watu wa heshima, lakini hawajibiki kumpigia simu msanii mmoja mmoja kumuelekeza namna ya kuishi.

“Jukumu langu mimi ni kuishi kwa mfano. Sisi tumeshafanya kwa mfano, na kwa kuwa hawajayazingatia madhara yake, sasa ndio hayo wameyaona,” anasema.

Sugu anaongeza kuwa lengo lake ni kuhakikisha muziki wa Bongoflava haupotei na kuimarisha sanaa ya ndani, akisisitiza kuwa haamini maendeleo ya muziki ni matokeo ya makosa ya waasisi bali ni mafanikio yanayoshuhudiwa.

“Bongoflava imekuwa kubwa na inasomba kila kitu, katika mawazo mapya yanakuja, wazalishaji wapya, waandishi wapya, lakini ngumu ni vyombo vya habari kuchagua kutounga mkono ile ya asili na kuiunga mkono mpya wakiamini ndiyo yenye soko,” anasema.

Anasema hakuwahi kuimba tangu aanze muziki, bali amekuwa akirap tu, lakini hadi sasa anakula fedha zilizotokana na muziki wake. Sugu anasema hayaangalii maendeleo ya muziki kwa mtazamo hasi, kwani mabadiliko yameshuhudiwa si Tanzania pekee bali duniani kote.

“Muziki umekua, mabadiliko yametokea, badala ya kulalamika, sisi waasisi jukumu letu ni kuhakikisha tunakulinda kile tulichokiasisi, na kile ndiyo kinabaki kuwa msingi,” anasema.

Anasema hana mtazamo hasi kuhusu maendeleo ya muziki, kwani msingi wa uasisi wake ni kuzalisha ajira, jambo ambalo limeonesha matunda yake.

“Vijana wanatakiwa watambue kuwa hii ni sehemu yao ya kupata riziki, wanatakiwa kuiheshimu. Nashindwa kushambulia sana kwa sababu naona sehemu ya vijana kupata kula tumefanikiwa,” amesema.


Sanaa ilivyomvusha kisiasa

Sugu anasema hadi anafikia hadhi yake ya kisiasa, muziki wake umechangia kwa kiasi kikubwa.

Anasema sanaa ndiyo iliyomfikisha katika hadhi ya kisiasa aliyonayo sasa, akifananisha mafanikio yake na michakato ya taaluma nyingine:

“Ukiniuliza kwa mafanikio ya jumla kati ya sanaa na muziki nini kimekufikisha hapo, nasema ni kama kumuuliza daktari wa sekondari au chuo, yote ni michakato inayozalisha kitu kimoja,” anasema.

Anasema anafurahia kuitwa majina yoyote kati ya msanii, mwanasiasa au mfanyabiashara kwa sababu ni kweli anahusika na yote.

“Tena usanii ndio najivunia sana kwa sababu ndio msingi wa yote, kwanza sio chaguo, ni kipaji ambacho Mungu anakupa, hiyo ni baraka,” anasema.


Kuhusu kauli zake

Katika ukurasa wa mitandao ya kijamii, Sugu amekuwa akitumia msamiati fulani, unaoonekana kama tusi dhidi ya wale wanaokera au kupishana naye mtazamo.

Amewahi kuutumia alipoandika katika ukurasa wake wa mtandao wa Instagram, akipingana na mitazamo ya watu wanaowatetea wasanii kuhusu kuimba nyimbo zisizokemea utekaji na kupotea kwa watu.

Alipoulizwa kuhusu hilo, Sugu anasema asili ya neno hilo ni mama yake mzazi, aliyekuwa analitumia pale anapomuonya zaidi ya mara moja katika kosa fulani.

Alipokuwa mdogo, anasema mama yale kila alipomtaka kufanya kitu kwa zaidi ya mara moja, alilitumia neno hilo kuweka msisitizo.

“Tukiwa wadogo kizazi chetu na walionizidi unakuta nyumbani mama anakwambia nenda kaoge, anazunguka anarudi saa limepita hujaenda kuoga, anakwambia wewe si nimekwambia ukaoge hadi sasa unazunguka zunguka nitakuchapa (neno lenyewe…), huko ndiko ilikotokea kutoka kwa mama yangu,” anasema.

Hata hivyo, anasema anaendelea kulitumia neno hilo ili kufurahisha watu, kwa sababu anaona limepokelewa vizuri na watu wanapenda.

“Naona watu wamelipokea, basi tunaenda nalo. Unajua nchi yetu hii ina mambo mengi sana, tukisema tuwe serious wakati wote, hatutafika. Utajikuta unaumwa magonjwa mbalimbali, lazima tutafute vitu vya kufurahishana,” anasema Sugu.