Tungo za mapenzi zinavyombeba Joh Makini

Muktasari:

  • Joh Makini, (43) aliyeanza muziki na kundi la River Camp mkoani Arusha, alitoka kimuziki na wimbo wake, Chochote Popote (2006) ambao ulijumuishwa katika albamu yake ya kwanza, Zamu Yangu (2007).

Msanii wa Hip-hop Bongo kutoka kundi la Weusi, Joh Makini anaendelea kubamba na wimbo wake mpya ‘Formula’ au ‘Moto ‘Zimelia’ akiwashirikisha Jay Melody na Bien ambaye ni mwanachama wa kundi la Sauti Sol nchini Kenya. Kitendo cha Joh Makini kuachia wimbo huo unaozungumzia mapenzi kwa ustadi mkubwa, ni wazi anaendelea kuenzi utamaduni wake na hasa kukumbuka kule alipotoka kimuziki takribani miaka 18 iliyopita. 

Joh Makini, (43) aliyeanza muziki na kundi la River Camp mkoani Arusha, alitoka kimuziki na wimbo wake, Chochote Popote (2006) ambao ulijumuishwa katika albamu yake ya kwanza, Zamu Yangu (2007). Wimbo huo uliotengenezwa na Dunga katika studio ya Madungu Digital ni wenye maudhui ya mapenzi kwa asilimia 100, uandishi na midondoko yake katika mdundo huo vikamfanya Joh Makini kupokelewa kwa mikono miwili ndani ya Bongofleva.

Tangu wakati huo Joh Makini amejenga utamaduni wa kutoa nyimbo za mapenzi walau moja kwa mwaka, kwa asilimia kubwa katika mashairi yake anamsifia yule aliyenaye kama ilivyokuwa kwa ‘Chochote Popote’, ni mara chache sana huimba kuhusu kuumizwa.

Huu ni mwaka 2024 anatamba na wimbo, Formula (Moto Zimelia) na hata mwakani huwenda akatoa wimbo mwingine wa mapenzi kama huu, siyo kwa bahati mbaya bali anajua ni sehemu kubwa ya biashara yake na mashabiki wanapenda kumsikia upande huo.

Mathalani tangu 2020 hadi 2024, hakuna mwaka uliopita bila kutoa wimbo wa mapenzi, alianza na Dangerous (2020) ft. Nahreel, Swagg (2021) ft. Nandy, Tanzanite (2022) ft. Jay Rox, Bobea (2023) na Formula (Moto Zimelia) (2024).Nyimbo zake nyingine za aina hiyo ni kama Sitochoka (2007) ft. Farida, Nikumbatie (2013) ft. Fundi Samweli, XO (2014) ft. G Nako, Unanichora (2014) ft. Ben Pol, Waya (2017), Mipaka (2017), Kiwembe (2020) ft. Lady Jaydee, Too Much (2023) ft. Damian Soul .

Hadi sasa video ya Joh Makini iliyotazamwa zaidi YouTube kwa muda wote ni ya wimbo wake, Perfect Combo (2016) ft. Chidinma ambao pia ni wa malavidavi ukiwa na ‘views’ zaidi ya milioni 1.7 tangu utoke miaka saba iliyopita. Kolabo hii ilikuja baada ya Joh Makini na Chidinma kutoka Nigeria kukutana Nairobi, Kenya kwenye msimu wa nne wa Coke Studio Africa 2016 ambapo walishirikiana kutumbuiza wimbo wake, Nikumbatie (2013).

Joh Makini ambaye ni mshindi wa tuzo ya TMA 2012 kama Msanii Bora wa Hip Hop, katika nyimbo zake hizo amekuwa akiitaja ‘couple’ maarufu duniani ya wasanii, Jay Z na Beyonce. Joh amefanya hivyo katika nyimbo zake kama Chochote Popote na Waya.Ikumbukwe Jay Z na Beyonce ambao ni wanandoa tangu mwaka 2008, tetesi za kuchipuka kwa penzi lao zilianza walipotoa kolabo yao ya kwanza, 03 Bonnie & Clyde (2002) iliyosampo wimbo wa 2Pac, Me and My Girlfriend (1996).

Video ya wimbo huo wa mapenzi ilifanyika Oktoba 2002 nchini Mexico, Jay Z anaonekana akiendesha gari aina ya Aston Martin Vanquish akiwa na Beyonce, ukitazama utajua siyo wasanii walioshirikiana tu, bali ni wapenzi kweli.Katika video hiyo Jay Z na Beyonce walicheza mfano wa tukio la ujambazi katika benki lilofanywa miaka ya 1930 na Clyde Barrow na Bonnie Parker (Bonnie & Clyde), kisa chake kinatokana na filamu ya uhalifu na mapenzi, True Romance (1993).

Mwaka 2003 video hiyo ilishinda tuzo za MTV kama Video Bora ya Hip Hop, huku 03 Bonnie & Clyde ikifika namba nne kwenye chati za Billboard Hot 100, ukiwa ni wimbo wa pili wa Jay Z kuingiza 10 bora ya chati hizo na wa kwanza wa Beyonce kama solo.