Bei za petroli, dizeli zashuka kiduchu

Muktasari:

  • Ewura imesema kupungua kumetokana na kupungua kwa bei ya mafuta yaliyosafishwa katika soko la dunia (FBO).

Dar es Salaam. Bei ya rejareja ya mafuta ya petroli kupitia Bandari ya Dar es Salaam inayoanza kutumika leo Juni 5, 2024 imeshuka kwa Sh52.72 na kufikia Sh3, 261 kwa lita moja, ikilinganishwa na bei ya mwezi uliopita.

Taarifa iliyotolewa na Mamlaka ya Udhibiti Huduma za Nishati na Maji (Ewura) inaonyesha bei ya dizeli inayochukuliwa kwenye bandari hiyo imeshuka hadi Sh3, 112 kutoka Sh3,196 iliyokuwa inatumika mwezi uliopita.

Hata hivyo, kushuka kwa bei ya petroli bado kunaifanya kuwa ya juu zaidi katika kipindi cha miezi mitano kati ya Desemba 2023 na Machi 2024.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kupungua huko kumetokana na kupungua kwa bei ya mafuta yaliyosafishwa katika soko la dunia (FBO) kwa wastani wa asilimia 11.82 kwa petroli na asilimia 7.77 kwa dizeli.

“Mabadiliko ya bei yamechangiwa na kupungua kwa gharama za kuagiza mafuta kwa wastani wa asilimia 2.26 kwa petroli na asilimia 8.51 kwa dizeli kwa Bandari ya Dar es Salaam,” imesema taarifa iliyosainiwa na Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Dk James Mwainyekule.

Kwa Bandari ya Tanga bei ya petroli imeshuka hadi Sh3,263 kutoka Sh 3,360 kwa mwezi uliopita kwa upande wa dizeli nayo imeshuka hadi Sh 3,121 kutoka Sh 3,242.

Katika Bandari ya Mtwara petroli imeshuka na itauzwa kwa rejareja kwa Sh 3,267  kutoka Sh 3,317 kwa mwezi uliopita na dizeli itauzwa Sh3,122 kutoka Sh3,200 mwezi uliopita.

Kwa mujibu wa mtandao wa Treading Economics, bei ya mafuta ghafi kwenye soko la dunia katika miezi miwili liyopita imepungua kwa asilimia 15 hadi Dola za Marekani 73.89 (Sh184,725) kwa pipa Juni 4 ikilinganishwa na Dola za Marekani 86.63 (Sh216,575) kwa pipa iliyorekodiwa Aprili 5 mwaka huu.