Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Anko Kitime: Tumerudi tulikotoka?

Muktasari:

  • Katika muda huo,  muziki wa aina hiyo katika zama mbalimbali umekuwa unaandamana na mambo mengi sana ambayo mengine yamebadilisha muziki, na matukio mengine yamewabadilisha wapenzi na wadau wa muziki

Dar es Salaam. Nimekuwa nikijihusisha na muziki wa majukwaani, maarufu kama muziki wa dansi, kwa namna moja au nyingine hasa kuanzia mwaka 1968.

Katika muda huo,  muziki wa aina hiyo katika zama mbalimbali umekuwa unaandamana na mambo mengi sana ambayo mengine yamebadilisha muziki, na matukio mengine yamewabadilisha wapenzi na wadau wa muziki. Na kuna matukio mengine ambayo yaliwabadilisha wanamuziki wenyewe.

Labda turudi nyumba kabla ya Uhuru. Muziki katika zama hizo haukuchukuliwa kama kitu ambacho kingeweza kukidhi gharama za maisha. Muziki ulichukuliwa kama burudani kwa wanamuziki na wapenzi na wadau mbalimbali wa muziki.

Vikundi vingi vya muziki vilitambulika kama ni klabu. Vyombo vya muziki mara nyingi pia vilikuwa mali ya klabu. Maonyesho mengi ya bendi yalifanywa kwa ajili ya sherehe za wanachama wa klabu, kama vile harusi na kadhalika. 

Katika maonyesho ambayo kwa namna moja au nyingine fedha zilipatikana, mapato hayo yalikuwa ni mali ya klabu na mapato yalitumika kadri ya maamuzi ya viongozi wa Klabu. 

Kama mwanamuziki alionekana anahitajika sana kwenye bendi, aidha klabu au mwanachama mmoja wa klabu  alimtafutia chumba cha kuishi na mara nyingine pia alitafutiwa hata kazi. Ratiba za mazoezi zilikuwa mara nyingi jioni wakati kila mtu amekwisha maliza kazi zake za ajira.

Tukio lililoanza kubadilisha mfumo huo ni ujio wa bendi za Kikongo. Vikundi vya muziki vya nyumbani vikaona vikundi vya kigeni vikiishi kwa kutegemea muziki tu. Taratibu na vikundi vya nyumbani vikaanza kuiga mfumo wa utawala kama vikundi vya Kikongo.

Katika kipindi hicho ikawa ndio awamu ya kwanza ya bendi za hapa nchini kuanza kuiga taratibu za muziki wa Kikongo. Ukaanza mfumo wa kuiga kutoka  Kongo kila kitu. 
Uvaaji, upigaji wa muziki na hata ukaanza utaratibu wa kuiga nyimbo za kutoka Kongo na kuziimba kwa tungo za Kiswahili. Nyimbo kama, Nacheka Cheka Kilwa Leo wa Kilwa Jazz Band, National Service wa NUTA Jazz Band, Lau Nafasi wa Kilwa Jazz Band na nyimbo nyingine nyingi kutoka bendi mbalimbali zikarekodiwa katika mfumo huo. 

Bahati nzuri serikali ya wakati uke ikaamua kuingilia kati na wanamuziki waliitwa na kushauriwa kuacha kuiga moja kwa moja nyimbo za bendi.  Kwa kufuata ushauri huo, hakika kilianza kipindi ambacho bendi za Tanzania ziliweza kuja juu na kuwa bendi pendwa Afrika Mashariki. 

Wapenzi walimiminika katika kumbi za muziki, ushindani ulikuwa mkubwa, ushindani ambao ulileta maendeleo chanya katika tasnia ya muziki. Karibu kila mji mkubwa ulikuwa na bendi japo moja, na kila bendi ikijitahidi kupiga muziki wa aina yake, hakuna bendi mbili zilizofanana, ilikuwa ni wakati mzuri kwa wanamuziki na wapenzi wa muziki. Ushabiki wa bendi ulikuwa mkubwa kila upande ukisisitiza kuwa bendi yao ndio bora. 

Moja kati ya tishio kubwa lililoleta mtikisiko katika utawala wa muziki wa bendi, ni ujio wa muziki wa  Disco. Disco liliingia kwa nguvu nchini katika miaka ya sabini, japo lilikuwako kabla ya hapo kwa jina jingine, kwenye shule hasa za sekondari. Mfumo wa kupiga santuri ulikuwa unaitwa ‘social evening’. 

Miaka hiyo ya sabini muziki huo uliingia na kufanywa maarufu zaidi baada ya filamu ya Saturday Night Fever ambayo alishiriki John Travolta na filamu ya Kihindi iliyoitwa Disco Dancer ambayo alishiriki Mitun Chakraboty, vijana walipagawa na muziki wa disco, kumbi za muziki wa dansi zikaanza kupungukiwa na wapenzi. 

Bendi ambazo zilikuwa zikipiga muziki wa rumba tu, zikaanza kufanya mazoezi nyimbo maarufu za Disco, ili kushawishi wapenzi wa disco kujiona wakiingia katika kumbi za dansi wanapata muziki wa rumba na pia muziki wa disco.

Kulikuwa na kumbi zilizojengwa maalumu kwa ajili ya disco, kumbi kama Gogo, Mbowe, Msasani Beach Club, Rungwe Oceanic zilipambwa kwa taa za rangi maalumu kwa disco na hakika zilifanikiwa.  Wadau wa disco, walifanya mashindano na matamasha ya kuvutia na hakika Disco lilitemba. Lakini hatimae bendi ziliweza kuinuka na kuendelea na utawala wake.

Kuruhusiwa kwa vyombo huru vya utangazaji, kulileta furaha kwa wanamuziki. Mawazo yalikuwa vyombo hivyo vitajikita katika kuunga mkono muziki wa nyumbani, kumbe ilikuwa ni ndoto. 

Muziki kutoka nje ndio uliopewa kipaumbele. Hata maonyesho ya wanamuziki kutoka Kongo yakaongezeka sana. Leo Kand bongoman, kesho Pepe Kalle  hakika uwanja ukachangamka sana kwa upande wa muziki kutoka Kongo. Wakati huohuo wasambazaji wa kanda za kaseti na CD nao walikuwa wakisambaza muziki huo kwa ufanisi. Vita ikawa kubwa sana kwa bendi za nyumbani. 

Vita hiyo ikiwa wazi  hadharani kulkawa na vita nyingine ya chini chini, gonjwa la UKIMWI likaanza kupukutisha wanamuziki maarufu. Hakika miaka kuanzia mwaka 1990 na kuendelea ilikuwa ni mibaya sana kwa tasnia ya muziki wa dansi.

Bendi chache zikaanza kubadili muziki wake na kuiga muziki uliokuwa unapigwa  katika vyombo vya utangazaji. Ile hali iliyokuwa ikitawala miaka ya 60 ikarudi tena, bendi zikarudia tena kuwa kivuli cha muziki wa Kongo.

Hakika ni bendi chache sana ambazo zina muziki wake siku hizi, asilimia kubwa ya bendi ni mabingwa kupiga, kuimba na kucheza kama bendi za sasa za Kongo. Na safari hii sioni uwezekana wa serikali kuingilia mtiririko huo.