Wanamitandao waliochumbiana juu ya jengo refu wadakwa
Muktasari:
- Wawili hao walipanda kwenye sehemu ya juu ya jengo hilo bila kutumia vifaa vya usalama. Jambo lililosababisha taharuki na kuwalazimu maafisa wa usalama kuendesha operesheni ya kuwashusha salama
Marekani. Waandaaji maudhui na wapenzi maarufu, Angela Nikolau na Ivan Beerkus, wamekamatwa jijini New York City baada ya kupanda juu ya jengo refu Empire State Building bila kibali na kuvishana pete.
Wawili hao walipanda kwenye sehemu ya juu ya jengo hilo bila kutumia vifaa vya usalama. Jambo lililosababisha taharuki na kuwalazimu maafisa wa usalama kuendesha operesheni ya kuwashusha salama.
Baada ya kushushwa, walikamatwa na kupelekwa kituo cha polisi kwa mahojiano na hatua zaidi za kisheria.
Angela Nikolau, ni raia wa Urusi, alianza kujulikana mwanzoni mwa miaka ya 2010 baada ya kupiga picha na video akiwa juu ya majengo marefu bila kutumia vifaa vya usalama.
Alianza kufanya hivyo akiwa na umri mdogo, akivutiwa na upigaji picha wa maeneo ya juu na maisha ya kutafuta matukio ya kipekee.
Kwa upande wa Ivan Beerkus, ambaye pia anatokea Urusi, alianza kupanda majengo na cranes kupitia kundi la wapenda mchezo unaojulikana kama rooftopping. Baadaye alikutana na Angela, na tangu hapo wakaanza safari pamoja wakirekodi matukio yao na kuyachapisha kwenye mitandao ya kijamii.
Katika kipindi cha zaidi ya muongo mmoja, wawili hao wamewahi kupanda majengo maarufu duniani kama Shanghai Tower, Merdeka 118, Princess Tower pamoja na cranes na majengo mengine marefu katika nchi mbalimbali.
Picha na video zao zimewavutia mamilioni ya watu, lakini pia zimekuwa zikikosolewa kwa kuhamasisha vitendo hatarishi.
Umaarufu wao uliongezeka zaidi baada ya kushiriki kwenye filamu ya Skywalkers: A Love Story, inayosimulia maisha yao, safari zao za kupanda majengo marefu na uhusiano wao wa kimapenzi. Tukio la kukamatwa kwao New York limeibua mjadala kuhusu mipaka ya kutafuta umaarufu mtandaoni na umuhimu wa kuzingatia sheria na usalama.