Ndani ya boksi: Konde, Mbosso ni uhuru wa manayani?
Muktasari:
- Mishe zimekuwa ngumu kinoma. Mtaa umekula ganzi kimyaa, ni kama ‘muvi’ za James Bond. Kila kitu kipo juu kimegoma kushuka chini. Ni mwendo wa mateka na mkia upo juu kama ngiri. Tupo ‘resi’ ile laaana babaake. ‘Tripu’ gereji, ‘tripu’ shamba ‘bedifodi’ ya kijiji ikasome.
Dar es Salaam. Mishe zimekuwa ngumu kinoma. Mtaa umekula ganzi kimyaa, ni kama ‘muvi’ za James Bond. Kila kitu kipo juu kimegoma kushuka chini. Ni mwendo wa mateka na mkia upo juu kama ngiri. Tupo ‘resi’ ile laaana babaake. ‘Tripu’ gereji, ‘tripu’ shamba ‘bedifodi’ ya kijiji ikasome.
Tutafanyaje sasa? Ni kukomaa kwa kila kitu mradi kumekucha. Tunaishi Kiyahudi kama nyakati za Mussa kuwapeleka Kaanani.
Kuna ‘taim dashbodi’ haisomi siku nzima, unaamka huna kitu na kurudi huna kitu. Lakini upo njwii kinoma.
Tunataka pesa nyingi, tunataka madem wengi, tunataka tuishi miaka mingi. Tunapata marafiki wengi, tunapata maradhi mengi na wanasepa ahera ni wengi. Kila kitu kwa wingi. Magonjwa mengi, shida nyingi, ndoa nyingi, talaka pia ni nyingi. Hujui kipi zaidi.
Matokeo yake ni ‘stresi’ mtindo mmoja. Huyu anatala mshahara, yule anataka kuhara, na huyu pia analeta masihara. Hii dunia kwa ujumla nayo ina ‘stresi’, na ndo maana maji mengi kuliko ardhi. Kwa sababu muda wowote dunia inaweza ‘kubasti’ soon.
‘Long taim’ wakati tupo ‘skonga’, ‘klasi’ tulikuwa tunasoma na pisi zenye mabwana huko mitaani. Na skuli yote inatambua Salome anatoka na Mdosi flan. Yaani pisi zilikuwa na bwana ndani na nje ya shule. Na halikuwa jambo la kificho.
Lakini pamoja na hili, bado bikira zilikuwa nyingi kuliko. Ajabu leo ikiwa ni msala mkubwa kutoka na ‘denti’ ndo wamedata zaidi. Hii leo kukuta ‘denti’ bikira wa ‘seko’ bado ana usichana wake ni ajabu la mwaka. Kifupi ukidhibiti saana jambo fala ni kosa kubwa.
Hata ‘korona’ mataifa ambayo yalidhibiti sana. Ilidedisha watu kibao, lakini huku Mungu aliacha janga liserereke lenyewe. Watu waliodedi kwa ‘korona’ ikawa siyo kiviile. Hata watoto wa kike kama ukiwabana sana lazima wakutoe nishai mshua dingi.
Oya! Nakuchana ‘laivu’ hata kwa mataifa ambayo raia walibanwa. Kama Gaddaf kule Libya, mwisho wake ukawa wa kindezi. Kiasili mtu anapenda kuwa ‘frii’ kuliko kubanwa sana na sheria, taratibu au kanuni. Sasa wewe endelea kubisha kibwege.
Kama manzi ya Adam, ‘Saa Godi’ angeilia mikausho tu. Alipopiga mkwara wa kutokula tunda lile la mti wa katikati likawa kosa. Ndo maana yule bwege shetani naye akatumia onyo hilo kuwarubuni. Kamba ‘Saa Godi’ anawazingua hilo tunda mzuka.
Manzi ikaona yule bwege nyoka ana akili. Kisa tu kampa uhuru wa kutafuna tunda la mti wa kati. Ukawa msala rasmi kwetu hadi leo. Manzi ya Adam ulituponza wengine, kwa sababu tu mwanzo ilibanwa banwa sana kutokula lile tunda.
