Rayvanny kamuongezea Dayoo mamilioni

Muktasari:

  • Utakumbuka Dayoo alianza kuchukua usikivu wa wengi katika Bongo fleva alipotoa wimbo wake, ‘Nikuone’ (2022), ambao pia ulikuwa na remix akimshirikisha Kusah, kisha kolabo yake na Young Lunya, ‘Handsome’ (2022), ikamsogeza mbele zaidi. 

Dar es Salaam. Mwimbaji wa Bongo fleva, Dayoo amesema kitendo cha kumshirikisha Rayvanny katika wimbo wake ‘Huu Mwaka Remix’ kinaenda kuongeza thamani yake katika soko na kutoka kufanya shoo kwa Shilingi  6 milioni na kwenda bei ya juu zaidi.

Amesema ilikuwa ni ndoto yake siku moja kutengeneza wimbo mkubwa kama huo ambao utamfanya apige hatua kubwa kimuziki, kiuchumi na kichapaa, huku akiwasihi vijana wanaopambania ndoto na vipaji vyao kutokata tamaa. 

Utakumbuka Dayoo alianza kuchukua usikivu wa wengi katika Bongo fleva alipotoa wimbo wake, ‘Nikuone’ (2022), ambao pia ulikuwa na remix akimshirikisha Kusah, kisha kolabo yake na Young Lunya, ‘Handsome’ (2022), ikamsogeza mbele zaidi. 

Akizungumza na Mwananchi, Dayoo amesema ‘Huu Mwaka’ ulikuwa ni miongoni mwa nyimbo ambazo yupo nazo kwa muda mrefu, ila ilitokea siku moja akiwa studio akaukumbuka na kuamua kuurekodi na sasa ni habari nyingine.

“Nilikuwa nipo studio namalizia kazi, katika kutazama nyimbo ambazo nimekuwa nikirekodi kupitia simu nyumbani ndipo nikakutana na huu wimbo, kwa hiyo nikaona ni kitu kizuri, nikarekodi kama masihara hivi na ndiyo ukawa wimbo mkubwa,” alisema.

“Umenipa mafanikio makubwa, umeniheshimisha, lakini pia umenipa kolabo kubwa na Rayvanny hadi wasanii wengi wakubwa kuanza kuniamini, kwa hiyo naweza kusema ndiyo ngoma iliyonipa mafanikio makubwa zaidi tangu nimeanza muziki,” anasema Dayoo.

Je, ilikuwaje hadi staa huyo wa Next Level Music (NLM) kusikika katika remix ya wimbo huo? Dayoo anasema licha ya awali kumtumia, ulipotoka na kupata mapokezi mazuri ndani ya muda fupi uliongeza ushawishi kwa Rayvanny kushiriki.

“Rayvanny ndiye msanii wa kwanza ambaye nilimtumia kabla hata wimbo wenyewe haujatoka, baadaye ulipotoka na kuanza kufanya vizuri katika mitandao ya kijamii akaupenda, hivyo ikawa rahisi kufanya naye kazi,” alisema Dayoo.

“Natamani kuendelea kufanya kazi na wasanii wengi Mungu akiendelea kunibariki, siwezi kuwataja kwa sasa maana sijui muziki wangu utafika wapi, ila bado nataka kuendelea kushirikiana na wasanii wote wanaofanya vizuri nchini,” anaeleza.

Hata hivyo, wimbo ‘Huu Mwaka Remix’ na video yake vyote vipo katika YouTube chaneli ya Rayvanny ambaye kashirikishwa tu, Dayoo anasema hilo limetokea kutokana na makubaliano yao ya kibiashara. 

“Makubaliano yote kati yetu yapo kwenye mikataba, hivyo sitapenda kuliongelea sana maana vitu vipo kwenye mikataba tayari kwa maslahi ya pande zote mbili.”

Hadi sasa tangu kuachiwa kwa lyric video ya wimbo ‘Huu Mwaka Remix’ Januari 12, 2024, tayari umefikisha ‘views’ zaidi ya milioni 2.3 YouTube na kuwa wa kwanza wa Dayoo wenye namba kubwa zaidi katika mtandao huo.

Ikumbukwe Rayvanny amesikika sana kwenye remix za nyimbo za wasanii wenzake, baadhi ya hizo ni Mapopo (2020) wa Mavokali, Sukuma Ndinga (2021) wa Rosa Ree, Jennifer (2021) wa Guchi, Hi Hi Hi (2023) wa Lil Jay Bingerack, Kibela (2023) wa Chino Kidd .

