Prime
Usiyoyajua kuhusu Nanga kutoka hotelini hadi uchekeshaji
Muktasari:
- Akizungumza na Mwananchi mchekeshaji huyu ambaye ni baba wa mtoto mmoja amesimulia visa, mikasa na mafanikio ya tasnia yake
Dar es Salaam. Victor Happymaki Victor ndilo jina halisi la Nanga, mchekeshaji maarufu nchini anayesumbua kuanzia kwenye mitandao ya kijamii hadi tamthilia za kwenye televisheni kama ile ya Upepo inayoruka DSTV.
Akizungumza na Mwananchi mchekeshaji huyu ambaye ni baba wa mtoto mmoja amesimulia visa, mikasa na mafanikio ya tasnia yake.
Nanga mzaliwa wa Morogoro akiwa ni mtoto wa kwanza katika familia ya watoto wawili amesema safari yake kwenye sanaa ilianza tangu akiwa shule ya msingi.
“Nimesoma shule ya msingi Kigogo CCM, Sekondari nimesoma Mbopo A. Mimi sanaa nimeanza muda mrefu toka tunakua kwa sababu kaole kuna kipindi walikuwa wanafanya mazoezi pale TZF na nilikuwa nafanya nao japo tulikuwa hatujafanya kazi yoyote
“Kipindi hicho ilikuwa 2006 kama sio 2005 nilikuwa darasa la tano. Lakini rasmi kabisa kufanya ilikuwa ni kidato cha pili mwaka 2009. Nikiwa sekondari nikakutana na wenzangu kuna mtu anaitwa director Chuma na wengine tulivyokutana pale tukatengeneza kundi tukawa tunajiita ‘Serious Funny’. Lakini kabla ya hapo tulikuwa tunafanya mashairi tukajiita ‘Haladali’,”amesema Nanga.
Akizungumzia mashairi waliyokuwa wakiyafanya anayafananisha na yale yanayofanywa na ‘Mjomba’ Mrisho Mpoto
“Kuanzia form 2 hadi 4 tukafanikiwa ku-shoot tukapeleka kwenye Fema TV Show. Ila mtu ambaye alitupelekea akatuzunguka akaenda kuuza alafu akasema yamepotea tukakata tamaa. Baadaye tukasikia vitu vyetu vinaoneshwa Mbeya, Iringa kwenye mafunzo,”amesema.
Amesema baada ya kuzulumiwa ndipo wakaanzisha kundi la Serious Funny.
“Mwaka 2016 tukaanza kufanya picha za dk moja na ndiyo kundi la kwanza kufanya komedi za dk moja. Ndiyo yakazaliwa makundi mengine kama haya Timamu wakawa Mkali Wenu, Ebitoke , Jay Mondi, mpaka leo komedi imekuwa tasnia inaangaliwa,” amesema Nanga.
Mchekeshaji huyo ambaye kwa kabila ni Mluguru amesema safari yake ni tofauti na baadhi ya wasanii waliopata sapoti kutoka kwa wazazi wao.
“Mimi uzuri ama ubaya familia haikunizingatia. Baba ni mtu ambaye toka nazaliwa na kujitambua sio mfuatiliaji wa kitu chochote. Siyo chochote hata shule yeye anachojua huyu kaamuka amekula anaumwa basi. Ila mama kipindi ambacho nimemaliza shule akanipeleka kusoma ‘Hotel Management’.
“Nikawa nafaya kazi hotelini pale Mwenge. Nilikuwa nafaya kazi huku nashuti. Sasa familia zetu za Kiswahili haziamini katika sanaa. Kwahiyo wakawa wananihimiza nifanye kazi na hicho ninachofanya. Walijua hakitaniingizia chochote,”amesema
Nanga amesema kuna kipindi akawaza kuachana na kazi ili awekeze nguvu kwenye sanaa.
“Hapo mama alinuna akaona naenda kuchanganyikiwa ikabidi afuatilie kama navuta bangi mwisho nikamuelekeza. Nikamwambia lazima nifanye ninachofanya hapo nilikuwa nishaachana na ‘Serious Fanny’ kwa sababu tulikuwa tumefanya sana lakini hatujawahi kutengeneza hata buku.
