Ricardo Kaka aliachana na Caroline akaoa Carolina
Muktasari:
- Carolina ni miongoni mwa wanamitindo maarufu zaidi kutokea Amerika Kusini akijivunia kazi yake yenye mafanikio makubwa lakini kwa upande wa pili wa maisha ni rafiki, mke na mshirika wa karibu wa Kaka aliyestaafu soka 2017.
Uingereza. Wiki iliyopita kiungo mshambuliaji wa zamani wa AC Milan na Real Madrid, Ricardo Kaka (43), alisherehekea siku ya kuzaliwa ya mkewe Carolina Dias (30) ambaye wamekuwa pamoja kwa takribani miaka 10 ikiwa ni ndoa ya pili kwa mchezaji huyo wa Brazil.
Carolina ni miongoni mwa wanamitindo maarufu zaidi kutokea Amerika Kusini akijivunia kazi yake yenye mafanikio makubwa lakini kwa upande wa pili wa maisha ni rafiki, mke na mshirika wa karibu wa Kaka aliyestaafu soka 2017.
"Hii ni siku ya kuzaliwa ya tisa tunaisherehekea pamoja. Nilipokutana nawe ulikuwa na umri wa miaka 21, mzuri, umejaa nguvu na ujasiri. Leo unatimiza miaka 30 ukiwa na nuru ya mtu anayetembea na Kristo na ukiwa mzuri zaidi," alisema Kaka wakati akimtakia heri ya kuzaliwa mke huyo.
"Pamoja tumeendelea kujenga na kukusanya kumbukumbu zisizosahaulika ufukweni, kwenye theluji, shambani, angani na popote pale. Bwana akufunike kwa neema, akuongoze katika kila hatua na akufanye ujazwe furaha tele," Kaka alieleza kupitia Instagram. Ikumbukwe Kaka ni miongoni mwa wachezaji wachache wa Kibrazili waliowahi kutangaza kuwa wameokoka kiimani katika Ukristo.
Katika dunia ya sasa ambapo wake na wapenzi wa wachezaji wa soka hupata umaarufu kwa kuwaunga mkono wenza wao, kwa Carolina mambo ni tofauti kidogo. Kabla ya kukutana na Kaka tayari alishatengeneza jina lake kupitia mitindo na soka.
Carolina alikuwa shabiki wa soka tangu zamani na ameeleza mara nyingi kuwa alipenda kuhudhuria mechi akiwa na baba yake tangu utotoni.
Alikutana na Kaka 2016, yaani mwaka mmoja baada ya mchezaji huyo kutalikiana na mke wake wa zamani, Caroline Celico ambaye ndoa yao ilidumu kati 2005 hadi 2015 walipoachana wakiwa tayari na watoto wawili. Halafu usije kuchanganya mambo hapa mke wa kwanza wa Kaka ni Caroline na wa pili ni Carolina. Yaani kaachika Caroline kaolewa Carolina. Rapa Kontawa anasema mradi wa maji umesombwa na maji!
Kaka na Carolina wameendelea kuwa na uhusiano imara na hawajawahi kusita kuonyesha mapenzi yao hadharani hasa kupitia mitandao ya kijamii.
Wakiwa tayari na watoto wawili huhakikisha wanatoa muda wa kutosha kwa familia licha ya kazi zao zenye majukumu mengi. Wakiwa wamepishana miaka 13 ya kuzaliwa, wawili hao waliweka wazi uhusiano wao mwishoni mwa 2016 walipoonekana pamoja kwenye harusi ya mshambuliaji wa zamani wa Tottenham Hotspur, Lucas Moura.
Wakati huo Kaka alikuwa bado akicheza katika timu ya Orlando City huku Carolina akiwa shabiki wake uwanjani.
Walifunga ndoa Desemba 2019 na sasa ni wazazi wenye furaha wakiwa na mabinti wawili wadogo Esther na Sarah. Carolina alikuwa na ndoto ya kuwa mwanamitindo tangu utotoni na alianza kazi hiyo akiwa mdogo.
Alianza kama mwanamitindo huru kabla ya kusaini mkataba na Ford Modeling Agency hatua iliyompa nafasi kubwa ya kuingia rasmi katika tasnia hiyo.
Kupitia shirika hilo, mke wa Kaka amekuwa sura ya chapa kubwa za Brazil kama Eve Beauty na Easy Sim 4U na pia ameonekana kwenye majarida kadhaa makubwa huko Amerika Kusini.
Aidha, amejaribu pia biashara kama mwekezaji, akiwa msemaji na mshauri wa chapa za mitindo za Soller Assessoria na Choisir.
Mbali na kazi yake ya uanamitindo, Carolina pia ni mshawishi wa chapa kupitia mitandao ya kijamii akiwa na wafuasi zaidi ya 975,000 kwenye ukurasa wake wa Instagram.
Kupitia mitandao mara nyingi hupenda kushirikisha mashabiki wake maisha yake ya kila siku ikiwemo picha za familia na safari zake za kila mara akiongozana na familia yake.
Anaendelea kuwa mfano wa kuigwa kwa wanamitindo wachanga Amerika Kusini wanaotamani kufuata nyayo zake. Ni jambo la kuvutia kuona Kaka amepata tena mapenzi kupitia Carolina huku wawili hao wakiendelea kung’ara katika nyanja zao tofauti.
Baada ya Kaka kuachana na mkewe wa zamani na mpenzi wake wa utotoni, mashabiki walidhani hatapata tena upendo wa kweli, lakini sasa inaonekana yupo kwenye ndoa imara na maisha yanaendelea kama kawaida.
Ikumbukwe Kaka na mkewe wa zamani, Caroline, 38, walikutana 2002 alipokuwa na umri wa miaka 15 - ikiwa ni miaka mitano pungufu ya Kaka. Wakati huo bibie alikuwa anasoma katika shule ya St Paul’s mjini Sao Paulo huko kwao Brazil.
Walidumu kwenye uhusiano kwa miaka miwili kabla ya Kaka hajamposa kisha wakaoana 2005 Kaka akiwa na umri wa miaka 23 tu, wakati huo akiichezea AC Milan. Licha ya kuoana wakiwa bado vijana waliishi pamoja kwa miaka 10.
Kwa mujibu wa Caroline, Kaka alikuwa mwaminifu sana. Hakuwahi kumsaliti.
Alimpenda na kumjali sana na alimpa familia nzuri. Ila aliushangaza ulimwengu aliposema Kaka alikuwa 'mtu mkamilifu sana' kwake kiasi kwamba hakuona furaha ya ndoa hiyo na ndio sababu ya kuachana kwao!