Rayvanny, aliyetoka kimuziki na wimbo wake, Kwetu (2016) chini ya WCB Wasafi, ni msanii mwenye mashabiki wengi nchini na kimataifa aliposhinda tuzo kama BET (Marekani) 2017, Zikomo (Zambia) 2022, Afrimma (Marekani) 2022, EAEA (Kenya) 2022, DIAFA (Dubai) 2022, hivyo Dayoo amepanua wingo wa kusikika kwake.

Dayoo anasema baada ya wimbo ‘Huu Mwaka’ kufanya vizuri, kilichobaki sasa ni yeye na ‘menejimenti’ yake kukaa na kupanga bei mpya ambayo atakuwa anatoza katika shoo zake tofauti na ile ya awali ya Sh6 milioni.

“Gharama za shoo tangu nimeanza kufanya vizuri kwenye muziki nilikuwa natoza Sh6 milioni, ila kwa sasa tangu nimetoa wimbo huu mpya ina maana kiwango changu kimepanda japo bado sijafanya mabadiliko ya bei za shoo hadi nikitulia na timu yangu tupange,” anasema Dayoo.

Ni wazi muziki unampa maisha kijana huyo ambaye ndoto yake tangu akiwa mdogo ilikuwa ni kuja kuwa mwanamuziki mkubwa nchini, mazingira aliyokulia yaliotesha na kuikuza ndoto hiyo na sasa matunda yameanza kuonekana.  

“Kitu ambacho kimefanya nikaingia kwenye muziki, kwanza nilikuwa naupenda kwa muda mrefu, na pili, nimezaliwa katika maisha ambayo mama yangu alikuwa akiamka asubuhi anapiga muziki maana kwetu kulikuwa na klabu ya kuuza pombe,” alisema.  

“Hivyo mazingira hayo yalinifanya nikaanza kuupenda muziki tangu nikiwa mdogo, ilikuwa nikiamka muziki unapigwa hadi muda wa kulala bado ni muziki tu, kuanzia hapo nikavutiwa na muziki hadi nikaanza kuimba.”

Anasema mwaka 2019, akiwa Temeke ndiyo alirekodi wimbo wake wa kwanza ‘Tulia’ baada ya watu kuona uwezo wake na kuchangia gharama za studio. Hata hivyo, anakiri kuwa wimbo wake, Nikuone (2022) ndiyo ulimfungulia milango kimziki, tangu hapo mambo yakabadilika.  

“Muziki umebadilisha kila kitu kwenye maisha yangu, naweza kusema kwa vijana ambao wanapambana mtaani kwa ajili ya vipaji vyao waendelee, maana kila kitu kinawezekana, muziki unabadilisha maisha yangu kabisa, nimekuwa shuhuda wa hiki kitu,” anasema.

“Nashukuru Mungu nimejichanga nimenunua gari, naishi sehemu nzuri, familia yangu inaishi sehemu nzuri, hivyo mashabiki waendelee kuniunga mkono katika kazi zangu nyingine zitakazokuja mbeleni,” anasema Dayoo.

Dayoo anasema mipango yake kwa sasa ni kuandaa albamu au EP kwa sababu tayari ameshatengeneza kundi kubwa la mashabiki ambalo ni wazi linategemea mambo makubwa kutoka kwake, hivyo mwaka huu atajitahidi kuwapa kile wanachotaka.

“Ndiyo nitatoa kwa sababu awali ilikuwa ni ndoto yangu siku moja nipate wimbo utakaofanya vizuri na watu wengi kunitambua, hivyo baada ya kutambulika nitatoa hiyo albamu na vitu vingi vikubwa ambavyo nilikuwa na ndoto navyo mwaka huu nitavifanikisha,” alisema.

Katika safari yake ya elimu, Dayoo anasema alisoma shule ya msingi Kipunguni, IIala, Dar es Salaam, mwaka 2015 ndiyo alipaswa kuhitimu kidato cha nne ila hakuweza kufanya mitihani kutokana na changamoto zilizojitokeza ambazo hajapenda kuziweka wazi.

Ukiachana na Rayvanny, Kusah na Young Lunya, tayari Dayoo ameshirikiana na wasanii wengine Bongo kama Nedy Music, Kontawa, DJ Seven, Bonge la Nyau, Rasco Sembo, Bando, Mr. LG, Lody Music na Harmonize katika albamu ya P-Funk Majani, Majani (2023).