Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Diamond kutoka kwa Alicia Keys hadi Ciara

Muktasari:

  • Hii ni stori nyingine kubwa kwa muziki wa Bongo Fleva kuzidi kuishika dunia.

Dar es Salaam. Nyota ya Diamond Platnumz inazidi kupaa. Kimataifa kwa sasa hakamatiki. Baada ya kuiteka Afrika na kufanya kolabo na wasanii wengi, sasa mwenyewe anasema anawaza zaidi nje ya Afrika.

Hii ni stori nyingine kubwa kwa muziki wa Bongo Fleva kuzidi kuishika dunia.

Juzi Jumatatu usiku, msanii wa Marekani, Ciara Princess Wilson ‘Ciara’, aliachia albamu mpya inayokwenda kwa jina la ‘Cici’ ikiwa na ngoma nane.

Katika albamu hiyo kuna ngoma ambayo ameimba na Diamond Platinumz iitwayo ‘Low’ na kuongeza idadi ya nyimbo ambazo Mondi amefanya na wasanii wa kimataifa kufikia saba kwa zile ambazo zimefanya vizuri au kupokewa vizuri.

DIA 01

1. Marry You – ft Ne-Yo (2017)

Hii ilikuwa kolabo ya kwanza kufanya na msanii wa Marekani. Ni wimbo ‘Marry You’ ulikuwa na ladha ya Afro Pop na RnB.

Ni moja ya mafanikio ya mwanzo kwa muziki wa Diamond kimataifa hasa nje ya Afrika kwani Ne-Yo aliwahi kunyakua tuzo kadhaa za Grammy, pia amewahi kufanya kazi na wasanii wakubwa kama Beyonce, Rihanna na Usher.

Ingawa Marry You haikupenya kwenye chati za Marekani, Diamond alipata faida kubwa ya kuonekana kwenye vyombo vikubwa vya habari kama Billboard na MTV Base, vilivyoandika kuhusu kolabo hiyo. Kibiashara wimbo huo ulifungua milango ya Diamond kufanya shoo kubwa Marekani, ikiwemo One Africa Music Festival (Dubai, London na Houston) na alishiriki jukwaa moja na mastaa wa dunia.

DIA 02

2. Waka – ft Rick Ross (2017)

Mwaka huo huo, Diamond alifanya kolabo nyingine akiwa na Rick Ross, rapa kutoka Marekani na mmiliki wa lebo kubwa ya Maybach Music Group.

Waka ni moja ya video zilizorekodiwa kwa gharama kubwa kuanzia eneo lenyewe Miami, mandhari ya kifahari na magari.

Kolabo hiyo iliwavutia mashabiki wengi na kumwona kama staa wa Afrika mwenye uwezo wa kufanya ngoma na wasanii wakubwa na ikaleta ushawishi mkubwa kwenye muziki wake.

DIA 03

3. Hallelujah – ft Morgan Heritage (2017)

Huu ulikuwa mwaka wa kufanya ngoma na wasanii wa kimataifa, baada ya Marry, Waka akaja na muendelezo wa Hallelujah.

Wimbo huo ulitoka kwenye albamu ya A Boy from Tandale ukiwakutanisha Diamond na kundi la Morgan Heritage, washindi wa tuzo za Grammy kwenye muziki wa Reggae.

Kiufupi Diamond alipata kolabo na bendi hiyo mwaka mmoja baada ya kushinda Tuzo ya Grammy mwaka 2016 na albamu yao ‘Strictly Roots’ kipengele cha Best Reggae Album.

Hii ilikuwa moja ya kolabo kubwa kwani Reggae ni muziki unaopendwa duniani na una hadhira ya kudumu katika mataifa mengi ya Ulaya, Caribbean na Amerika Kusini na ilimfungulia mlango wa kushiriki matamasha ya mchanganyiko badala ya mashoo ya Afrika pekee.

DIA 04

4. African Beauty – ft Omarion (2018)

Mwaka mmoja baadaye Diamond alishirikiana na Omarion, mwanamuziki na dansa kutoka Marekani, wimbo huo ulipata mapokezi makubwa kutoka kwa mashabiki wa msanii huyo.

