Prime
Ndani ya Boksi: Vesi moja ya Kiba, Mondi na Konde hoi
Muktasari:
- Pengine alijua anaingia kitaani na kakaake Mondi. Ghafla kakutana na ‘jebu’ la King Kiba, lililokuwa linapita njia. Hakujiandaa kabisa na vita ya mtu tatu katikati yake, na bahati mbaya wale siyo kina Marioo. Mibuyu mikubwa miwili, kapigwa mtu kati.
Dar es Salaam. Harmonize anajuta kutoa ngoma katikati ya milima miwili. Kajala kapambana wapi, mashost zake wamepambana waaapi. Kimsingi dogo atoe pini lingine tena kama anataka kwenda mjini. Alilotoa ni kama limepita na upepo.
Pengine alijua anaingia kitaani na kakaake Mondi. Ghafla kakutana na ‘jebu’ la King Kiba, lililokuwa linapita njia. Hakujiandaa kabisa na vita ya mtu tatu katikati yake, na bahati mbaya wale siyo kina Marioo. Mibuyu mikubwa miwili, kapigwa mtu kati.
Na hapa ndo unapata picha kuwa ‘fansi’ wa Konde ni wale wa Kiba. Ndo maana safari hii kaingia cha kike, vesi moja ya Kiba imemtupa nje ya mpambano. Mwenye watu wake yupo mtaani, lazima wewe utulie kwanza mpaka apite zake.
Kama ‘Godi Faza’ wake Diamond kakalishwa raundi ya kwanza tu. Unategemea bwamdogo Konde atafanya nini? Kimsingi ni kama mwana aliyekatwa kofi la usoni na mwela. Ana wenge la nyota nyota na kichwa kama kina nzi ndani yake. Noma!
Konde Boy kapigwa na shoti ya umeme. Hata ‘taim’ ya kutafakari kaikosa kajikuta kwenye mfumo na haelewi ajinasue vipi. Mabroo wameingia mzigoni ‘kudistabu pisi’ kitaa, lazima njuka utulie. Na hili ni jibu kamili kuwa nuziki una wengi wao.
Tunavyoongea hivi Mond na yeye anatweta huko aliko. Hana hamu, kaingia shimo la Tewa kakutana na harufu kali. Uchafu ni mwingi kila mtu ametii huko, na kipyenga kimelia refa kaweka mpira kati mechi imeisha. Usiombe balaa kama hili likukute. Utajuta.
Mondi katoa pini jipya baada ya Happy, nalo linachechemea na kitaa ni kama hakijaelewa picha. King Kiba amekuwa kama Iran, hakuna namna masela waombe mazungumzo, kama Trump na Iran, wakitaka meli za pini zipite kitaa bila mkwamo.
Kiba kafunga mtaa na vesi moja tu. Na hata Bien machale yake yako vyede, kaanza kufungua, angesubiri Kiba aanze bila shaka tusingejua hata kama naye yupo kwenye ngoma hili. Mitaa inaruka na vesi la Kiba, kutoka Posta hadi Malamba Mawili.
Tunachukulia poa poa tu, ukweli ni kwamba vesi moja ya Alikiba imefunika nyimbo mbili. Na siyo nyimbo tu, za wanamuziki wawili wakubwa nchini. Unaweza kudai jamaa kama ‘rango’ kaotea kama kuotea. Ni vile tu watu tuna hulka ya kusahau. Sikiliza!
Mwaka jana Alikiba alimrudisha Dully Sykes kwenye ramani kwa ghafla sana. Ngoma la Kimara Temboni mbali, lilikimbiza kitaa hata Madam Samia alilihusudu. Ni Kiba huyo huyo na vesi yake moja tu, akamfanya Dully awe juu kama mawingu.
Wasanii walipaswa kushtuka na kile kitu. Haikuwa kawaida kama wanavyotaka tuamini, Kiba kuna njia anapita ambazo zipo miaka yote. Lakini masela wengi bado hawajashtuka. Hiki kitu alifanya Dogo Aslay miaka kama kadhaa iliyopita na alileta balaa mjini.
Unamkumbuka Dogo Aslay wa 2017/18? Natambaa... Sura yake ya Upole? Kwenye shoo dogo alikuwa anaacha watu waimbe yeye kashika maiki kama fimbo tu. Watu waliimba nyimbo zake zote mwanzo mwisho, Fiesta ni kama aliiteka yote.
Kwanini? Aslay alipita katikati ya msimu wa ‘Amapiano yao na ule ‘Unaijeria’ wao mwingi mwingi. Yeye akakandamiza na ladha ya Bongo Fleva halisia. Kikawa kitu kipya sikioni kwa Ge Z yeyote. Akajitofautisha na kina Marioo, Jay Melody nk.
Ndicho alichofanya Kiba kwenye pini la Dully, Kimaraaa Temboni Mbali. Kisha amerudia kwenye hili pini na Bien. Nadhani aliona utofauti akaamua kupita mule mule. Watu walimisi zile fleva za Bongo Fleva, ambazo ni adimu sana kwa sasa.
Sikiliza vizuri vesi ya Kiba, haina maajabu. Lakini ina upekee na utamu kutokana na fleva yake kuwa adimu. Watu kuna aina flan ya ngoma zimewakinai kinyama ni vile hawajui shida ilipo. Hapa kutoboa inabidi uwe na akili ya kibiashara zaidi.
Tofauti ni moja. Alikiba bado ana mtazamo wa Karikoo zaidi. Dai ana mtazamo wa Bangkok. Hili utaliona kwenye aina ya nyimbo zao wanaozotoa. Ndo maana kuna watu husema Mondi kwa sasa anabebwa na Zuchu. No, haiko hivyo.
Mondi akifanya kazi na Zuchu au msanii wa Bongo, anaweka fleva za msosi wa kuwalisha ndani ya Bongo. Na akifanya peke yake au na msanii wa nje anatoa chakula cha kuilisha dunia, kitu ambacho Tarime hawaelewi. Na hapa ndo ilipo tofauti yake.
Pini kama Happy haliwahusu Joti na Mpoki. Linawahusu kina Chris Rock, Eddie Muphy na wenzao. Kuna Diamond wawili hivi sasa, yule anayewalisha Wabongo kwa kushirikishwa na kina Zuchu, na yule Diamond wa kuilisha dunia akiwa kivyake.
Diamond wa kuilisha dunia yule hamuwezi Alikiba. Pia Alikiba hamuwezi Diamond anayeilisha dunia. Ngoma yaHappy soko lake halipo Mburahati wala Mabibo. Kama ambavyo Watatii ya Kiba na Bien mwisho wake kisoko ni Afrika Mashariki tu.