Maisha yamekuwa kinoma. Kauli ya mtakula kwa jasho na kuzaa kwa uchungu. Kwa sasa haina ile nguvu kwa mademu, siku kisu kinatumika zaidi kupasua tumbo kuliko kukatia nyama buchani. Ni kweli hawazai kwa uchungu tena kama zamani.
Lakini adhabu ya kiumeni ile ya kula kwa jasho imehamia kwao pia. Na wao ‘nou deizi’ wanakula kwa jasho balaa, masela hawana ‘taimu’ ya kutunza wala kulealea mademu. Ubaba unapungua siku baada ya siku na kubaki ule uzazi mwenza tu. Ndo nakuchana sasa.
Ongezeko la ‘singo maza’ kitaa lina kasi ya ajabu sana. Kila dem uliyesoma naye, uliyekua naye utotoni au mtaani. Hivi sasa ana mtoto lakini baba wa mtoto hana. Na mshikaji wa kitambo, ukikutana naye leo atakuambia ana mtoto yupo kwa bibiake.
Mama zetu walitulea toka utotoni hadi ukubwani. Na sasa wanalea watoto wa watoto wao, sisi kama sisi tumeshindwa kulea. Ni tatizo zito sana hili kwa sasa, ila watu wanachukulia poa na kuacha vitu viende tu kama mafuriko ya maji. Ila ni noma sana.
Watu mishahara haitoshi kuishi wao wenyewe. Anaogopa kuishi na mtoto wa mtu atakayeweza kumpa mtoto na yeye. Mechi za sasa hizi zinachezwa ‘gesti’ tu na hotelini, watu wanaishia huko na hakuna kujuana hata magetoni.
Hata madem siyo kwamba wao ndo wanataka sana kuolewa. Na wao hawataki kuolewa ili wawe huru. Ndoa kwao ni kukosa uhuru na kubanana tu, yaana alibanwa na wazazi leo abanwe na bwana tu? Hilo hawataki ndo maana ni ‘usingo maza’ tu.
Uhuru wa kuingia ndani muda anaotaka. Kutoka na mwanaume anayetaka. Kulala anakotaka na kula na kunywa anachotaka. Ndo kitu wanataka wadada wa dunia hii. Ukizama ndani sana unaweza kugundua kuwa hata uchache wa ndoa chanzo ni ‘dadazi’ kuutaka uhuru.
Umemfuatilia Harmonize siku za karibuni? Umemfuatilia Mbosso siku za karibuni? Hata wao pia kule WCB walikosa kitu flan hivi. Watazame sura zao pia wakiwa na King Kiba. Hizi momenti kwa miaka mingi walizikosa. Pengine kutokana na kambi ya awali.
Tunajua WCB na Alikiba ni chui na paka. Watoto wa WCB hata kama walitamani kushika mkono wa King Kiba, walishindwa. Sasa hivi wapo huru tazama namna walivyo ‘bize’ na King Kiba. Yes, ni wazi kuwa walikosa uhuru huo kwa mzazi wao.
‘Ene wei’, kushirikiana ni jambo jema sana. Lakini naiona taswira flan ya kukosekana kwa uwepo wa fursa nyingine kwa Mbosso na Konde mwingine. Mtaani kuna kina Mbosso na Harmonize wengi sana. Mondi ataendelea kuzalishia Mambosso mapya?
Ushikaji wa Mbosso na Alikiba. Ukaribu wa Harmo na King Kiba. Mondi hana kwere moyoni? Ni kwamba anaona poa tu maisha yanasonga? Je, uwepo wa Konde na Mbosso kando ya King Kiba. Ni funzo kwa nani kati ya Alikiba na Diamond?
Harmo na Mbosso ni chanzo cha King Kiba naye kaunza kuzalisha Konde Boy na Mbosso Khan wengine? Au chanzo cha Mondi kuacha kutuletaa kina Konde na Mbosso wengine? Hii wacha tu picha liendelee, mwisho tutaona ‘steringi’ ni yupi?