Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

ATCL yazindua safari za ndege Mwanza–Dodoma

Muktasari:

  • ATCL imeeleza kuwa inaendelea kupanua mtandao wake kwa kuanzisha ruti mpya za ndani na kimataifa, zikiwemo Musoma, Shinyanga, Moscow na Muscat.

Mwanza. Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) limezindua rasmi safari za ndege kati ya Mwanza na Dodoma, hatua inayopunguza muda wa safari kutoka kati ya saa 10 hadi 12 kwa barabara hadi saa 1 na dakika 20 kwa anga.

Uzinduzi huo ulifanyika usiku wa Juni 19, 2026 katika Uwanja wa Ndege wa Mwanza, ukitajwa kuwa kichocheo kikubwa cha ukuaji wa uchumi katika Kanda ya Ziwa.

Akizungumza katika hafla hiyo, Meneja wa ATCL Mkoa wa Mwanza, Paskas Samwel amesema uzinduzi huo ni sehemu ya mkakati wa serikali wa kufungua uchumi na kuboresha huduma za usafiri wa anga nchini.

Amesema safari hiyo ilianza rasmi kiutendaji Juni 5, 2026 na kwa sasa inaendeshwa mara mbili kwa wiki, Ijumaa na Jumamosi, huku akibainisha kuwa itarahisisha usafiri kwa wafanyabiashara, viongozi na wananchi kwa ujumla.

Viongozi na wananchi wakishuka katika ndege ya ATCL baada ya kuwasili Uwanja wa Ndege wa Mwanza wakitokea Dodoma kufuatia uzinduzi wa safari hiyo. Picha na Saada Amir

Samwel, aliyemuwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa ATCL, Peter Ulanga, amesema ongezeko la safari hiyo pamoja na ruti mpya kupitia Geita na Kilimanjaro limeongeza idadi ya safari hadi kufikia 160 kwa mwezi katika kituo cha Mwanza, sawa na wastani wa ndege tano hadi saba kwa siku.

Amesema kituo hicho kwa sasa kinahudumia kati ya abiria 1,000 hadi 1,300 kwa siku, ishara ya kuongezeka kwa imani ya wananchi kwa shirika hilo na ukuaji wa sekta ya usafiri wa anga.

“Safari hii imewekewa bei rafiki, ambapo tiketi ya kwenda ni Sh246,900 na ya kwenda na kurudi ni Sh409,600 ili wananchi wengi waweze kumudu,” amesema.

Mbali na uzinduzi huo, Samwel amesema ATCL inaendelea kupanua mtandao wake wa safari kwa kuanzisha ruti mpya za ndani na kimataifa katika kipindi cha karibuni.

Ametaja baadhi ya safari hizo kuwa ni pamoja na Musoma na Shinyanga, huku safari za kimataifa zikitarajiwa kuanza Moscow nchini Urusi kuanzia Julai 1, 2026 na Muscat nchini Oman kuanzia Julai 23, 2026.

Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Amiri Mkalipa, akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda amesema uzinduzi huo ni mageuzi makubwa ya miundombinu ya usafiri katika mkoa huo na Kanda ya Ziwa kwa ujumla.

Amesema awali wasafiri walilazimika kupitia Dar es Salaam ili kufika Dodoma, hali iliyoongeza muda na gharama za safari.

“Leo mtu anaweza kusafiri moja kwa moja kutoka Mwanza hadi Dodoma bila kupitia Dar es Salaam. Haya ni mapinduzi makubwa,” amesema Mkalipa.

Ameeleza kuwa Mkoa wa Mwanza ni wa pili kwa kuchangia pato la taifa na ni kitovu cha Kanda ya Ziwa yenye zaidi ya watu milioni 19, hivyo unahitaji huduma imara za usafiri wa anga.

MNEC na aliyekuwa Mbunge wa Ilemela, Dk Angelina Mabula amesema uzinduzi huo ni utekelezaji wa kilio cha muda mrefu cha wabunge wa Kanda ya Ziwa.

“Hiki kilikuwa kilio cha muda mrefu... leo Serikali imetekeleza na kuleta suluhisho kwa wananchi,” amesema.

“Mwanza ni hub (kitovu) ya maziwa makuu na ndiyo kitovu cha uchumi katika Kanda ya Ziwa, hivyo safari hii inakwenda kunyanyua uchumi wa kanda hii na kupunguza adha iliyokuwepo,” amesema.

Mbunge wa Bariadi Vijijini, Masanja Kadogosa amesema ruti hiyo itachochea maendeleo ya uchumi kwa mikoa ya Kanda ya Ziwa kwa kurahisisha usafiri na kupunguza gharama.

Naye Mbunge wa Rorya, Jafari Chege amesema huduma hiyo itapunguza muda wa utekelezaji wa shughuli za maendeleo kwa wananchi na viongozi.

“Huduma hii kwetu ni muhimu sana na ni muhimu kwa sababu sasa tunaenda kutumia muda mfupi kushughulika na changamoto ambazo awali tulitumia muda mrefu,”

“Nimetumia saa moja na dakika 20 kutua kwenye uwanja huu.. nipongeze sana Serikali, ni achievement (fanikio) kubwa sana wameifanya,” amesema.

Mbunge wa Ilemela, Kafiti William ameomba kuongezwa kwa siku za safari ili kukidhi mahitaji ya wananchi, akisema Mwanza ina abiria wengi na fursa kubwa za usafiri wa anga.

“Uwanja huu una abiria na fursa nyingi... pamoja na kushukuru safari hizi za Ijumaa na Jumamosi, wabunge wenzangu wa Kanda ya Ziwa na wananchi wameniagiza kuomba uongozi wa ATCL uangalie angalau kuwe na safari ya Jumanne, Ijumaa na Jumamosi,” amesema.