“Ilikuwa nikifanya kazi ndiyo nibebe hela watu wapate kula na nauli ilikuwa kama inaumiza upande mmoja. Nikaenda kufanya kazi kwenye kampuni moja ya beti dakika za mwisho nikachoka nikaona ninachokipata chote nalipa madeni hapo ndipo nikamwambia mama sitafanya tena hii kazi acha nifanye mambo ambayo ninayoamini,”amesema
Baada ya kuacha kazi katika kampuni hiyo ya kubashiri Nanga amesema nafasi yake alimuweka mdogo wake katika kampuni hiyo.
“Ili nisimkwaze mama nikamchukua mdogo wangu nikamuweka pale kazini. Yeye akawa ameshika badala yangu na akawa anaendelea kulipwa. Nikaingia mkoani sasa kwa sababu Dar pakawa sipaelewi nikaenda Morogoro, nikawa nawatengenezea watu content mimi nalipwa.
“Ikawa ni biashara nzuri, wakawa wanalipa vizuri kwelikweli na ndio nikatengeneza timu ambayo unaiona pale tulivyotoka hapo tukaenda Mbeya na Tanga sasa Mbeya tukaja kuvurugana kwa sababu ya hela,”amesema Nanga.
Kama wasemavyo waswahili pesa mwanaharamu ndivyo ilimgombanisha Nanga na boss wake.
“Boss alikuwa mdogo kiumri lakini alikuwa mjanja wa mitandao alikuwa anajua namna gani YouTube tunaweza kupata hela. Mimi nikawa natengeneza kontenti nyingi tunaposti na hela zinaingia nyingi akawa ananilipa.
“Mwaka 2020 tulitakiwa tupate kama Sh75 milioni mimi nikawa namuongoza boss kama mdogo wangu, kuwa kila mtu anatakiwa kupata kiwanja. Kuinua kampuni mipango yangu haikumpendeza bwana mdogo tukapishana nikaona hatuwezi tena kufanya kazi kwa mfumo huo nikapewa pesa zangu nikaondoka nikarudi Dar kuanza moja,”amesema Nanga.
Licha ya wengi kumpenda kwa uchekeshaji wake lakini Nanga amesema yeye ni mtu asiyependa masihara yaliyopitiliza.
“Mimi ni mtu fulani serious, napenda masihara lakini sio yaliyopitiliza. Usiniletee komedi kwenye maisha yangu ya uhalisia. Misingi na heshima ifuatwe. Sipendi masihara ya hela na sipendi ukaribu wala masihara na mwanamke wangu.
“Hata ushemeji ni stori tu na hii sio wanaume tu hadi wanawake mimi mambo ya kutengeneza vilinge sipendi ndiyo mwanzo wa umbea. Sitaki watu kuchati na mwanamke wangu,”amesema kwa msisitizo
Yaliyomkuta kwenye mapenzi
“Mahusiano hayana tafsiri ambayo inafanana kila mtu ana pigo lake ambalo amewahi kukutana nalo” hii ni kauli ya Nanga akisimulia tamu na chungu ya mapenzi kwa upande wake.
“Niliwahi kuwa na mwenzangu tukaishi nae tukafunga ndoa tukabahatika kupata mtoto mmoja, baadaye mambo yakaenda ndivyo sivyo tukashindwana akaamua kuishi maisha yake na mimi nikaamua kuishi maisha yangu. Katikati nikakutana na mtu mwingine ambaye nikaona safari yetu tunaweza kuitengeneza vizuri lakini dakika za mwisho akaona sina future napenda kukaa na watu wengi wasio na msaada.
“Changamoto ya wanawake ambao nakutana nao hawaamini mapambano yangu. Wanaona nasaidia watu wengi sana ambao mimi nikiwa na changamoto sisaidiwi. Wanashindwa kuelewa wale watu ni sehemu ya mafanikio yangu, kwa sababu siwezi kushuti pekeyangu,”amesema.
