Shakira afichua kilichomvutia kwa Ghetto Kids
Muktasari:
- Shakira amesema safari yake ya kuwafahamu watoto hao ilianza baada ya kutazama video walizokuwa wakifanya wakicheza chalenji ya wimbo wa 'Dai Dai' ambao ndio ngoma maalumu ya Kombe la Dunia 2026.
Colombia. Mwanamuziki maarufu kutoka Colombia, Shakira, ameeleza sababu zilizomfanya kulialika kundi la watoto wanaocheza dansi la Ghetto Kids kutoka Uganda kushiriki naye kwenye Halftime Show ya fainali ya Kombe la Dunia 2026.
Shakira amesema safari yake ya kuwafahamu watoto hao ilianza baada ya kutazama video walizokuwa wakifanya wakicheza chalenji ya wimbo wa 'Dai Dai' ambao ndio ngoma maalumu ya Kombe la Dunia 2026.
Amesema alivutiwa na namna walivyokuwa wakionesha ubunifu mkubwa licha ya kutumia mazingira na vifaa vya kawaida, jambo lililomfanya aanze kuwafuatilia kwa karibu.
Kwa mujibu wa Shakira, baada ya kufahamu zaidi kuhusu maisha yao, aligundua kuwa wengi wa watoto hao wanatoka katika mazingira yenye changamoto kubwa za kiuchumi, huku baadhi yao wakiwa wamekumbwa na changamoto za kukosa malezi ya wazazi.
Msanii huyo amesema vipaji vya Ghetto Kids vilimvutia kwa kiasi kikubwa na kuamini kuwa walistahili kupata nafasi ya kuonesha uwezo wao mbele ya maelfu ya mashabiki.
"Nimekuwa nikitazama video nyingi nzuri za ngoma ya wimbo wa 'Dai Dai', wimbo rasmi wa Kombe la Dunia. Lakini nilivutiwa zaidi na watoto hao wana vipaji vikubwa na wamebadilisha kwa kiasi kikubwa maisha yetu nimekuwa nao kwa kipindi fulani," amesema Shakira.
Shakira alieleza kuwa simulizi ya maisha ya watoto hao ilimgusa kwa sababu ilimkumbusha maisha yake ya utotoni, ambapo alikulia katika mazingira kama hayo.
Mbali na kuwaalika kushiriki kwenye onyesho hilo, Shakira amesema ataendelea kuwaunga mkono kupitia taasisi yake ya Barefoot Foundation, aliyoianzisha mwaka 1997 kwa lengo la kuwasaidia watoto wanaotoka katika mazingira yenye uhitaji kupata elimu bora na fursa za kujenga maisha yao.
Watoto hao nane wametokea kwenye video ya wimbo wa 'Dai Dai' pamoja na kupanda jukwaa moja na Shakira na Burnaboy.
Mbali na Kombe la Dunia, watoto hao pia walipata bahati ya kutumbuiza na mwanadada huyo kwa mara nyingine kwenye ziara yake ya Las Mujeres Ya No Lloran World Tour, ambapo alifanya maonyesho mawili yaliyofanyika Julai 20 na 21, 2026.
Walipopanda jukwaani mashabiki waliwashangilia watoto hao walionyesha shoo ya kiwango kikubwa na baada ya kumaliza kucheza walimwita Shakira 'The Queen'.
Naye Shakira amesema: "Ghetto Kids kutoka Uganda wamebadilisha maisha yetu. Kutumia muda pamoja nao kumekuwa jambo la tofauti sana na wametufundisha mengi sana."