Neno la Ciara baada ya mumewe kustaafu NFL
Muktasari:
- Ciara, mkali wa kibao cha How We Roll (2023) akishirikiana na Chris Brown, alimtaja mumewe kama mtu bora zaidi duniani na kusema anajivunia mafanikio aliyoyapata ndani na nje ya uwanja.
Marekani. Mwimbaji maarufu kutoka Marekani, Ciara, 40, amempongeza mume wake, Russell Wilson, 37, kufuatia kutangaza kustaafu Ligi ya Soka Marekani (NFL) baada ya kuitumikia ligi hiyo kwa miaka 14.
Ciara, mkali wa kibao cha How We Roll (2023) akishirikiana na Chris Brown, alimtaja mumewe kama mtu bora zaidi duniani na kusema anajivunia mafanikio aliyoyapata ndani na nje ya uwanja.
“Daima ninajivunia wewe. Ni baraka kubwa kuambatana nawe katika safari hii. Wewe ndiye chanzo changu kikubwa cha hamasa yangu,” aliandika Ciara.
Russell alitangaza rasmi uamuzi wake wa kustaafu kupitia video aliyoposti kwenye ukurasa wake wa Instagram, ambapo alitoa shukrani kwa watu mbalimbali waliokuwa sehemu ya kazi yake.
Hata hivyo, Russell bado ataendelea kuwepo katika ulimwengu wa michezo kwani anaenda kujiunga na kituo cha CBS Sports ambapo atafanya kazi kama mchambuzi wa michezo.
Mshindi huyo wa Super Bowl akiwa na timu ya Seattle, alimshukuru Ciara akisema ameifanya safari yake ndani ya NFL kuwa rahisi na yenye mafanikio.
“Na nakushukuru wewe, asante Ciara kwa kuwa umekuwa baraka yangu kubwa zaidi niliyowahi kuipata maishani. Wewe ni rafiki yangu wa karibu na mshirika wangu katika kila jambo. Safari hii ya maisha isingekuwa sawa bila uwepo wako,” alieleza Russell.
Tetesi za uwepo wa uhusiano wa Ciara na Russell zilianza kuenea baada ya kuonekana mara kwa mara wakiwa pamoja, ikiwemo kwenye mchezo wa Mariners huko Seattle Aprili 19, 2015, na siku chache mbeleni wakathibitisha.
Hatimaye Julai 6, 2016, wakabadilishana viapo vya ndoa katika sherehe ya faragha iliyofanyika Peckforton Castle, Cheshire nchini Uingereza. Waliohudhuria ni familia na marafiki wa karibu pekee, akiwamo Kelly Rowland, Jennifer Hudson na La La Anthony.
Na hadi sasa wamejaliwa kupata watoto watatu, Sienna Princess (2017), Win Harrison (2020) na Amora Princess (2015). Hata hivyo, kabla ya ndoa hiyo tayari Ciara alikuwa na mtoto mmoja, Future Zahir (2014) aliyezaa na mpenzi wake za zamani rapa Future.
Ciara, mshindi wa Grammy, wengi wanamkumbuka kupitia kolabo yake na Bow Wow, Like You (2005) ambayo ilifanya vizuri hadi kushika nafasi ya tatu katika chati ya Billboard Hot 100.
Hadi kufikia mwaka 2019, Ciara alikuwa ameuza nakala zaidi ya milioni 45 za kazi zake duniani kote, ikiwa ni baada ya kuachia albamu zake sita. Vilevile amecheza filamu kama All You’ve Got (2006), Mama, I Want to Sing! (2012), The Color Purple (2023), na The Devil Wears Prada 2 (2026).