Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Dhahabu, utalii zaipa nguvu Shilingi ya Tanzania

Muktasari:

  • Kufuatia kufanya vizuri kwa swkta ya Utalii na mauzo ya dhahabu, akiba ya fedha za kigeni imeimarika hadi kufikia takribani Dola 6 bilioni za Marekani kiwango kinachotosha kuhimili uagizaji wa bidhaa kwa miezi 4.3.

Dar es Salaam. Kuongezeka kwa mapato kutoka kwenye mauzo ya dhahabu na utalii kumeendelea kuipa thamani Shilingi ya Tanzania katika kipindi ambacho uchumi wa dunia umetikiswa na mgogoro wa Mashariki ya Kati ulioathiri masoko ya nishati na biashara.

Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imesema hayo leo Ijumaa, Julai 3, 2026 wakati ikizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam ilipokuwa ikitoa taarifa ya Kamati ya Sera ya Fedha (MPC).

Akizungumza wakati wa kusoma taarifa hiyo, Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba amesema kuimarika kwa mauzo ya nje ya dhahabu, mapato ya utalii pamoja na bidhaa za kilimo kumeongeza upatikanaji wa fedha za kigeni na kusaidia kuimarisha uthabiti wa shilingi.

Amesema kufuatia kufanya vizuri kwa sekta hizo, akiba ya fedha za kigeni imeimarika hadi kufikia takribani Dola 6 bilioni za Marekani kiwango kinachotosha kuhimili uagizaji wa bidhaa kwa miezi 4.3.

“Mwenendo huo umechangia kupunguza shinikizo la kushuka kwa thamani ya shilingi, huku mahitaji ya fedha za kigeni yakidhibitiwa na mapato yanayoingia nchini kupitia sekta za kimkakati,” amesema.

Jambo hilo lilifanya thamani ya Shilingi ya Tanzania kuwa imara na thamani yake isishuke kwa kiasi kikubwa dhidi ya fedha za kigeni kama ambavyo wengi walitarajia kuona.

Taarifa ya viwango cha ubadilishaji fedha za kigeni ya BoT inaonesha, licha ya misukumo iliyotokea hadi robo ya pili ya mwaka 2026 inafikia tamati  Juni 30 mwaka huu Euro ilikuwa ikinunuliwa kwa Sh2,977.23 na kuuzwa kwa Sh3,007 huku Dola 1 ya Marekani ilinunuliwa kwa Sh2,610.46 na kuuzwa kwa Sh2,636.51.

Ukilinganisha na tarehe ya mwisho ya robo ya kwanza ya mwaka 2026, Machi 31 mwaka huu  Euro ilikuwa ikinunuliwa kwa Sh2950.9 na kuuzwa kwa Sh2,980.45 huku Dola ya Marekani ikinunuliwa kwa 2,568.72 na kuuzwa kwa Sh2,594.

Hata hivyo, Benki Kuu imeonya mazingira ya uchumi wa dunia bado hayajatulia kutokana na athari za mgogoro wa Mashariki ya Kati ambao umeongeza gharama za nishati, usafirishaji na bima katika masoko ya kimataifa.

Kufuatia mashinikizo hayo, MPC imeamua kuongeza Kiwango cha Riba ya Benki Kuu (CBR) kutoka asilimia 5.75 hadi asilimia 6.25 kwa robo ya mwaka inayoishia Septemba 2026 ili kudhibiti mfumuko wa bei na kuhakikisha unabaki ndani ya lengo la asilimia 3 hadi 5.

BoT imesema licha ya changamoto hizo, uchumi wa Tanzania umeendelea kuonesha uimara, ukiungwa mkono na sekta za kilimo, ujenzi, madini, huduma na utalii, huku Tanzania Bara ikikadiriwa kukua kwa takribani asilimia 6 katika nusu ya kwanza ya mwaka 2026.

Kwa upande wa Zanzibar, uchumi umekua kwa asilimia 6.6, ukichochewa zaidi na sekta ya utalii na ujenzi.

Benki Kuu imesisitiza kuwa itaendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa uchumi wa ndani na nje ili kuhakikisha uthabiti wa bei, shilingi na ukuaji endelevu wa uchumi.

Mwenyekiti wa Taasisi ya Mabenki Tanzania (TBA), Teobald Sabi amesema hatua zinazochukuliwa na BoT zimeendelea kuimarisha uthabiti wa sekta ya fedha huku mfumuko wa bei ukibaki ndani ya viwango vinavyokubalika licha ya shinikizo kutoka kwa hali ya uchumi wa dunia.

Amesema sekta ya mabenki inaendelea kuwa na ukwasi wa kutosha na iko tayari kuunga mkono juhudi za kukuza uchumi.

“Kwa kuzingatia hali ya sasa ya uchumi, uamuzi wa Benki Kuu wa kuongeza kiwango cha riba ni hatua sahihi ambayo inaimarisha zaidi imani katika mfumo wa uchumi na uthabiti wa sera za fedha,” amesema.

Amesema katika majadiliano na wadau wa sekta ya fedha kutoka nchi nyingine, Tanzania imekuwa ikipata pongezi kutokana na viashiria vyake vya kiuchumi vinavyoonesha uimara, hususan ukuaji wa Pato la Taifa na udhibiti wa mfumuko wa bei.