Utamu wa muziki wa asili katika dansi

Muktasari:

  • Kurekodi katika mahadhi na lugha za asili za Tanzania, ilikuwa ni jambo la kawaida sana toka kuanzishwa kwa mfumo wa kupiga bendi. Maelfu ya nyimbo za aina hiyo lazima zimerekodiwa katika miaka takribani mia moja ya historia ya muziki wa bendi.

Mwaka 1986 bendi mpya iliyoitwa Tancut Almasi Orchestra iliingia katika studio za Radio Tanzania Dar es Salaam na kati ya nyimbo ilizorekodi ulikuweko wimbo wenye maneno haya,

Kweiyendyu mwana mtaulage, mtaulage mwana, mtaulage, ulikuwa utunzi wa Francis Kitime, baba yangu, mimi nikauchukua na kutengeneza kwenye mapigo ya bendi. 

Wimbo huu haukuwa wa kwanza kwangu kurekodi wimbo kwa lugha ya Kihehe kwani kulikuweko na nyimbo kadhaa ambazo tayari nilikuwa nimerekodi katika studio za Tanzania Film Company (TFC) kwenye mwaka 1981. 

Kurekodi katika mahadhi na lugha za asili za Tanzania, ilikuwa ni jambo la kawaida sana toka kuanzishwa kwa mfumo wa kupiga bendi. Maelfu ya nyimbo za aina hiyo lazima zimerekodiwa katika miaka takribani mia moja ya historia ya muziki wa bendi.

Hebu tujikumbushe baadhi ya bendi na nyimbo zilizopigwa katika mahadhi yaliyotokana na ngoma asili za hapa kwetu au kuimbwa kwa lugha za asili.

Nianze na bendi kongwe ya  Kiko Kids iliyokuwa na maskani katika mji wa Tabora, bendi ambayo kuna ushahidi wa picha kuwa ilikuwa tayari ikifanya maonesho mwaka 1955.  

Bendi hii wakati ikiwa  chini ya uongozi wa marehemu Salum Zahoro, ilirekodi nyimbo nyingi za lugha mbalimbali kama vile Nda Kuharashe iliyoimbwa Kitusi, Tula Ubona iliyoimbwa kwa lugha ya kabila dogo lililoitwa Wanyandani toka Nyanda za Juu Kusini, Nke Kubalile na nyingine nyingi ambazo zilimbwa kwa lugha ya Kinyamwezi. 

Bendi nyingine kongwe ambayo ilianza kupiga muziki mwaka 1944 huko Morogoro, na kuchukua jina la mji na kuitwa Morogoro Jazz Band ilikuwa na nyimbo nyingi za Kilugulu ikiwemo Bondwa, Mzese na Mzese, Bambalawe na nyingine nyingi. 

Hata zama hizo kuna simulizi kuwa kulikuwa na mvutano kuhusu kuimba Kilugulu, baadhi ya wanamuziki waliona hilo litaishusha hadhi bendi yao, lakini baada ya kuanza kuziimba nyimbo ukumbini, zikawa kati ya nyimbo pendwa za bendi hiyo hali ambayo inaendelea mpaka leo licha ya kwamba bendi hiyo ilikwisha kupotea miaka mingi.

Pamoja na kurekodi wimbo wa Mtaulage ambao nimeutaja hapo awali, Tancut Almasi Orchestra,  pia ilirekodi wimbo ulioitwa Wifi, wimbo ambao asili yake ni Kibena, vumbi lilikuwa ikitimka wimbo huo ulipokuwa ukipigwa, ni miaka zaidi ya thelathini na tano toka nyimbo hizi ziliporekodiwa, lakini bado husikika katika sherehe mbalimbali mpaka leo.

Mji wa Lindi ulikuwa na bendi iliyopata umaarufu mkubwa kutokana na wimbo wake wa Kimakonde ulioitwa Mariana, bendi hiyo iliitwa Mitonga Jazz Band. Wimbo wao huohuu haukurekodiwa ndani ya studio bali nje kwenye ukumbi, lakini utamu wa muziki huu uliwashika watu wote hata wale ambao hawakuwa wanajua Lugha ya Kimakonde.

