Wimbo 'We are the world' ulitakiwa kuimbwa Kiswahili

Muktasari:

  • Jambo hilo limewekwa wazi kupitia filamu ya 'The Greatest Night in Pop' ambayo inapatikana Netflix. Filamu hiyo ina saa moja na dakika thelathini na saba, ilikutanisha takribani wasanii 47 wa miondoko ya muziki wa pop.

Marekani. Katika hali ya kushangaza fahamu kuwa wimbo uliotoka zamani 'We Are the World', uliotungwa na Mfalme wa Pop Michael Jackson na Lionel Richie mwaka 1985, ulikusudiwa kutumia baadhi ya maneno ya Kiswahili.

Jambo hilo limewekwa wazi kupitia filamu ya 'The Greatest Night in Pop' ambayo inapatikana Netflix. Filamu hiyo ina saa moja na dakika thelathini na saba, ilikutanisha takribani wasanii 47 wa miondoko ya muziki wa pop.

Filamu hiyo inaelezea namna ambavyo wimbo huo 'We Are the World' ulivyokuwa ukitengenezwa kabla ya kutoka rasmi kwa wasikilizaji, ambapo katika dakika ya 45, filamu hiyo inamuonesha nguli wa muziki huo Stevie Wonder, akitamka maneno ya kiswahili kwenye wimbo huo yaliyowaacha watu na maswali, kutokana na kutoelewa lugha aliyozungumza. Alisikika akisema "Ulimwengu wa Latoto" akitaka kumaanisha "Sisi ni Ulimwengu".

Wakati filamu hiyo ikiendelea msimuliaji ambaye naye pia ni mmoja wa washiriki katika kuandaa wimbo huo Lionel Richie, anasimulia namna ambavyo Stevie Wonder alitaka kuweka kitu cha tofauti ndani ya wimbo huo, akisema "Stevie alisema, nadhani tunahitaji kuwa na Kiswahili mahali fulani kwenye wimbo."

Hata hivyo, baada ya Steve kuingiza lugha ya Kiswahili, ilisababisha kusitishwa kurekodiwa kwa wimbo huo kwa muda fulani, kutokana na jambo hilo kupelekea baadhi ya wasanii kama Waylon Jennings kuondoka studio akikataa kuimba kwa Kiswahili.

Jambo hilo lilizua wasiwasi miongoni mwa wasanii hao, huku baadhi yao wakihofia kwamba utumiaji wa Lugha ya Kiswahili unaweza kurefusha jambo hilo lisiishe mapema.

Licha ya mchango wa Stevie kukataliwa kutumia lugha ya Kiswahili, lakini amekuwa ni kati walioshiriki kwa nafasi kubwa kwenye wimbo huo.