Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Biashara ya Sh3.89 bilioni yafanyika Sabasaba, Rais Mwinyi atoa maagizo

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Mwinyi, leo Julai 13, 2026, akiwasili kufunga rasmi Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (DITF) ya Jubilei ya Miaka 50.

Muktasari:

  • Hadi Julai 12, taasisi mbalimbali zilizotoa huduma kupitia Business Clinic na mabanda yao, zikiwemo Idara ya Uhamiaji, Nida, Rita na Brela zilikuwa zimehudumia wananchi 27,350, huku watu 2,833 wakipata huduma za afya na wengine 23,435 wakihudumiwa na taasisi za kifedha na benki.

Dar es Salaam. Biashara ya papo kwa papo yenye thamani ya Sh3.89 bilioni imefanyika katika Maonyesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) huku Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi akiwataka wafanyabiashara na wazalishaji nchini kutumia kikamilifu fursa za masoko yanayopatikana.

Miongoni mwa masoko hayo ni  Soko Huru la Afrika (AfCFTA) na mpango wa ushuru sifuri (Zero Tariff) ili kuongeza uzalishaji na kupanua wigo wa biashara zao.

Akizungumza katika hafla ya kufunga maonyesho hayo leo Jumatatu Julai 13, 2026, Dk Mwinyi amesema Tanzania ina nafasi kubwa ya kunufaika na masoko ya kikanda na kimataifa kwa kuwaunganisha wazalishaji na wanunuzi wa ndani na nje ya nchi.

Amesema fursa hizo zinapaswa kutumiwa kuongeza uzalishaji wa bidhaa bora zenye ushindani na zinazokidhi mahitaji ya masoko mbalimbali, huku akisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa biashara na uwekezaji.

Hilo litafanyika kwa kuboresha mifumo ya kufanya biashara, kupunguza urasimu, kuimarisha miundombinu na kuhakikisha sera na mikakati inayowekwa inaleta matokeo chanya katika sekta ya biashara na viwanda.

“Serikali itaendelea kuhakikisha taarifa kuhusu fursa za masoko zinawafikia Watanzania ili waweze kushiriki kikamilifu na kunufaika na masoko makubwa ya Afrika na maeneo mengine duniani,” amesema Dk Mwinyi.

Amesema hatua hiyo itasaidia kuongeza uzalishaji, ajira na mchango wa sekta binafsi katika ukuaji wa uchumi wa Taifa.


Taarifa mkurugenzi

Akitoa taarifa ya maonyesho hayo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), Latifa Khamis amesema takwimu za awali zinaonesha biashara ya papo kwa papo ya Sh3.89 bilioni imefanyika.

Pia maonyesho hayo yamewezesha kupatikana kwa oda za mauzo ya nje zenye thamani ya Sh1.12 trilioni hatua inayoonesha kuimarika kwa ushirikiano wa kibiashara na fursa za kuongeza mauzo ya bidhaa za Tanzania katika masoko ya kimataifa.

“Hadi Julai 12, taasisi mbalimbali zilizotoa huduma kupitia Business Clinic na mabanda yao, zikiwemo Idara ya Uhamiaji, Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita) na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela) zilikuwa zimehudumia wananchi 27,350, huku watu 2,833 wakipata huduma za afya na wengine 23,435 wakihudumiwa na taasisi za kifedha na benki,” amesema.

Amesema takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 58.6 ya bidhaa zilizoonyeshwa zilikuwa zinazozalishwa nchini, asilimia 33.9 zikitoka nje ya nchi, huku asilimia 7.5 ya waoneshaji wakionyesha bidhaa za ndani na za nje kwa pamoja.

Pia utafiti uliofanywa na TanTrade kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) umebaini kuwa asilimia 92 ya watembeleaji wameridhishwa na maonyesho hayo na wako tayari kushiriki tena katika siku zijazo.

“Matokeo haya yanathibitisha kuwa Maonesho ya Sabasaba yanaendelea kuwa jukwaa muhimu la kukuza biashara, uwekezaji, ubunifu na upatikanaji wa huduma mbalimbali nchini,” amesema Latifa.

Kwa upande wake, Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga amesema maonyesho hayo yameonesha uwezo mkubwa wa Tanzania katika uzalishaji, ubunifu na kuongeza thamani ya bidhaa zinazozalishwa nchini.

“Maonesho haya yamekuwa sehemu muhimu ya kuunganisha wazalishaji, wafanyabiashara na wawekezaji kwa lengo la kukuza biashara na kuimarisha uchumi,” amesema.

Amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira rafiki kwa sekta binafsi kupitia maboresho ya sera, mifumo na miundombinu itakayowezesha viwanda kukua, kuongeza ajira na kuhakikisha bidhaa za Tanzania zinakuwa na ushindani katika masoko ya ndani na nje ya nchi.

Kapinga amesema mkazo utaendelea kuwekwa katika kuongeza thamani ya malighafi zinazozalishwa nchini ili kunufaisha wananchi na kukuza mnyororo wa thamani huku akiwataka wazalishaji na wafanyabiashara kutumia fursa zinazotokana na maonyesho hayo kuendeleza ubunifu, kuzingatia viwango na kuboresha ubora wa bidhaa zao.

Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- Kazi, Uchumi na Uwekezaji wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Shariff Ali Shariff amesema hatua ya sasa ya maendeleo ya uchumi inahitaji uwekezaji mkubwa katika ubunifu, matumizi ya teknolojia za kisasa na biashara mtandao pamoja na mifumo ya uendeshaji inayozingatia viwango vya ubora vinavyokubalika kimataifa.

Amesema maeneo hayo ni msingi wa kuongeza ushindani wa bidhaa na huduma zinazozalishwa nchini katika masoko ya kikanda na kimataifa, sambamba na kuongeza thamani ya uzalishaji wa ndani na kuimarisha uwezo wa sekta binafsi kushindana katika soko la dunia.

“Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji, kuimarisha miundombinu ya kiuchumi na kutekeleza sera zinazochochea ukuaji wa viwanda na biashara kwa lengo la kuongeza mauzo ya nje, kukuza uchumi na kuboresha ustawi wa wananchi,” amesema.