Taylor Swift wa moto Billboard, ajaza ngoma zake

Mwanamuziki kutoka nchini Marekani Taylor Swift ameutawala mtandao wa Billboard Hot 100, baada ya nyimbo zake 10 kuingia katika chati ya Billboard Top 10, ngoma hizo pia zipo katika album yake mpya ya ‘The Tortured Poets Department’.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram Taylor ametoa shukrani zake za dhati kwa mashabiki zake kwa sapoti wanayompatia na kuendelea kumkuza kimuziki huku akidai kuwa haamini kama amefanikiwa kuingia tena katika hatua hii ya kihistoria.

Mwanamuziki huyo ameitawala chati hiyo kupitia nyimbo zake 10 ambapo wimbo wa kwanza kushika chati ukiwa ni ‘Fortnight’ aliyomshirikisha Post Malone. Album hiyo yenye nyimbo 16 iliachiwa rasmi Aprili 19 mwaka huu.

Hii si mara ya kwanza kwa Swift kuweka historia kwenye chati hizo mwaka 2022 aliitawala Billboard Hot 100 kupitia album yake iitwayo ‘Midnights’ ambapo nyimbo 10 zilifanikiwa kushika Billboard top 10.

Hayo siyo mafanikio pekee ambayo ameyapata Taylor Swift mwaka huu, kumbuka kuwa mwanzoni mwa Aprili Forbes iliripoti kuwa Swift ameingia katika orodha ya matajiri duniani akiwa na utajiri binafsi wastani wa Dola za Marekani 1.1 bilioni ikiwa ni sawa Sh2.5 trilioni huku idadi hiyo ya fedha ikimfanya kuwa mtu wa 2,545 kati ya 2,781 ya mabilionea wa mwaka 2024.