Ndani ya boksi: Tuna ‘aleji’ na mafanikio ya mtu
Muktasari:
- Lakini kabla ya haya mafanikio yake. Alipigwa sana mishale. Alitandikwa sana madongo. Aliishi maisha ya kutandikwa kwa kebehi nyingi. Je, ni nani huyo mwenye moyo mgumu na mkunjufu? Endelea kusoma hii ipo chini huko.
Dar es Salaam. Game liko chini ya soksi zake. Ndiyo! Analiendesha. Akiliamrisha linamtii. Anajituma. Ana pesa. Ana demu mzuri sana. Ni maarufu na anapendwa. Ndio unaweza kuwa maarufu lakini bado ukawa hupendwi.
Lakini kabla ya haya mafanikio yake. Alipigwa sana mishale. Alitandikwa sana madongo. Aliishi maisha ya kutandikwa kwa kebehi nyingi. Je, ni nani huyo mwenye moyo mgumu na mkunjufu? Endelea kusoma hii ipo chini huko.
Hata Hitler alikuwa maarufu. Shetani ni maarufu lakini hapendwi. Unaweza kuwa na pesa usiwe maarufu. Kuna matajiri wangapi Bongo hii wanapita Kariakoo bila kutazamwa? Unaweza kuwa na kila kitu ila demu mbovu.
Hakuna uchawi kama kujituma na kujitambua. Utafanikiwa tu. Moja kati ya akili mbovu tuliyonayo waswahili ni kutopenda mtu awe juu kila siku. Sisi tunataka kuona mtu akipanda kisha ashuke. Tunaumizwa sana na wenye mafanikio.
Furaha ya Waswahili sisi ni kuzalisha masikini zaidi yetu. Hukerwa kuona mtu mmoja anaendelea kupaa kila siku. Hatupendi mtu mmoja kuwa juu kila siku. Hata kama anajituma sana na kupambana. Hatujawahi kufurahia hilo.
Tunapenda kuona mtu anapaa juu na kushuka chini ghafla. Hasira za watu kutopenda hilo. Tunalihamishia katika kutafuta mbadala wake. Hulazimisha upinzani wa mtu na mtu hata kama hao watu hawajuani.
Hakuna lolote zaidi ya kuona mtu aliye juu anatafutiwa mtu wa kuwa juu yake. Ndiyo maana hata dili zetu zinafanana. Mtaa huu kukiwa na saluni, kila ‘fremu’ wataweka saluni. Tuna tabia ya kuiga ama kuigana kibishara.
Wabongo baadhi siyo wote, hukerwa na umaarufu wa mtu. Mafanikio ya mtu hata uwepo wake duniani. Kuna watu wanaongea vibaya kuhusu mtu. Mpaka mtu hulazimika kuamini kuwa hawapendi hata yeye kuwa hai.
Watu wenye mioyo hiyo ya kipuuzi. Hutulazimisha tuamini huyu siyo yule. Hana mashairi mazuri kama zamani. Hana sauti wala uwezo wa kuimba. Tunasahau aliyeimba Parakatatumba, alivyotuteka.
Bila kuelewa lugha yake wala ubora wa sauti yake. Makhirikhiri walibamba hapa bila kuelewa lugha walizotumia. Wakongo mpaka kesho wanakimbiza Bongo bila kuelewa Kilingala. Na wao huona fahari kuongea Kikongo.
Hivi sasa kuna vita kubwa sana kwa baadhi ya watu na singeli. Yaani ule muziki wa singeli unawakera sana baadhi ya watu. Wanaweza kuwa na ‘pointi’. Kama walivyokuwa na ‘pointi’ wazee wetu na Bongo Fleva.
Wabongo wanataka wasanii waimbe ujumbe. Hizi siyo nyakati za masela wa Daz Nundaz. Ni dunia ya tofauti ambayo haitaki kusikia shida shida na karaha. Hii ni dunia mpya inayopuuzia shida na kuhusudu bata na furaha muda wote.
Unaletaje nyimbo zenye jumbe kama Chemsha Bongo. Wakati dunia hii inataka fleva tu. Sauti? ‘Bana Boi’ yule hafikii hata robo ya sauti ya Ibraah. Ila ni nani mwenye mafanikio, umaarufu na uzito kati yao?
Dunia ya sasa siyo ya kuimba shida za ukabaji Mwananyamala. Ama kero ya ardhi ya Matombo huko. Ni midundo mizuri na mtiririko mtamu wa maneno tu. Ili hata asiyeelewa lugha afurahie midundo na melody.
Waacheni madogo wapige mkwanja katika dunia yao. Waacheni mafogo wawakilishe taifa. Waacheni madogo wafurahie kujituma kwao. Waacheni madogo watimize dua za mama zao juu yao.
Ni madogo flani hivi wasio na elimu kubwa wala kukulia maisha bora. Na wao niwapambaji, pesa hawakurithi kwa baba zao. Wanapambania kesho yao kupitia muziki unaokukera lakini una mashabiki.
Paten, ni dogo aliyetamani kumpa mkono tu Zuchu. Achilia mbali kuimba kwenye jukwaa moja na Zuchu. Leo akiwa jukwaani na Zuchu anakuwa kavuka malengo. Furahia mafanikio yake badala ya kuchukia.
Hata Bongo Fleva wakati ikichipukia. Wazee walikuwa wanoko kinyama. Walikuwa wakisagia kunguni sana huu muziki. Ulionakena ni muziki wa kihuni usiuofaa kwenye jamii. Leo hii sanaa yenye utajiri ni Bongo Fleva.
Diamond yupo kwenye kilele cha Mlima Kilimanjaro. Anawatazama Watanzania na wanamuziki wenzake kwenye viunga vya mji wa Moshi. Ni gemu analiendesha vile atakavyo yeye. Lakini kabla alipigwa mishale mingi.