Benki ya Exim yaadhimisha wiki ya huduma kwa wateja, yaahidi huduma zilizoboreshwa zaidi

Wafanyakazi wa Benki ya Exim, wakiongozwa na Mkuu wa Idara ya Huduma kwa Wateja wa benki hiyo, Bwana Frank Matoro (katikati) wakitoa huduma kwa mmoja wa wateja wa benki hiyo wakati wa hafla hiyo.

Dar es Salaam. Benki ya Exim Tanzania imeungana na watoa huduma ulimwenguni kote kusherehekea wiki ya Huduma kwa Wateja huku ikiahidi kutoa huduma bora zaidi kwa wateja wake ili kuongeza ustawi wao sambamba na kuongeza huduma zenye ubunifu zaidi  kwenye soko la huduma za kifedha.

Kauli mbiu ya maadhimisho hayo kwa mwaka huu ni, "Nguvu ya Huduma," ambayo inaonyesha umuhimu wa huduma kwa wateja na pamoja na watoa huduma katika kusaidia wateja kila siku.

Akitoa salamu za heri kwa wateja na wafanyakazi wa benki hiyo jijini Dar es Salaam leo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki hiyo, Jaffari Matundu alisema kuna haja ya kulinda wateja kwa bidii na kuleta kwenye soko bidhaa za ubunifu ambazo zitasaidia kuinadi benki hiyo kama chapa yenye nguvu.

"Wiki ya Huduma kwa Wateja imetoa tena nafasi nzuri kwa benki kusherehekea jukumu muhimu ambalo tumekuwa kukilifanya kila siku yaani kuwahudumia wateja wetu  na kuonyesha umuhimu wa ushirikiano baina yetu kama uongozi, wafanyakazi pamoja na wateja wetu,’’ alisema.

Kwa upande wake Ofisa Mkuu Idara ya Fedha, Shani Kinswaga alipongeza wafanyakazi wote wa benki hiyo akisema utoaji bora wa huduma ni kiungo muhimu katika kuhakikisha wateja hao wanaridhika huku akiwataja wafanyakazi hao kama mashujaa muhimu ambao wamekuwa wakihakikisha wateja wanaridhika kupitia huduma bora wanazozitoa.

"Zaidi pia ningependa tuendelee kuzingatia na kujitolea katika kutoa huduma bora kwa wateja wetu ambao wameendelea kuwa waaminifu kwetu pia.” alisema Kinswaga wakati akihimiza timu ya wafanyakazi hao kujisikia fahari kwa michango yao.

Katika tukio hilo, ilishuhudiwa wafanyakazi hao wakihudimiwa kifungua kinywa na Matundu sambamba na kujadili pamoja maswala muhimu ikiwemo namna bora ya uboreshaji wa huduma sambamba na kujadili  fursa zinazopatikana kupitia ukuaji wa biashara.

Huku akisisitiza kuwa kila siku ni siku ya huduma kwa wateja katika benki hiyo, Mkuu wa Idara ya Huduma kwa Wateja wa benki hiyo, Frank Matoro alisema benki imeendelea kujitolea kutoa kiwango cha huduma zenye ubora wa hali ya juu kwa wateja wake na wadau bila kujali hali zao au wapi walipo kote nchini.

"Kama sehemu ya hatua za kurejesha fadhila na uaminifu wa wateja wetu, tumepanga shughuli kadhaa za kipekee na maalum kuwathamini wateja. Baadhi ya shughuli ni pamoja na kutembelea wateja kwa kushtukiza na kuwazawadia kama njia ya kuwashukuru kwa kuwa waaminifu kwetu.,’’ alisema

"Kuridhika kwa wateja ndiko kunatufanya tuendelee… bila wateja wetu sisi sio chochote. Kaulimbiu ya kimataifa ni 'Nguvu ya Huduma "lakini katika benki ya Exim tulienda mbali zaidi na kwa kuwa tunajivunia kuwahudumia wateja wetu, kwetu sisi kaulimbiu ni' Fahari Kukuhudumia " alisema.