Tusijizime data kukumbatia mwonekano, kuacha vipaji

Muktasari:

  • Yupo wapi Lisa Jensen? Kaenda wapi Nargis Mohamed? Wote wametemana na sanaa hii. Huku halikuwa eneo lao sahihi. Nguvu ya sura na maumbile yao ndiyo iliyotaka wawe hapa ila siyo uwezo halisia na kiu ya sanaa.

Kuendekeza sura na mionekano kunaimaliza sanaa. Isiwe kitu cha kuchukuliwa juujuu tu. Kama kweli tuna uchu na maendeleo ya kweli ya sanaa hii kuna kitu tunatakiwa kufanya. Tunapwaya kwa sasa.

Kuna kitu kilikuwa kinashangaza. Wengine tulijiuliza kwa nini 'mamisi' wengi badala ya kuvamia mitindo wakavamia uigizaji? Katika hili haikuwa sahihi. Lakini ukweli ni kwamba sanaa ya uigizaji ilivamiwa na walimbwende.Yupo wapi Lisa Jensen? Kaenda wapi Nargis Mohamed? Wote wametemana na sanaa hii. Huku halikuwa eneo lao sahihi. Nguvu ya sura na maumbile yao ndiyo iliyotaka wawe hapa ila siyo uwezo halisia na kiu ya sanaa.

Tafakari kwa kina, kati ya uigizaji na uanamitindo ni wapi panapaswa kuwa rahisi kwa 'mamisi'? Wapi wanapaweza kwa ukaribu kama wakiamua? Walikataa katika mitindo wote wanapataka huku.

Soko la filamu lilikuwa juu. Siyo vibaya 'misi' kuwa mwigizaji. Hata India wamejaa waigizaji waliowahi kuwa 'mamisi' na wanafanya vizuri sana. Hapa hakuna tatizo.

Ila katika kustahili ndipo linapokuja tatizo lenyewe. Ndiyo ni mrembo, je, kweli anastahili kuwa mwigizaji? Kati ya wote walioingia katika uigizaji ni wachache sana wenye kuonyesha kufiti. Yupo Aunt Ezekiel, Irene Owoya, Wema Sepetu. Ila wengi ni kama walilazimisha.

Uigizaji ni fani tofauti sana na 'umisi'. Ipo tofauti ya muonekano na uigizaji.

Unamkumbuka Kemmy, yule mke wa Sembe katika mchezo wa ITV? Nani kama yeye sasa? Nani anaweza akafanya nusu ya kile alichokuwa anatuonyesha? Wengi wanabaki kuwa wasichana warembo ila vipaji vikiwa mbali na ukweli halisi.

Kutokana na hili ndiyo maana wanamuziki walikimbia kwa kasi kimaendeleo kuliko waigizaji. Leo tuna wanamuziki wa kimataifa. Leo kuna mapato makubwa kwenye muziki tofauti na kwenye filamu. Kuna kitu inabidi kitazamwe vizuri.

Wengi waliingia katika filamu si kwa sababu ya kupenda sanaa. Hawana huba wala mahaba na fani wala hawajawahi kuwa nayo. Walikuja kwa kasi kwa sababu wana kiu na njaa ya kutazamwa na wengi. Ni hilo tu.

Ndiyo maana hakukuwa na ubunifu, hawakusonga mbele, zaidi ni fulani katoka na fulani kila siku. Wakati mwingine fani hii inatia huzuni. Wapo wenye dhamira na vipaji vya kweli. Wengi wanaihusudu sanaa siyo kwa wito bali kwa mizuka ya mjini.

Waigizaji wenye ubora kina Ommy wapo, wakina Asha  wapo, ila kuna kundi lina nguvu fulani ni kama linataka hawa wasitambe. Linataka sura na mionekano mizuri. Wanataka sura za na maumbo ya mauzo mjini ili michongo iende.

Siyo mbaya, ila vipi kuhusu vipaji na weledi wa fani? Vipi kuhusu mafunzo katika jamii kama moja ya makusudio ya sanaa yanavyotaka? Enzi  za kina Kibakuli na Nyamayao sio mbali sana. Ila katika kipindi hiki kifupi tumepoteza mengi ya maana.

Tumepoteza maigizo yenye uhalisia, vipaji vya uhakika na hadithi za kibunifu zenye kutoa mafunzo na muongozo kwa jamii. Huwa nafurahi sana nikiikumbuka Kaole. Kaole iliyowatoa wakina Dr Cheni na Swebe.

Pia huwa naikumbuka Splendid ya kina Billy na Migomba. Ndiyo liyowatoa kina Mau, Dude na Chekibudi.

Japo hawa walifanya sanaa bila kuwa na wawekezaji na muitikio mkubwa ila waliacha alama muhimu za kukumbukwa? Wadau wa siku hizi wanashindwa wapi?

Kama una uwezo wa kwenda kukodi jumba na magari ya thamani kwa ajili ya kunogesha tamthiliya yako. Sasa unashindwa kupata unachotaka kwa kukosa wasaniii bora, kwa nini usisake vipaji halisi? Kwani kina Kipemba wako wapi?

Kina Christant Muhenga wako wapi kwa ajili ya ushauri. Kina Kasimu Twalibu (Ticha) wako wapi?

Kila mwenye uwezo apewe nafasi. Na kila mwenye ubunifu na aonyeshe katika kiwango halisi. Toeni nafasi kwa wenye vipaji halisi.

Sanaa haiwezi kukuwa kwa nyodo na mikogo. Hakuna sanaa itakayopanda kama kila siku sura na kujuana kunatangulia kabla ya weledi. Weka wasanii wa kweli sawa sawa na uwekezaji wa watu kwenye runinga na mitandao.


Jiongeze

Chillah hajapoteza sauti yake, anaimba vizuri, amekomaa kuliko wa Smooth Vibes kwa Ruge Mutahaba. Hivi sasa anateswa na mazingira. Mbona hafanikiwi?

Ni kweli muda aliupoteza katikati hapo, lakini mbona amejirekebisha na bado mafanikio hayaoni? Ukiuvaa uhusika wake utaelewa mateso haya ndani yake. Anawaona kina Diamond na wengine wanatengeneza pesa kwenye muziki, halafu anaumia kwa ndani.

Chillah anaona wote hao hawamuwezi kikazi. Hawamuwezi kwa muda alioutumia kuujenga muziki wa Kitanzania na thamani yake kwa jumla. Wote hao hakuna mwenye kuifikia gharama ya maumivu aliyopata.

Leo hii Chillah anaomba nafasi atambulishe ngoma mpya. Wakati hadhi yake ni kutafutwa na watangazaji waombe kumhoji. Hapo inabidi uwaweke na TID, Daz Nundaz, MB Dog ambao bado wanadai pesa nyingi kwenye muziki. Lakini wanapewa kisogo kama vile hawapo.