Amesema mwanamke huyo wa pili naye wakaachana
“Mungu sio Bwana Kondo akatokea mdada ,huyo kabeba madhaifu yangu yote yupo mpaka sasahivi anakula starehe mahusianao yetu yana mwaka wa tatu. Mwaka hauishi naoa
Alivyoachiwa mtoto wa miezi kumi
Amesema yeye na aliyekuwa mkewe walibahatika kupata mtoto wa kiume aitwaye Alvin ambaye kwa sasa ana miaka tisa.
“Mwanangu yupo darasa la tatu anaishi kwa bibi yake nilikuwa naye tangu ana miezi kumi. Aliachwa akiwa na miezi hiyo mama yangu ndiye amemlea mpaka amefika miaka tisa. Ndoa yangu ilivunjika 2018 ilidumu kwa mwaka mmoja na tulikaa kwenye mahusiano miaka mitano ya uchumba.
“Mwanangu kama ana kipaji cha kufanya komedi namruhusu, lakini yule simuoni kuna muda anashinda na mipira kuna muda anacheza kama Mose Iyobo kwa hiyo haeleweki,”amesema Nanga
Komedi Kimataifa
“Kutoboa kimataifa siyo jambo rahisi sana. Lakini linawezekana kama serikali ikiamua kutia mkono wake. Hata marehemu The Great alipambana lakini hatukufika hiyo levo. Bado mtu kama Coy anapambana lakini hatuko hiyo Levo.
“Mpaka leo sisi ni watu wa kuwaita wenzetu waje kufanya lakini sisi ni mara chache kuitwa kwenda kufanya komedi nje inamaana bado watu hawajatuelewa. Ili tufanikiwa kwanza sanaa yetu iwe sekta rasmi ya kufahamika.
“Mfano hivi tunavyoongea hakuna ofisi ya Meta hapa Tanzania, hakuna ya TikTok wala Google kuna vitu vingi sisi hatuna leo hii ukitaka msaada na Instagram huwezi. Hakuna sehemu ya kusema matatizo na sisi tukitumia hivi vitu kama fursa watu watapiga hela na mambo yatakuwa makubwa.”amesema.
Amesema sasahivi serikali inasapoti lakini bado juhudi zinahitajika.
“Kama hivi imeandaa mikopo lakini bado kuna vile vitu vya msingi hawajaviweka mfano TikTok leo hii lazima umpigie mtu aliye Afrika Kusini au Kenya ndiyo akutolee hela wenzetu wana TikTok inayowalipa kwa kuposti sisi ni mpaka zawadi,”amesema
Anavyopamba na Changamoto
“Mimi mara nyingi nipo tofauti kutokana na makuzi na malezi kukata tamaa mwiko. Huwa naenda mbele nikiona hili jambo kama linanishinda namsukumia Mungu. Mimi sio mtu wa kukata tamaa jambokuwa changamoto zipo nyingi tasnia ya kinafiki wanaonesha nia kama wanataka kukusaidia lakini ukionesha nia wanakutupa.
“Lakini mtu kama Shafii alinitafuta tukafanya mpaka leo na yeye ni mchango mkubwa kuhakikisha narudi kwa nguvu zote japo kuna wengine nyuma,”amesema Nanga Licha ya hayo Nanga amesema starehe yae kubwa ni pombe lakini siyo mlevi wa kuanguka kwenye mitaro.
“Nikikaa nakula mtungi nakuwa na furaha na siyo ya kumletea mtu kero nakunywa nyumbani kwangu. au na marafiki lakini bila shida ndiyo maana kuna watu ukiwaambia Nanga anakunywa sana pombe watakataa,”amesema Nanga
Kuonekana kwenye tamthilia
Nanga ni kati ya waigizaji wanaoonekana kwenye tamthilia ya upepo inayoruka DSTV anasimilia alivyopata mchongo. “Ishu ya kuigiza kwenye tamthilia ya Upepo ni Director Majagi amekuwa brother anaweza kunipigia simu kwa matukio yote. Amekuwa sehemu ya familia tangu nipo Morogoro.