Kumbukumbu ya Hemedi Maneti na Halila Tongolanga
Muktasari:
- Usiku uleule kumbe aliongea na wanamuziki wenzangu wengine wa Tancut Almasi ambao walikubaliana kuhamia Vijana Jazz Band. Shaaban ‘Wanted’ Yohana, wakati huo hajaanza kuitwa Wanted kwani jina hilo lilitokana na harakati za Tancut Almasi Orchestra kujaribu kila njia kumrudisha Shaaban, na ndipo Maneti akampa jina la Wanted.
Dar es Salaam. Kwa mara ya kwanza nilikutana ana kwa ana na Hemedi Maneti ilikuwa mwaka 1989. Wakati huo nilikuwa mwanamuziki wa kundi la Tancut Almasi Orchestra. Vijana Jazz Band ilikuwa safarini kuelekea kwenye onyesho lao Songea, na kama ilivyokuwa ada miaka ile, bendi ikipita katika mji ambao kuna bendi wanamuziki walikuwa wakipiga muziki pamoja. Vijana Jazz Band chini ya Hemedi Maneti walitutembelea katika ukumbi wetu na kupiga nyimbo kadhaa. Tulikaa pamoja pembeni, tukiwa na Kida Waziri na tukaongea mambo kadhaa kuhusu muziki wa Tanzania.
Jambo moja alilofurahia ni setting ya muziki wa bendi yetu ambapo alisifu kuwa kila chombo kilikuwa kikisikika vizuri kabisa. Kwa vile mimi ndio nilikuwa fundi mitambo wa bendi alinisifia kwa kazi hiyo.
Usiku uleule kumbe aliongea na wanamuziki wenzangu wengine wa Tancut Almasi ambao walikubaliana kuhamia Vijana Jazz Band. Shaaban ‘Wanted’ Yohana, wakati huo hajaanza kuitwa Wanted kwani jina hilo lilitokana na harakati za Tancut Almasi Orchestra kujaribu kila njia kumrudisha Shaaban, na ndipo Maneti akampa jina la Wanted.
Pia waliokuwa katika mpango wa kuhama walikuwa Mohamed Gotagota na Mohamed Shaweji. Tena walikuwa wakitaka kuondoka na kujiunga na msafara wa kuelekea Songea mara moja, lakini ikaonekana ni ngumu hivyo wote waliondoka baada ya bendi kurudi Dar es Salaam. Katika mlolongo huohuo nilijikuta nikiitwa kujiunga na Vijana Jazz Band mwezi wa Septemba mwaka huohuo na kufikia Oktober 1989 niliwasili Dar es Salaam kujiunga na Vijana Jazz Band.
Tuliweza kurekodi album moja iliyokuwa na nyimbo kama Nyongise, Wifi Zangu, Siri ya Ndani, Heshima ya Ndoa na kadhalika, ndipo Hemedi alipoanza kuugua. Miezi michache baadaye, tarehe 31 Mei, 1990 siku ya Alhamisi majira ya saa kumi na moja jioni, Hemed Maneti alifariki katika hospitali ya Mwananyamala. Kesho yake mwili wake ulisafirishwa na akaenda kuzikwa Tanga.
Bendi ya jeshi iliyo na makao yake makuu kule Monduli, Les Mwenge, hukumbukwa sana kwa kibao chake kinachoitwa ‘Kila munu ave na kwao’ – kila mtu ana kwao. Kibao hicho cha Kimakonde ni utunzi wa marehemu Halila Tongolanga.
Baada ya wimbo huo kupata umaarufu mkubwa Tongolanga aliitwa kujiunga na bendi iliyokuwa mali ya Dr Alex Khalid, bendi iliyoitwa Makondeko Six na makao yake yalikuwa katika ukumbi wa burudani wa Makondeko, uliokuwa Kwembe, nyakati hizo ikiwa ni nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.
Kundi hili lilikuwa na wanamuziki wengine kama Innocent Nganyagwa, Anna Mwaole wakaweza kurekodi tena wimbo wa Kila Munu Ave na kwao na kundi kupata umaarufu mkubwa. Bahati mbaya Dr Alex Khalid alifariki na kundi kusambaratika, lakini Tongolanga aliendelea kutumia jina la Makondeko, na akaweza kurekodi nyimbo nyingine zilizopata umaarufu nchini na nchi jirani ya Msumbiji.
Tongolanga na mabingwa wenzie wa muziki kama Moshi William, Muhidin Mwalim, Huluka Uvuruge, Kandaya na wengine, waliunda kundi lililojikita kurekodi tu, lililojulikana kama Bana mwambe. Bendi hii iliweza kurekodi nyimbo nyingi nzuri sana wakati huo biashara ya kuuza album ilipokuwa ina faida.
Tongolanga aliaanza kuugua miezi ya kwanza ya mwaka 2017 akiwa kwao, alipozidiwa akapelekwa hospitali ya Ndanda, hali yake ilipoonekana inahitaji matibabu zaidi, Mbunge wa Tandahimba Mheshimiwa Katani Ahmed Katani aliwezesha Tongolanga kuhamishiwa Muhimbili, lakini pamoja na juhudi zote za kibinadamu, Tongolanga alifariki.
Wanamuziki kadhaa walikusanyika kuuaga mwili wa Tongolanga pale Muhimbili, lakini pia serikali iliwakilishwa na Katibu Mtendaji wa BASATA.
Katika jambo moja kubwa lililotokea wakati wa kuaga mwili ni kujitokeza kwa balozi wa Msumbiiji Bi Monica Patricio Clemente aliyefika Muhimbili kuaga mwili wa Tongolanga akiwa amesindikizwa na maofisa wengine wa ubalozi huo. Balozi alitoa rambirambi zake kama Balozi na alitoa rambirambi kutoka kwa Waziri wa Ulinzi wa Msumbiji. Taarifa zilizopatikana pale ni kuwa Tongolanga alikuwa mtu maarufu sana nchini Msumbiji, na alikuwa ni msanii muhimu wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu nchini humo.
Halila Tongolanga alizikwa Mchichila tarehe 6 Juni 2017.
Mungu awalaze pema Hemed Maneti na Halila Tongolanga.