Absa, wadau wajadili mwelekeo wa uchumi, masoko ya fedha nchini
Mtaalamu mwandamizi wa masuala ya biashara kutoka Absa Group, Kabelo Bogopa akizungumza na baadhi ya washiriki kutoka taasisi kubwa za uwekezaji katika warsha iliyozungumzia mwelekeo wa uchumi wa ndani na nchi nyingine mbalimbali duniani, iliyofanyika jijini Dar es Salaam.
Muktasari:
- Licha ya changamoto zinazoendelea kujitokeza katika uchumi wa ndani na wa kimataifa, bado zipo fursa kwa wawekezaji watakaokuwa na taarifa sahihi na mikakati madhubuti ya usimamizi wa hatari.
Dar es Salaam. Benki Benki ya Absa Tanzania imewakutanisha wawekezaji wa taasisi na wadau mbalimbali wa sekta ya fedha nchini katika semina iliyojadili mwelekeo wa uchumi wa Tanzania, pamoja na mwenendo wa masoko ya fedha ya kikanda na kimataifa.
Semina hiyo imelenga kutoa jukwaa la wadau kujadili masuala muhimu ya uchumi, kubadilishana uzoefu na kupata maarifa kuhusu mazingira ya sasa ya uwekezaji na fursa zinazopatikana nchini.
Akizungumza katika semina hiyo iliyofanyika jana, Jumatano, Juni 17, 2026, jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Masoko ya Fedha za Kigeni wa Benki ya Absa Tanzania, Irene Rwegalulira, amesema kuwa katika mazingira ya sasa ya masoko, mafanikio yanategemea zaidi utayari na mikakati sahihi kuliko uwezo wa kutabiri mabadiliko yote yanayotokea.
“Mafanikio katika mazingira ya sasa hayategemei uwezo wa kutabiri kila mabadiliko ya soko. Kinachohitajika ni kuwa tayari, kulindwa na kuwa katika nafasi nzuri wakati mabadiliko yanapotokea,” amesema mkurugenzi huyo.
Amesema licha ya changamoto zinazoendelea kujitokeza katika uchumi wa ndani na wa kimataifa, bado zipo fursa kwa wawekezaji watakaokuwa na taarifa sahihi na mikakati madhubuti ya usimamizi wa hatari.
Rwegalulira amesema Absa itaendelea kuwawezesha wateja wake wa taasisi kupitia utaalamu wa masoko, suluhisho bunifu za kifedha na ushauri wa kimkakati ili kuwawezesha kufanya uamuzi sahihi wa uwekezaji.
“Jukumu letu kama mshirika wenu katika masoko ya kimataifa ni kuwasaidia kukabiliana na hali ya kutokuwa na uhakika, kusimamia hatari kwa ufanisi na kutumia fursa zilizopo kwa kujiamini na kwa usahihi,” amesema.
Mtaalamu mwandamizi wa masuala ya biashara kutoka Absa Group, Kabelo Bogopa akizungumza na baadhi ya washiriki kutoka taasisi kubwa za uwekezaji katika warsha iliyozungumzia mwelekeo wa uchumi wa ndani na nchi nyingine mbalimbali duniani, iliyofanyika jijini Dar es Salaam.
Aidha, Rwegalulira amezipongeza taasisi za udhibiti, zikiwamo Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (Tira) na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kwa mchango wao katika kujenga imani ya washiriki wa soko na kuimarisha ukuaji endelevu wa sekta ya fedha.
Semina hiyo iliyowashirikisha wataalamu wa Absa kutoka masoko mbalimbali barani Afrika, imewapa washiriki fursa ya kujadili mwenendo wa uchumi mpana unaoathiri Tanzania na dunia, mikakati ya kudhibiti hatari zinazotokana na mabadiliko ya viwango vya ubadilishaji wa fedha za kigeni na viwango vya riba, pamoja na suluhisho za uwekezaji zinazolenga kuongeza tija huku zikizingatia kiwango cha hatari kinachokubalika kwa taasisi husika.
Kwa mujibu wa Absa, semina hiyo ni sehemu ya mkakati wa benki hiyo wa kuwawezesha wawekezaji kwa kuwapatia taarifa na uchambuzi wa masoko unaoweza kutumika moja kwa moja katika kufanya maamuzi ya uwekezaji, pamoja na kuimarisha ushirikiano wa muda mrefu.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Ushauri wa Kifedha ya Exodus Advisory, Ramadhan Kagwandi, amesema athari za kiuchumi zinazotokana na majanga ya kimataifa, hususan kupanda kwa bei ya mafuta, zinahitaji hatua za muda mfupi na muda mrefu.
Amesema ni muhimu kuongeza uwekezaji katika nishati mbadala na matumizi ya gesi ili kupunguza utegemezi wa mafuta yanayoagizwa kutoka nje.
“Serikali inapaswa pia kuangalia namna ya kuwa na akiba ya kutosha ya mafuta kwa matumizi ya baadaye endapo nishati hiyo itaendelea kutumika kwa kiwango kikubwa. Hata hivyo, suluhisho la kudumu ni kujenga uchumi unaojitegemea,” amesema.
Ameongeza kuwa hatua zinazochukuliwa na Serikali katika kuongeza mchango wa mapato ya ndani kwenye bajeti ni miongoni mwa mikakati inayoweza kusaidia kuimarisha uwezo wa uchumi wa taifa kujitegemea.
Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Diamond Global Securities, Beatus Mlingi, amesema semina hiyo imewapa washiriki fursa ya kupata mawazo na mbinu mpya za kuendesha shughuli zao kwa ufanisi, licha ya changamoto zinazoendelea kujitokeza katika mazingira ya biashara na uwekezaji.
“Majadiliano yaliyofanyika yamechangia kupanua uelewa wa washiriki kuhusu namna ya kutumia fursa zilizopo na kukabiliana na hatari zinazoweza kuathiri shughuli zao za kifedha,” amesema.