Nyuma ya moto wa Robert Lewandowski, kuna huyu mrembo
Muktasari:
- Lewandowski, 36, amekuwa bora tangu akiwa Ligi Kuu Ujerumani (Bundesliga) akizichezea klabu za Borussia Dortmund na Bayern Munich lakini nyuma ya mafanikio yake kuna Anna Lewandowska ambaye ni mtaalam wa mazoezi na lishe pamoja na michezo.
Ulaya. Mshambuliaji wa FC Barcelona, Robert Lewandowski ndiye kinara wa upachikaji mabao katika Ligi Kuu ya Hispania (La Liga) ndani ya kipindi cha miaka mitano iliyopita akienda kambani mara 69 ikiwa ni sawa na Karim Benzema, mchezaji wa zamani wa Real Madrid.
Lewandowski, 36, amekuwa bora tangu akiwa Ligi Kuu Ujerumani (Bundesliga) akizichezea klabu za Borussia Dortmund na Bayern Munich lakini nyuma ya mafanikio yake kuna Anna Lewandowska ambaye ni mtaalam wa mazoezi na lishe pamoja na michezo.
Mbali na taaluma yake, kazi na biashara, Anna, 36, ni mke na mama watoto wa Lewandowski wakiwa wamedumu katika ndoa kwa zaidi ya miaka 10 sasa na tayari wamejaliwa kupata watoto wawili, Klara (2017) na Laura (2020).
"Tumekuwa tukichambua mechi za Lewandowski pamoja kila mara. Yeye hupiga simu baada ya mechi za ugenini ambazo sikuhudhuria na hutaka kusikia maoni yangu," anasema Anna na kuongeza.
"Ninao mtazamo tofauti na wake, lakini pia nimetoka kwenye michezo ya ushindani na nimesomea masuala ya michezo. Ni kama majadiliano ya kiufundi kati ya wanamichezo wawili," alieleza Anna.
Kauli ya Anna ilikuja baada ya Lewandowski kuwa ni msimu bora kabisa ndani ya Bundesliga chini ya Bayern ambapo msimu wa 2019/2020, alifunga mabao 34 ya Ligi, sita ya Kombe la DFB na 15 ya Ligi ya Mabingwa Ulaya (UEFA CL).
"Lewandowski hajawahi kuridhika kwa asilimia 100 na utendaji wake, hata kama akifunga mabao mawili, husema alipaswa kufunga moja au mawili zaidi. Anajitazama kwa jicho la ndani sana. Na tamaa yake ya kufanikiwa ni kubwa mno," anaeleza Anna.
Inaripotiwa kuwa uhusiano wa Anna na Lewandowski ulianzia mwaka 2008 kabla hata ya mchezaji huyo kutimkia Bundesliga. Walifunga ndoa Juni 22, 2013 katika Kanisa la Catholic huko Serock, Poland ambapo wote wanatokea.
Mnamo Desemba 2016, miaka miwili baada ya kujiunga na Bayern akitokea Dortmund, Lewandowski alitangaza kuwa Anna alikuwa mjamzito na alikuwa na ujauzito wa miezi mitano.
Anna alikuja kujifungua binti yao, Klara hapo Mei 4, 2017. Na kufikia Novemba 2019, akathibitisha kuwa Anna alikuwa mjamzito kwa mara ya pili - binti yao wa pili, Laura alizaliwa Mei 6, 2020.
Lakini huyu Anna Lewandowska ni nani hasa?, mrembo huyu alizaliwa Septemba 7, 1988 huko Lodz nchini Poland. Wazazi wake ni Bogdan Stachurski na Maria ingawa hakuna taarifa nyingi mtandaoni kuwahusu.
Ni mhitimu kutoka Chuo cha Warsaw ambapo alisomea masuala ya afya na mazoezi ya mwili lakini kwa asilimia kubwa ametumia muda wake mwingi katika mchezo wa karate akishinda medali nyingi katika mashindano ya Dunia, Ulaya na ya kitaifa.
Kwa ujumla, ameshinda medali 38 za karate kutoka katika mashindano ya kitaifa na kimataifa kitu ambacho kimpa heshima kubwa sio kwao Poland pekee bali duniani kote. Hata hivyo, aliamua kupumzika kutoka kwenye mchezo huo baada ya kujifungua mtoto wake wa kwanza.
Wakati akiwa katika ubora wake, alishinda medali tatu katika mashindano ya dunia kwa watu wazima, medali sita za mashindano ya Ulaya katika makundi tofauti ya umri - ikiwa ni pamoja na mbili kwa watu wazima, na medali 29 za mashindano ya kitaifa ya Poland.
Septemba 2013, alianza kutoa elimu ya lishe baada ya kuanzisha blogu yake iitwayo Healthy Plan by Ann, inayotoa ushauri wa lishe na mipango mizuri ya mazoezi.
Mwaka 2014, alichapisha kitabu chake cha kwanza "Zyj zdrowo i aktywnie z Anna Lewandowska" (ishi kwa afya na kwa uchangamfu pamoja na Anna Lewandowska), ambacho kinawahamasisha wasomaji kubadili tabia zao za ulaji.
Pia kitabu hicho kinafundisha aina mbambali za mapishi ya vyakula kutoka makundi tofauti, pamoja jinsi ya kufanya mazoezi katika mtindo bora unaozingatia afya huku akitoa uzoefu wake wa miaka mingi katika eneo hilo.
Mwaka 2016, Anna alianzisha chapa yake ya kuuza vyakula, Foods by Ann, inayouza vitafunwa vyenye virutubisho lishe. Na pia ana chapa yake ya vipodozi iitwayo Phlov, pamoja na studio ya mazoezi aliyoifungua huko Barcelona mwaka jana.
Wakati dunia ikipambana na virusi vya Corona, Anna na Lewandowski walichangia Euro 1 milioni kusaidia mapambano hayo hapo Machi 2020. Taarifa ya wanandoa hao kwa umma ilieleza sababu ya kufanya hivyo.
"Leo, sote tunatambua ugumu wa hali inayotuzunguka. Leo, wote tunacheza katika timu moja. Tuwe imara katika mapambano haya na tuwe wamoja. Ikiwa tunaweza kumsaidia mtu kwa usalama, tufanye hivyo. Wema hurudi."
"Hali hii inatuathiri sisi sote, haichagui, hivyo tunawaomba tena: Tufuate maelekezo, tusikilize wanaofahamu vyema mambo haya," walieleza katika taarifa yao.
Akiwa na wafuasi zaidi ya milioni 5.7 katika ukurasa wake wa Instagram, Anna si tu chapa yenye nguvu ya ushawishi mtandaoni, bali amekuwa sehemu ya usukumo wa mafanikio ya Robert Lewandowski tangu akiichezea Lech Poznan ya huko kwao Poland.