Zanzibar yatenga Sh15 bilioni kujenga kijiji cha utamaduni
Muktasari:
- Mradi huo unatarajiwa kuonesha sanaa za jadi za Zanzibar, muziki, usanifu wa majengo, mila na desturi mbalimbali. Huku ukiimarisha utalii wa kiutamaduni na kutoa nafasi ya kukuza sekta ya ubunifu
Zanzibar. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetenga Sh15 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa kijiji cha utamaduni, kikilenga kuhifadhi na kuendeleza urithi tajiri wa kitamaduni wa visiwa hivyo.
Mradi huo unatarajiwa kuonesha sanaa za jadi za Zanzibar, muziki, usanifu wa majengo, mila na desturi mbalimbali. Huku ukiimarisha utalii wa kiutamaduni na kutoa nafasi ya kukuza sekta ya ubunifu.
Akizungumza wakati wa usiku wa tuzo, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Dk Riziki Pembe Juma, alisema uwekezaji huo unaonesha dhamira ya serikali katika kuendeleza uchumi wa utamaduni na kuongeza fursa kwa wasanii, waigizaji na wadau wa sekta ya sanaa visiwani humo.
“Nililazimika kuthibitisha hili ili muone mwanga juu ya changamoto za maeneo ya shughuli zetu za kiutamaduni,” alisema.
Kijiji hicho cha utamaduni pia kitatumika kama eneo la burudani na matukio ya kitamaduni. Kikitoa nafasi maalum kwa maonesho, tamasha na mikusanyiko ya kijamii.
Mpango huo ni sehemu ya juhudi pana za kukabiliana na changamoto za muda mrefu katika sekta ya utamaduni, ikiwemo upatikanaji wa maeneo na miundombinu bora ya shughuli za sanaa.
Dk Juma alisisitiza pia umuhimu wa kuwepo kwa mifumo endelevu ya kuwawezesha wasanii hata baada ya matukio makubwa kama Tamasha la Filamu la Zanzibar (ZIFF). Akisema vijana wa filamu, waandishi wa skripti na wakurugenzi wanahitaji msaada endelevu.
“ZIFF ni kubwa na maarufu sana. Lakini hawa vijana wasanii, waandishi wa skripti na wakurugenzi wa filamu wanahitaji msaada wa ZIFF zaidi ya siku za tamasha. Mnafanya nini ndani ya siku hizo tano ni muhimu. Lakini baada ya hapo je? Kuna nini baada ya ZIFF?”
Kauli yake ilisisitiza umuhimu wa kuimarisha majukwaa ya sanaa yanayoendelea mwaka mzima ili kuhakikisha matamasha yanakuwa chachu ya maendeleo ya muda mrefu katika sekta ya ubunifu Zanzibar.