Vaa hadi wakushangae; Mtoko wa usiku Met Gala ulivyobamba

Muktasari:

  • Tamasha la mitindo la Met Gala kwa mwaka 2024 lilifanyika kwenye Ukumbi wa Makumbusho ya Sanaa ya Metropolitan huko New York, ambako yamekuwa yakifanyika kila mwaka.

New York, Marekani,  Rapa Cardi B aliweka kando ugumu na kutupia kiwalo matata kabisa kwenye usiku wa tamasha la mitindo la Met Gala, akijaribu kuwafunika watu wengine maarufu kwa mtindo wake wa mavazi.

Rapa huyo aliyetupia gauni jeusi kubwaaa aliendana na kauli mbiu ya onyesho hilo la mitindo la mwaka huu inayosema, Sleeping Beauties: Reawakening Fashion.

Tamasha la mitindo la Met Gala kwa mwaka 2024 lilifanyika kwenye Ukumbi wa Makumbusho ya Sanaa ya Metropolitan huko New York, ambako yamekuwa yakifanyika kila mwaka.

Kundi la wasanii maarufu na mashuhuri wanaofanya vyema kwenye mitindo na biashara nyingine za burudani waliungana na mhariri mkuu wa jarida la Vogue, Anna Wintour kwenye tamasha hilo matata kabisa lililofanyika usiku wa Jumatatu.

Dizaini ya mitindo ya mavazi ya mwaka huu yalihusisha vitambaa vya maua na vya rangi tofauti na hakika mastaa hawakufanya mzaha kwa namna walivyotumia. Wasanii kibao walihudhuria akiwamo Jennifer Lopez.

Cheki hapa mastaa walihudhuria tamasha hilo na namna walivyofunikana kwa mitupio.


Cardi B 

Rapa Cardi B aliwaduwaza mashabiki wake kutokana na ukubwa wa gauni lake alilotupia, ambalo nusura lifunike ngazi zote za kuingilia kwenye ukumbi wa Met Gala. Gauni hilo lilikuwa na manyoya meusi na kunakshiwa na vipuri vilivyomfanya kuwa kwenye mvuto wa kipekee.

                        


Kim Kardashian na Kylie Jenner 

Mrembo Kylie Jenner aliwasili kwenye tamasha hilo la Met Gala akiwa amevaa gauni la rangi ya maziwa. Mrembo huyo matata kwa vipodozi, alivaa kwa ajili ya kuvutia watu, ambapo aligongelezea skinitaiti iliyoishia kwenye enka, ikiwa saresare na viatu vyake. Kylie, hakuwa yeye wa kutoka familia ya Kardashian, bali dada zake, Kim, 43, na Kendall, 28, nao walihudhuria. Mama yao, Kris Jenner, 68, aligongelea kivazi cheupe.

                       


Rita Ora 

Rita Ora, 33, alivaa kivazi ambacho kilifanya mwili wake kuonekana waziwazi. Nakshi za maua maua ziikuwa za rangi nyeusi, pinki na machungwa pamoja na nyeupe kumfanya kuwa kwenye mwonekano wa kipekee kabisa. Mwimbaji huyo wa wimbo wa Praising You, mavazi yake ni ya mtindo wa kizamani.

                         


Lana Del Rey 

Mrembo Lana Del Rey alishtua kutokana na mtindo wake wa mavazi aliotinga nao kwenye tamasha hilo. Mwimbaji huyo wa wimbo wa The Off To The Races, mwenye umri wa miaka 38, alitinga kivazi kilichobana mwili wake, lakini huku kichwani akijifunika na kitu kinachofanana na chandarua.

                     


Demi Moore

Mwigizaji Demi Moore, 61, hakupitwa na umri, naye aliibuka na kuonyesha mbwembwe zake katika kutupia viwalo. Mrembo hiyo alionekana kuwa mwenye furaha muda wote wakati alipokuwa akiweka mapozi kwa ajili ya kupiga picha akiwa kwenye gauni la rangi nyeusi pamoja lililoshonewa na ua moja kubwa lenye rangi ya pinki na nyeupe.

                      


Jessica Biel 

Mwigizaji Jessica Biel alionekana ni mwenye kupendeza kwenye kigauni cha pinki. Mke huyo wa mwimbaji wa pop, Justin Timberlake aliwaduwaza mashabiki wake kwa mtindo wake wa mavazi, alipotinga na kivazi kilichokuwa na manyoya kuendana na usiku wenyewe unavyohitaji.

                       


Gabrielle Union na Dwayne Wade 

Mke na mume, Gabrielle Union na Dwayne Wade nao hawakutaka kujipunja na kuibukia kwenye tamasha hilo la mitindo wakiwa kwenye mavazi matata kabisa. Mkali wa mpira wa kikapu kwenye ligi ya NBA, Wade, alipigilia suti fulani ya kibabe na fulana yenye mkato wa V shingoni. Wakati huo, mrembo Gabrielle alipigilia gauni la staili ya nguv...a.

                        


Watu wengine maarufu 

Tamasha la Met Gala 2024 lilivutia watu wengi maarufu akiwamo mwanamitindo, Zendaya ambaye alionyesha mtindo wake moto kabisa, sambamba na Doja Cat, huku wengine waliohudhuria ni Gigi Hadid, Nicole Kidman, JLO, Elle Fanning, Bad Bunny, Sarah Jessica Parker, Andy Cohen, Chris Hemsworth, Ashley Graham, Ayo Edebiri, Josh O’Conor na Mike Faist.