Ndoa ya Kanye West na Bianca inapumulia mashine

Muktasari:

  • Tangu Septemba 2023 watu wa karibu wa Bianca wamekuwa na wasiwasi kuhusu mwenendo wake katika himaya ya rapa huyo, marafiki zake wanajaribu kumuokoa lakini hakuna anayeweza kwa sababu ya vizuizi ambavyo Kanye ameviweka.

Dar es Salaam. Afya ya ndoa ya pili ya Kanye West, inaelekea kudhoofika baada ya kuripotiwa kumpiga marufuku mkewe Bianca Censori kutumia mitandao ya kijamii kwa ajili ya kile kilichotajwa kama kuimarisha ulinzi wake binafsi.

Hatua hiyo inakuja wiki chache baada ya Kanye West kuwekwa kitimoto mtandaoni kufuatia kuchapisha picha zisizo na maadili za mkewe kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii.

Wawili hao walikutana Novemba 2020 baada ya Bianca kuhamia Los Angeles akitokea kwao Australia, Kanye alimtumia ujumbe Instagram na kumwambia aende LA kumfanyia kazi katika kampuni yake, Yeezy kama Mbunifu Mkuu.

Januari 9, 2023 waliripotiwa kufunga ndoa ya faragha na yenye utata ikiwa miezi miwili tangu kukamilika kwa talaka ya Kanye West na aliyekuwa mkewe Kim Kardashian, ambaye walikuwa pamoja tangu mwaka 2012.

Kwa mujibu wa Daily Mail, Kanye West amechukua uamuzi huo ili kumzuia Bianca kuchangamana na watu wengine kwenye mitandao ya kijamii, ili kuepusha maoni hasi kufuatia vitendo vyake vya hivi karibuni.

"Bianca yupo na mitandao ya kijamii kila mara na alikuwa akijishughulisha nayo hadi alipoolewa na Kanye. Hataki awe nayo kwa sababu anafikiri itamdhuru ikiwa atasoma mambo machafu ambayo watu wanasema," chanzo kimoja kilieleza. Marafiki wa mrembo huyo mwenye umri wa miaka 29 sasa wanaripotiwa kudai kwamba Bianca mwenye nguvu waliyekuwa wakimfahamu hapo awali, anaonekana kutoweka tena.

"Anavaa anachotaka, kwenda anakotaka na kufanya anachotaka kwa sababu hana chaguo lingine. Alitoka kuwa mbunifu wake hadi kuwa mkewe nafasi ambayo kwa bahati mbaya haina malipo. Amenaswa," chanzo cha ndani kiliiambia Daily Mail.  Tangu Septemba 2023 watu wa karibu wa Bianca wamekuwa na wasiwasi kuhusu mwenendo wake katika himaya ya rapa huyo, marafiki zake wanajaribu kumuokoa lakini hakuna anayeweza kwa sababu ya vizuizi ambavyo Kanye ameviweka.

Aliyekuwa mke wa Kanye West, Kim katika mahojiano yake ya Desemba 2022 alisema licha ya mwenendo wa rapa huyo kutofurahisha wengi, bado amekuwa akimlinda mbele ya watoto wake, hivyo hawajui chochote kinachoendelea huko nje.

Ikumbukwe Kanye West alipata mashabiki wengi zaidi kupitia  albamu yake, ‘The College Dropout’ (2004). Kabla ya Bianca alikuwa na uhusiano na wanawake kama Alexis Phifer (2000 - 2006), Amber Rose (2008 - 2010), Julia Fox (2021), Venetria (2022) na Kim Kardashian (2012 - 2023).