Ndani ya Box: Zay B kaondoka na upekee
Muktasari:
- Katika ubora usiopimika Inspekta Haroun, akiwa na wimbo wa taifa ‘Mtoto wa Geti Kali’. Anapendwa na madem, masela, mabishoo na wazee. Akakubali kutia ‘vesi’ yake katika pini la msanii mpyaaa tena wa kike Zainab Lipangile Zay B.
Dar es Salaam. Aliiingia kwenye gemu na pini lake la ‘Gado’. Humo ndani alipigwa tafu na mtoto wa uswazi huko mitaa ya Mikoroshini Temeke, Inspekta Haroun a.k.a Babu. Kama wewe ni ‘jini zedi’ muulize Bi Mkubwa hapo homu, atakuelezea.
Katika ubora usiopimika Inspekta Haroun, akiwa na wimbo wa taifa ‘Mtoto wa Geti Kali’. Anapendwa na madem, masela, mabishoo na wazee. Akakubali kutia ‘vesi’ yake katika pini la msanii mpyaaa tena wa kike Zainab Lipangile Zay B.
Ule wimbo ukawa mkubwa sana. Mpaka Majani akautamani kama siyo kuuonea wivu. Ikatokea ‘bifu’ la ghafla Inspekta na Zay B. Sasa hapo ndo Majani akaona mzuka. Majani akanyonga biti na kumpa Zay B ili ashirikiane na Nature.
Wakati huo Inspekta na Nature ni chui na paka. Na Majani akaona ule wakati wa kumpaisha msela wake Juma Nature. Akapiga Niko Gado remix, humo ndani mjomba Nature kaua balaa na Majani pia alinyonga biti la hatari. Ni kama walipania sana dizaini.
Hapo tayari upekee wa Zay B ni kufanya kazi na mastaa wawili wakubwa wa kiume. Yeye akiwa msanii mpya tena wa kike, oyaa narudia tena. Kamuulize baba au mama, akuambie Babu na Nature wa kipindi kile walikuwaje? Sasa Zay B alifanya nao kazi.
Sister P akaibuka na ‘Anakuja’, na yeye akamchana Zay B ‘kujibusti’ kisanii. Mwana FA naye akaamua Sister P kwa pini lake na Jaymoe. Akiuliza “Ingekuwa vipi Sister P asingekuwapo Zay B?” Sister P akakereka akaja na “Hey Dj” hilo pini ndani kamuua FA. Ilikuwa ni chana nikuchane.
Tazama mtiririko chanzo akiwa Zay B. Wimbo mmoja wa Zay B, ukamleta Nature na Babu, Sister P na Mwana FA. Huu ni upekee wa kipekee unapofanya kazi yako inayogonganisha watu kibao bila kutarajia. Leo hii Zay B ana wiki ndani ya udongo. Tumuombee na sisi tujiombee.
‘Resti ini pisi dada’, mbele yako nyuma yetu. Tulikuzimia kinoma sema ‘Saa Godi’ kakuzimia zaidi. Mpe salamu zetu Maunda Zorro, tena mwambie aliondoka ghafla sana. Bila kumuaga hata kaka yake Banana, naye alishituliwa na taarifa tu, kuwa sista kasepa.
Langa, usiache kumweleza kuwa walio wengi walimuelewa zaidi baada ya kusepa. Kumbe wakati mwingine ‘Saa Godi’ anakubeba ili yatimie yale aliyoyaweka ndani yako. Ndo ilivyo kwa ‘brazameni’ na Mfalme wa Salasala God Zilla. Waambie tunawamisi.
Vipi Complex na Vivie. Tunajua hawa walikuwa katika ubora wao pindi weee ukiwa kwenye ubora wako pia. Ni wazi kwamba mna mengi ya kuongea, kupeana michano na kukumbushia ‘gemu’ ilikotokea. Waambie msela wao AY yupo Masaki na maisha yapo.