Ngoma hiyo ilikuwa na mchanganyiko wa Afro Pop na Bongo Fleva, Diamond alimbadilisha Omarion hadi kuimba mistari yenye lugha ya Kiswahili.

Kolabo hii ilimpa Diamond nafasi ya kushiriki kwenye tamasha ya Essence Festival Marekani na kufanya mahojiano na vyombo vya habari vya Marekani kama BET na jina lake lilianza kujulikana zaidi.

Ngoma hiyo ilimpa tuzo Omarion ya African Muzik Magazine Awards mwaka 2018 kama kolabo bora ya mwaka.

Hilo liliongeza hadhira yake barani Asia kwa sababu Omarion alikuwa na mashabiki wakubwa Japan na Korea Kusini.

DIA 05

5. Wasted Energy – Alicia Keys ft Diamond (2020)

Kwenye ngoma hiyo Diamond alishirikishwa na mwanadada huyo mwenye sauti ya kipekee na kolabo hiyo ilishtua Afrika kutokana na jina la msanii huyo. Alicia Keys ambaye ni mshindi wa Grammy mara 15 alimshirikisha Diamond kwenye wimbo huo ambao ulikuwa moja ya ngoma kwenye albamu ya Alicia. Ingawa Diamond hakusikika sana kama sehemu kuu ya wimbo, kitendo cha kuwepo kwenye albamu ya Alicia Keys kilimweka kwenye ramani ya muziki wa dunia kwa kiwango cha juu.

Kolabo hiyo ilimfanya Diamond kutajwa kwenye vyombo vya habari vya kimataifa kama CNN, BBC na Billboard na kuthibitisha ubora wake. Ilimpeleka Diamond kwenye majukwaa ya kifahari zaidi kama kupata mialiko ya kushiriki kwenye Global Citizen Festival na majukwaa makubwa kama Apple Music na iHeartRadio.

DIA 06

6. Jugni – Diljit Dosanjh ft Diamond Platnumz (2022)

Kolabo hiyo na Diljit Dosanjh, staa mkubwa wa muziki wa Punjabi na filamu za Bollywood, ilikuwa mfano wa ubunifu wa kuvuka tamaduni. Diljit ni moja ya nyota wakubwa wa India na amewahi kushiriki kwenye filamu za Netflix na kolabo hiyo ilimpa nafasi ya kufanya shoo Dubai, Abu Dhabi na India, ambako muziki wa Punjabi una mashabiki wengi.

Faida kubwa ilikuwa ni kuongeza wigo wa hadhira yake na kuthibitisha muziki wa Bongo Fleva unaweza kuunganishwa na tamaduni nyingine bila kupoteza ladha yake. Hata hivyo, baada ya ngoma hiyo ilifungua fursa kwa muziki wa Bongo Fleva na mwaka huu Rayvanny alifanya kolabo na Nora Fatehi na Shreya Ghoshal kwenye remix ya wimbo wa Ooh Mama Tetema uliofanya vizuri duniani.

DIA 07

7. Komasava – ft Jason Derulo, Khalil Harisson na Chley

Wimbo huo ulitoka mwaka jana na Diamond aliwashirikisha wasanii watatu Derulo msanii wa kimataifa kutoka Marekani na Khalil na Chley kutoka Afrika Kusini.

Ilifanya vizuri na kuingiza zaidi ya watazamaji Milioni 48 kwenye Youtube. Ingawa Derulo hajawahi kushinda tuzo kubwa kama Grammy lakini ni msanii mwenye mamilioni ya mauzo ya rekodi, mabilioni ya streams na mafanikio makubwa kibiashara, hasa kupitia nyimbo kama Whatcha Say, Talk Dirty na Savage Love.

Baadhi ya tuzo zake za muziki ni MTV Video Music Awards alinyakua mwaka 2010 na 2014 kama Best Male Video, Best New Artist, Best Pop Video na Best Choreography.