‘Wadau leteni bidhaa soko la mitaji na dhamana’
Muktasari:
- Wakati thamani kwenye masoko ya mitaji ikipaa hadi kufikia Sh37.3 trilioni katika kipindi kilichoishia Januari 2024, Serikali imewataka wadau wa sekta hiyo kupeleka bidhaa endelevu za masoko ya mitaji ili kupata rasilimali fedha na kuchochea maendeleo.
Dar es Salaam. Wakati thamani kwenye masoko ya mitaji ikipaa hadi kufikia Sh37.3 trilioni, katika kipindi kilichoishia Januari 2024, Serikali imewataka wadau wa sekta hiyo kupeleka bidhaa endelevu za masoko ya mitaji zitakazowezesha kupata rasilimali fedha na kuchochea maendeleo endelevu.
Hayo yamebainishwa leo Februari 28, 2024 jijini Dar es Salaam kwenye ufunguzi wa mkutano wa siku tatu unaohusu maendeleo ya masoko ya mitaji katika Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
Mkutano huo unaoratibiwa na Taasisi ya Uendelezaji wa Sekta za Fedha Barani Afrika, (FSDA), kwa kushirikiana na Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana, (CMSA) na Kamati ya Masoko ya Hisa ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika, (COSSE) umehudhuriwa na wadau kutoka mataifa mbalimbali.
Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema Serikali kupitia CMSA imekuwa ikitekeleza mikakati ya kuanzisha bidhaa bunifu na endelevu za masoko ya mitaji ambazo zimewezesha kuongezeka kwa thamani ya uwekezaji wa masoko ya mitaji na mauzo kwenye soko la hisa.
Ametaja baadhi ya mafanikio yaliyopatikana katika kuanzisha bidhaa bunifu na endelevu ni pamoja na utoaji wa hatifungani ya kwanza ya Kijani Bond yenye thamani iliyowezesha kupata Sh171.8 bilioni ambapo fedha zilizopatikana zinatumika kutekeleza miradi ya kutunza na kuhifadhi mazingira.
“Pia utoaji wa hatifungani ya Jasiri Bond imeweza kupata Sh74.2 bilioni na fedha hizo zinatumika kuendeleza biashara ndogo na za kati zinazomilikiwa na kuendeshwa na wanawake na zile zinazomilikiwa na wanaume,” amesema.
Pia ameitaja Social Bond imewezesha kupata Sh212.9 bilioni ambazo zinatumika kutekeleza miradi ya maendeleo na biashara endelevu kwa jamii.
“Natoa rai kwa washiriki wote kutumia fursa ya mkutano huu kuongeza ujuzi na kupata uzoefu zaidi wa namna ya kutekeleza mikakati inayochagiza maendeleo endelevu ya masoko ya mitaji katika ukanda wa SADC, ili kuyawezesha masoko haya kuwa na thamani zaidi,” amesema Profesa Mkenda.
Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji Mkuu wa CMSA, Nicodemus Mkama amesema wanawavutia wawekezaji wa kitaifa na kimataifa kuwekeza nchini, ili kupata fedha za kigeni zinazochochea maendeleo ya kiuchumi.
“Tunaitangaza nchi yetu kwenye ramani ya ulimwengu kupitia utoaji bidhaa bunifu kwenye masoko ya mitaji na vilevile itawavutia wawekezaji hao,” amesema Mkama.