Mazao kutohifadhiwa vizuri kunavyoathiri lishe, uchumi

Thursday October 22 2020
uchumi pic

Miongoni mwa malengo ya Umoja wa Afrika ni kuondoa njaa na usalama wa chakula na lishe kwa wananchi wake. Hata hivyo, uwezekano wa kuhakikisha usalama wa chakula na lishe una changamoto zake.

Taarifa ya hali ya uzalishaji wa chakula kwa kuzingatia kigezo cha upimaji wa kiwango cha utoshelevu inaonyesha kuwa kwa mwaka wa chakula 2019/20 Tanzania itakuwa na kiwango cha utoshelevu cha asilimia 119.

Hata hivyo, baadhi ya mikoa huathirika kwa uhaba wa chakula kutokana na mifumo hafifu ya kuhifadhi mazao baada ya kuvuna, hali inayosababisha upungufu wa mazao na kupanda kwa bei.

Hali hiyo inatokana na upotevu wa mazao ya nafaka baada ya kuvuna unaokadiriwa kuwa kati ya asilimia 30 na 40.

Inakadiriwa kuwa zaidi ya tani 1.3 bilioni za chakula imekuwa ikipotea duniani kote kwa mwaka baada ya kuvunwa na kusababisha hasara ya zaidi ya Dola 750 bilioni za Marekani.

Mbali na kupotea, uhifadhi hafifu wa chakula huzalisha sumu zinazosababisha magonjwa.

Advertisement

Hivi karibuni, wadau wa kilimo wamekutana Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (Sua) kujadili njia ya kupambana na upotevu wa chakula nchini.

Akizungumza hivi karibuni katika kongamano hilo lililoandaliwa na Jukwaa la Kilimo (Ansaf), Helvetas na Serikiali, mtaalamu wa usalama wa chakula, Benny Rushunju anasema endapo chakula hakitahifadhiwa vizuri kuna hatari ya kuzalisha sumu hatari kwa maisha ya binadamu na wanyama.

Anataja baadhi ya sumu zinazozalishwa kutokana na uhifadhi hafifu wa chakula kuwa sumu kuvu ikiwamo ya Aflatoxin.

Nyingine ni Fumonisins, Ochratoxin, T-2 Toxin, HT-2 Toxin, Patulins, Zearalenone na Deoxynivalenol.

“Aflatoxin ni sumu zinazojitokeza kiasili na husambaa kwenye vyakula. Ni ukungu aina ya Aspergillus unaozalisha sumu aina ya aflatoxinsare,” anasema Rushunju.

Mazao yanayotajwa kukumbwa zaidi na sumu hizo ni mahindi, karanga, mpunga, mbegu za mafuta, pilipili, matunda yanayokaushwa na maziwa.

Anasema sumu hizo zikitumiwa na binadamu na wanyama hubaki kwenye nyama na mazao yake kama maziwa na mkojo.

Rushunju anaendelea kusema licha ya kuwa na athari, wataalamu hawazitilii maanani hadi zinapoathiri watu wengi kwa wakati mmoja.

Mbali na magonjwa, sumu hizo zina athari ya kiuchumi na kimazingira. “Mwaka 2014 watu 317 waliugua; 125 kati yao walifariki dunia Kenya, mwaka 2016 watu 68 waliugua na kati yao 20 walifariki dunia Tanzania na mwaka 2019 Watanzania walikutwa na ugonjwa huo na wanane kati yao wamefariki dunia,” anasema Rushunju.

Anataja athari nyingine kuwa ni udumavu na utapiamlo kwa watoto walio chini ya miaka mitano na unapunguza kinga za mwili, kuharibu afya ya uzazi.

“Pia, sumu hizo zinasababisha ugonjwa wa saratani ya ini na koo. Inakadiriwa kuwa zaidi ya wagonjwa 3,000 wa saratani ya ini wa Tanzania mwaka 2016 walitokana na sumu hizi,” anasema.

Kuhusu afya ya wanyama, anasema sumu hizo hupunguza kinga na ukuaji wa wanyama, huku pia kukiwa na usugu wa chanjo hasa kwa magonjwa kama mdondo kwa kuku.

Mbali na kuongeza gharama za matunzo ya wanyama, pia sumu hizo hupunguza uzalishaji na hivyo kukosesgha mfugaji mapato na nguvu kazi.

Ili kukabiliana na sumu hizi, Rushunju anashauri mbinu ikiwa pamoja na kutumia vyakula vinavyopunguza simu mwilini kama mboga ya mnafu, bamia na maparachichi.

Pia kuna vyakula vyenye madini ya zinki kwa wingi kama mazao ya mikundekunde, mbegu za matunda, nyama nyekundu, mbegu za mafuta kama korosho na karanga, chokoleti nyeusi na mayai, alizeti na samaki pia hupunguza sumu na kukarabati seli zilizoathirika.

Pia, anashauri kula matunda yenye vitamini C kama machungwa, mapera na mboga za majani ili kuongeza kinga ya mwili.

Njia za kuhifadhi mazao

Akizungumzia kuhusu utafiti wa uhifadhi wa chakula uliofanywa mwaka 2018, mtaalamu wa kilimo, Aneth Kayombo anashauri matumizi ya mifuko isiyopitisha unyevu hermetic storage bags (HSBs), kuhifadhia mazao ya nafaka.

“Utafiti umeonyesha kuwa asilimia 42 ya wakulima hutumia mifuko isiyoingiza unyevu kama njia kuu ya kuhifadhi chakula. Kuna wazalishaji wakuu watatu ambao huzalisha mifuko 666,667 kwa mwaka kwa soko la ndani,” anasema Kayombo.

“Kwa kutumia mifuko ya kuhifadhia chakula, mkulima anapunguza upotevu wa chakula kwa asilimia 2.8 zaidi kuliko asiyetumia. Mkulima ataokoa Sh26,000 kwa msimu na hakutakuwa na gharama za viuatilifu ambavyo huongeza gharama ya Sh5,980 kwa kila tani.”

Anasema kama mazao yatahifadhiwa kwenye mifuko kama hiyo kuna uwezekano wa kuuza chakula kwa bei ya juu wakati kikiwa kimepungua sokoni.

“Matumizi ya mifuko isiyopitisha unyevu inaweza kupunguza upotevu wa mazao kwa asilimia 67 na kumwezesha mkulima kuokoa Sh25,760 kwa kila tani kwa msimu,” anasema Kayombo.

“Itamwezesha mkulima kupata mapato ya Sh32,062 kwa gunia kwa gharama ya Sh19,159 na hivyo kupata faifa ya Sh12,903 kwa gunia.

Ili kuwawezesha wakulima kutumia mifuko hiyo, Serikali imeshauriwa kuondoa kodi ya ongezeko la thamani kwa wazalishaji.

“Utafiti unaunga mkono kuondolewa kwa kodi ya ongezeko la thamani (asilimia 18) kwa wazalishaji wa mifuko hiyo, kwa sababu kuondolewa kwa kodi hiyo kutaleta manufaa kwa wakulima na uchumi wa nchi maradufu,” anasema Kayombo.

Hali ya upotevu wa mazao baada ya kuvuna nchini imeifanya Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kuandaa mkakati wa Taifa wa usimamizi mazao baada ya kuvuna.

Mkakati huu utatekelezwa kwa kipindi cha miaka kumi na utahusisha mazao ya aina mbalimbali yakiwamo ya nafaka, jamii ya mikunde, matunda, mboga, mizizi pamoja na mazao ya mbegu za mafuta.

Advertisement