Safari ya miaka 11 ya Angel Nyigu kwenye dansi
Muktasari:
- Kutoka kuwa msichana mwenye ndoto za kufanikiwa kupitia kucheza muziki. Hadi kuwa mmoja wa madansa wanaotambulika ndani na nje ya nchi. Safari yake imejaa changamoto, mafanikio na mafunzo mengi.
Dar es Salaam. Jina la Angel Nyigu limeendelea kuwa miongoni mwa majina makubwa katika tasnia ya dansi nchini Tanzania.
Kutoka kuwa msichana mwenye ndoto za kufanikiwa kupitia kucheza muziki. Hadi kuwa mmoja wa madansa wanaotambulika ndani na nje ya nchi. Safari yake imejaa changamoto, mafanikio na mafunzo mengi.
Akizungumza katika mahojiano na Mwananchi, Angel amesema mwaka huu anatimiza miaka 11 tangu aanze safari yake ya dansi. Kazi ambayo sasa imekuwa chanzo kikuu cha kuendesha maisha yake.
“Nilipoanza nilikuwa najifunza mwenyewe. Nilikuwa na ndoto kubwa tu kama vijana wengine wengi. Leo hii naweza kusema ndoto yangu ndiyo inaendesha maisha yangu kwa sababu imenipa fursa nyingi na inaendelea kunifungulia milango mbalimbali,” amesema.
Mbali na kujijengea jina, Angel amekuwa akitambulika kwa kuwapa nafasi madansa wachanga na kuwasaidia kujitangaza. Anasema kufanya hivyo si hasara kwake, bali ni sehemu ya ukuaji wa tasnia nzima.
“Dansi ni kusaidiana. Kumsaidia mtu mwingine ni dalili ya kukua kwangu . Hata kwenye muziki tunaona wasanii wakubwa wakiwashika mkono wachanga. Sanaa inatakiwa iwe hivyo,” amesema.
Hata hivyo, amesema moja ya changamoto kubwa zinazowakabili madansa nchini ni kukosa nafasi za kutosha pamoja na mtazamo hasi wa baadhi ya watu katika jamii.
“Bado kuna watu wanawadharau madansa na hawatupi hadhi inayostahili. Hiyo ni changamoto kubwa kwa vijana wengi wenye vipaji,” amesema.
Kutokana na hali hiyo, Angel anaamini elimu kwa jamii ndiyo njia muhimu ya kubadili mtazamo huo.
Amesema amekuwa akifikiria kuanzisha programu za uhamasishaji na mafunzo zitakazosaidia kuinua tasnia ya dansi na kuwajengea uwezo vijana wenye vipaji.
Kuhusu aina ya muziki anaoupenda kucheza zaidi, Angel amesema alianza safari yake kupitia Hip Hop kabla ya kuhamia Bongo Fleva na baadaye Singeli, ambayo kwa sasa ndiyo inayomvutia zaidi.
“Nilianza na Hip Hop, nikafanya Bongo Fleva na baadaye Singeli. Kwa sasa Singeli ndiyo muziki ninaoupenda zaidi kucheza,” amesema.
Kupitia ushirikiano wake na watu mbalimbali ndani na nje ya Tanzania, Angel amesema amejifunza umuhimu wa kujituma na kusimamia ndoto kwa vitendo.
“Nilichojifunza kwa wenzetu ni kwamba wakiamua kufanya jambo wanalisimamia mpaka lifanikiwe. Wanapokuwa kazini wanaweka moyo wao wote kwenye kazi,” amesema.
Licha ya mafanikio yake kwenye dansi, Angel amekiri kuwa aliwahi kuwaza kuingia kwenye muziki kama msanii wa kuimba. Hata hivyo, amesema kwa sasa hana mpango huo.
“Nilikuwa natamani kuimba zamani, lakini kwa sasa mimi ni dansa tu. Nimejikita kwenye kile ninachokifanya,” amesema.
Akizungumzia mtazamo wa baadhi ya watu wanaodhani dansi si ajira rasmi, Angel amesema hali hiyo imebadilika kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na miaka ya nyuma.
“Kwa mwaka 2026 siwezi kusema dansi haina heshima. Watu wengi wanaendesha maisha yao kupitia dansi. Wapo wanaosoma na kupata vyeti vya taaluma hii. Tatizo ni kwamba Afrika bado watu wengi hawajaielewa vizuri,” amesema.
Katika kumbukumbu zake za kazi, Angel amesema ameshiriki maonyesho mengi makubwa. Lakini moja ambalo hawezi kulisahau ni alilofanya pamoja na msanii Zuchu nchini Uganda.
“Show ya Uganda niliyofanya na Zuchu ni moja ya kazi ambazo siwezi kuzisahau kabisa,” amesema.
Kwa madansa wachanga wanaojitahidi kutafuta nafasi kwenye tasnia hiyo, Angel ana ushauri wa kutokata tamaa.
“Waendelee kupambana na kukomaa. Wasikate tamaa kwa sababu ipo siku kila kitu kitaeleweka na juhudi zao zitalipa,” amesema.