Wimbo mwingine wa Kimakonde uliokuja kushika hisia za wapenzi wa dansi ulikuwa ni utunzi wa mrehemu Halila Tongolanga, ambao aliurekodi na bendi ya Jeshi la Wananchi iliyoitwa Les Mwenge ambayo makazi yake yalikuwa Monduli Arusha , wimbo huu uliitwa Kila munu ave na kwao, yaani kila mtu ana kwao, pamoja na kuwa wimbo huo umerekodiwa miaka mingi iliyopita, na pia Tongolanga alikwisha fariki miaka mingi, wimbo bado unaleta hisia kwa wanaojua Kimakonde na hata wale wasioijua lugha hiyo.

Jiji la Dar es Salaam kwa kuwa ndiko kulikuwa na mkusanyiko wa watu kutoka mikoa mbalimbali, bendi za jiji hili zilikuwa na tungo kutoka karibu kila kabila. 

Eddy Sheggy katika bendi alizopitia aliweza kutoa nyimbo kadhaa za Kisambaa zilizopendwa sana, na hata  yeye jina lake la utani likawa ni jina la wimbo wake maarufu wa Shakaza. 

Patrick Balisdya akiwa na bendi yake ya Afro 70 akatupatia wimbo wa Kigogo wa Mavula. Kilimanjaro Band katika album yao waliyoitoa mwaka 2004, walikuwa na wimbo ulioitwa Boko, ambao ulikuwa wa Kidigo, Tummogele wa Kinyakyusa, Maige wa Kisukuma, Jitu wa Kihehe.

Bendi zilizokuwa za asili ya Kongo ambazo ziliweka makazi yao Tanzania nazo hazikuwa nyuma kwenye kutengeneza nyimbo za makabila ya Tanzania. 

Bendi hizi baada ya kuingia nchini awali, zilikuwa zikitunga nyimbo zake kwa kilingala tu, lakini tangazo la Wizara ya Utamaduni likaelekeza kuwa lazima asilimia kubwa zaidi ya tungo zake ziwe ni za Kiswahili, bendi hizi zikafanya zaidi ya hapo na kuanza hata kuimba kwa lugha za asili za Tanzania, Orchestra Safari Sound walikuja na wimbo wao wa Kinyakyusa ulioitwa Mwaipungu, Orchestra Makassy now walikuwa na wimbo ulioitwa Asumani ambao nao ulikuwa na kibwagizo cha Kinyakyusa.

Marquis Original nao hawakuwa nyuma wakashusha tungo ya Kibondei iliyoitwa Mangolibo. Bendi ya Toma Toma iliyokuwa mali ya Timmy Thomas ilikuwa na wimbo wa Kinyamwezi ulioitwa Kesachane.

Akiwa na baadhi ya waimbaji wakiwa ni kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, mkongwe Shem Karenga akisindikizwa na  bendi ya MK Group alirekodi wimbo mtamu kabisa ulioitwa Bela ombwe, pia Mzee Shem Karenga wakati akiwa na MK Beat. Alirekodi wimbo ulioitwa Yuva Vangu ambao ulikuwa wa Kihehe.

Katika kuonyesha umuhimu wa nyimbo zenye mahadhi ya asili ya Tanzania,  mwaka 1988 na mwaka 1989 kulikuwa na mashindano ya Kitaifa ya bendi nchini yaliyoitwa Top Ten Show, mojawapo ya sharti ilikuwa kuwa na wimbo mmoja ambao una mapigo ya ngoma yoyote ya asili ya Tanzania.

Jambo hili lilionyesha pia nia iliyokuwepo ya kushawishi bendi kuendelea kutunga nyimbo za aina hiyo ili kuongeza utambulisho wa muziki wa Tanzania. Katika shindano hilo wimbo ambao nilishiriki nikiwa Tancut Almasi Orchestra, ulioitwa Lung’ulye, uliweza kushinda kama wimbo bora wa asili katika mashindano yale.