Ansaf yashauri kuboresha sekta ya kilimo “tuweke vichocheo”
Mkurugenzi Mtendaji wa Jukwaa la Wadau wa Kilimo Lisilo la Kiserikali (Ansaf), Audax Lukonge.
Muktasari:
- ANSAF yashauri kufanyika kwa maboresho katika teknolojia ya uvunaji wa maji ya mvua ili yatumike kikamilifu katika kilimo ili kupunguza mfumuko wa bei za vyakula pindi unapotokea.
Dar es Salaam. Mkurugenzi Mtendaji wa Jukwaa la Wadau wa Kilimo Lisilo la Kiserikali (Ansaf), Audax Lukonge ameshauri uboreshaji wa teknolojia ya uvunaji wa maji ya mvua ili yatumike kikamilifu katika kilimo.
Ametoa ushauri huo leo Jumatano Januari 18, 2023 katika mjadala wa Twitter Space uliondaliwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), wenye mada ya ‘nini kifanyike kudhibiti mfumo wa bei za vyakula.’
“Tukaboresha zaidi uvunaji wa maji ya mvua inayoendelea kunyesha kwa kuwa asilimia 90 inapotea haitumiki, haya maji tuliyoyaona yatapotea kuna haja ya kuboresha teknolojia. Tuvune maji ili tuyatumie kumwagilia,” amesema Lukonge.
Amesema hatua hiyo itasaidia kupunguza mfumuko wa bei akishauri kuongeza thamani na uchakataji wa haya mazao, akisema suala hilo linakwenda sambamba na uimarishaji wa sekta binafsi.
Amesema ni lazima kuendelea kuweka vichocheo, kuna watu wanaochukua bidhaa wanaziweka sokoni.
“Kuongeza thamani na uchakataji wa mazao. Kitu hiki kinaenda na uimarishaji wa sekta binafsi kwani ni lazima kuendelea kuweka vichocheo kuna watu wanachukua hizi bidhaa wanaziweka sokoni, tutafanyaje kuwahamasisha vichocheo vya kikodi, huduma kama umeme, barabara vinawavutia kuwekeza ili kuhakikisha vyakula vinapatikana kwa wakati na kwa bei rahisi,” amesema
Akichangia mada hiyo, Mwaura Robert amesema kitu ambacho kitaongeza chakula nchini na kuzuia bei zisipande ni uwepo na mashamba makubwa yanayotumia miundombinu ya kisasa.
Amesema jambo la muhimu jingine lazima maji yapo ili shughuli hiyo ifanikiwe.
“Wakulima wadogo wanalima na roho zao wakiomba Mungu mvua inyeshe wakulima wakubwa wanalima kwa umwagiliaji na kisasa zaidi. Wakulima wa Afrika Kusini wanatumia mbegu za kisasa na kilimo cha umwagiliaji tofauti na sisi, watu wawekeze katika kilimo kikubwa, na tukiwa na mbegu za kisasa chakula kitaongezeka,” amesema Robert.
Naye, Zirack Andrew amesema tangu mwaka 2019 uzalishaji wa chakula umekuwa ukipanda kutoka tani milioni 16 na mwaka 2021 ilikuwa tani milioni 18 iliongezeka ingawa takwimu za mwaka 2023 hazijatoka inaonyesha kuna upungufu ukiangalia uhalisia twa uzalishaji kwa mwaka.
“Inaweza kuwa sababu kubwa iliyosababisha bei kupanda ni vita vya Urusi na Ukraine nchi hizi mbili zinauza nafaka, kiasi kikubwa cha ngano kinatoka nje ya nchi bidhaa kama chapati, mikate zinapanda kwa zaidi.
“Lakini pia hizi nchi ni wazalishaji wa mafuta hivyo gharama zikipanda uzalishaji pia unapanda. Inachangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la gharama tangu vita ilipoanza wataalamu walishatabiri kwamba itachangia mfumuko wa bei kwa asilimia 17,” amesema Andrew.