Mwambie Mandojo kuwa huku Domokaya anammisi. Na ‘gemu’ linaimisi fleva ya mchanganyiko wao. Maana hakuna Domo bila Dojo, lakini sasa tunakubaliana na hali kuwa kuna Domokaya bila Mandojo. Familia ya muziki wetu inasonga bila ubunifu wa daraja lao. NakNak!
Mwambie Y P, kwamba Temeke siyo ile ya kipindi kile. Temeke ya sasa imeshindwa kuzalisha kina Juma Nature wapya. Hata kina D Voice wanakosa ile ‘testi’ kamili ya Tmk. Ni ngumu kumtofautisha Mtemeke na Mmikocheni, wana swaga mfanano kama nanasi.
Kuna Mr Ebbo, kuna Jebby, kuna Ngwair, kuna Cpwaa, kuna Mtoto wa Dandu, kuna Pancho Latino. Hapo ni Mtoto wa Dandu pekee anayeweza kukosa maongezi marefu na wewe. Kwa sababu ya kutangulia zamani zaidi. Lakini hao wengine wote stori haziishi.
Wapo wana kibao waliotangulia kabla yake sister. Ukiwakuta huko waambie tuliwapenda na bado tunawapenda. Ongea na Ruge na umwambie B Dozen karudi tena eneo lake. Kisha mtembelee na Gadner G Habash mpe salamu zake, mwambie bintiye Karen siyo mnyonge.
Mwambie Steve 2 K, kwamba Fid Q bado kakaza na kubum kabam. Anaongoza msafara. Usimsahau John Mjema mwambie stori zake za wachumba 30, kwa sasa kuna Diamond hayo ndo maisha yake. Kazalisha kila taifa ukanda wote wa Afrika Mashariki, yaani watu wanaishi alichokiimba.
Zay B usiache kutembelea mtaa wa Steve B. Kumbuka Sir Nature katika wimbo wa Niko Gado alisema: “Steve B, Vanture na Nature ni mafundi wa kukesha.” Mwambie huku sasa msela wake Dj Vanture yupo Block House anawakilisha sana tu. Kuna pisi kali balaa.
Nenda kitaa ambacho wanaishi masela kutoka Arachuga. Cheki na G Son na Faza Nelly. Waambie X-Plastaz siyo kivile, ila Arachuga ipo katika mikono salama ya Joh Makini, Lord Eyes na G Nako. Na waambie G Nako bado hanywi pombe. Anazingua bigi taimu ila ndo masta wa ‘korasi’ kwa sasa.
Zainabu Lipangile, najua kwamba mtaa wa Ngwea ndo wa Mabovu. Mwambie ‘homu boi’ wako Geez Mabovu, kwamba pini lake lile la Mtoto wa Kiume, ni chachu ya upambanaji wa masela mitaani. Na wanakubali kuwa yeye ndiye rapa bora zaidi. Ila walimuelewa zaidi baada ya kusepa.
Piga misele dadaangu, pitia hata mitaa ya Roy Bukuku. Mwambie ukweli, ni Mr Blue pekee toka G Records. Ambaye anawakilisha kibabe kisanaa. Na wengineo akiwepo dadake Enika ni kama wamelisusa gemu lote. Mchane kuwa tunamisi biti zake.
Ukiweza pita kwa Banza Stone, mwambie dansi imeyumba sana. Kisha cheki na Amina Chifupa, na usiache kumueleza kuwa taarabu haipo huku. Hata Bi Khadija Kopa mtoto wake anaimba singeli na kina Dogo Paten. Unamkumbuka D Rob? Hao ndo Kwanza Unit na Nigga One. Wape hi.
Bongo Fleva imetoka mbali sana, na maana ya kutoka mbali ndiyo majina kama haya ya kina Zay B. Huyu ni alama ya Bongo Fleva katika nyoyo za kikeni. Najua kuna mapimbi watasema mbona akiwa hai hamkusema? Maneno ya aina hii husemwa mtu akiwa kasepa. Lala Zaibab Lioangile a.k.a Zay B.