Nigeria kama Marekani, mabifu kila kona

Mwanamuziki wa Nigeria, Kizz Daniel amezua mijadala baada ya majibizano yaliyotokea kati yake na msanii mwenzake Tekno huku mashabiki wakidai kuwa Kizz alimtumia Tekno kuingiza maokoto kupitia wimbo wao wa ‘Buga’.

Minong’ono hiyo ilianza baada ya ujumbe uliokuwa ukisambaa katika mtandao wa X (zamani Twiter) ambao umeeleza kuwa Tekno aliwahi kusema kuwa amekuwa akipatiwa asilimia 50 ya mapato kutoka wimbo wa ‘Buga’ hata baada ya mafanikio ya ziara yake alimtumia Naira bilioni 1 sawa Sh 1.8 bilioni huku akimlipa kila mwezi mapato yote anayoyapata kwenye Streaming Platforms.

Kutokana na ujumbe huo Tekno aliamka na kukanusha taarifa hiyo kupitia ukurasa wake wa X akidai kuwa taarifa hiyo haina ukweli wowote huku akienda mbali zaidi na kudai kuwa Kizz Daniel hana fedha za kumlipa yeye.

Aidha Kizz naye hakulikalia kimya suala hilo ambapo aliamua kujibu akimtaka msanii huyo aache kumzungumzia kwani yeye ndiyo amemsaidia kurudi tena mjini kupitia wimbo wake wa ‘Buga’, hata hivyo Tekno alimjibu kwa kumwambia pia na yeye amuache kwa sababu ana siri zake nyingi atakuja kumdhalilisha.

Kizz Daniel na Tekno wamewahi kutoa ‘kolabo’ ya pamoja ya wimbo wa ‘Buga’ ambao ulitrend zaidi kupitia mitandao ya kijamii yenye zaidi ya watazamaji milioni 200 kupitia mtandao wa YouTube ikiwa na mwaka mmoja tuu tangu kuachiwa kwake.

Wiki hii nchini Nigeria kumeibuka mabifu kadhaa miongoni mwa wasanii ikumbukwe kuwa siku kadhaa zilizopita mwanamuziki Davido na Wizkid wamekuwa wakirushiana madongo kupitia mtandao wa X (zamani twiter) huku Davido akienda mbali zaidi akitaka yeye na Wizz watoe ngoma siku moja ili ijulikane nani mkali zaidi.