Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Fedha yatajwa changamoto kupanua biashara za vijana

Mratibu wa kikao cha tatu cha maarifa cha TELS, Gloria Lema, akizungumza na wajasiriamali vijana jijini Dodoma hivi karibuni.

Muktasari:

  • Majadiliano hayo yaligusia pia changamoto zinazowakabili vijana wengi wanapojaribu kuhamisha biashara zao kutoka mfumo usio rasmi kwenda biashara zenye mifumo ya ukuaji na usimamizi wa kisasa.

Dodoma. Wajasiriamali vijana wameanika changamoto zinazokwamisha ukuaji wa biashara zao ikiwemo dhamana, pamoja na kupata fedha ambapo bado inaathiri ukuaji licha ya kupata maarifa na mafunzo mbalimbali ya biashara.

Changamoto hizo zimeanishwa hivi karibuni kupitia kikao cha tatu cha maarifa kilichofanyika jijini Dodoma kilichoandaliwa na Jukwaa la Wakurugenzi Watendaji Tanzania (CEO Roundtable of Tanzania-CEOrt), kupitia programu yake ya Think Equal Lead Smart (TELS) inayotekelezwa kwa ushirikiano na Vodacom Tanzania Foundation pamoja na Chemba ya Wanawake Wafanyabiashara Tanzania (TWCC).

Kikao hicho kilichojadili namna biashara zinazoongozwa na vijana zinaweza kujijengea uwezo wa kupata ufadhili wa kifedha kwa uendelevu wa biashara zao kilibebwa na kaulimbiu isemayo:  “Nini Kinahitajika kwa Biashara Inayoongozwa na Vijana Kuwa Tayari Kupata Ufadhili wa Kifedha”,  kiliwaleta pamoja wajasiriamali vijana, wadau wa maendeleo na wataalamu wa biashara kujadili changamoto na fursa zinazohusiana na upatikanaji wa mitaji.

Mjasiriamali kijana na mwanzilishi mwenza wa Mama Health, Salma Nguku, amesema wamiliki wa biashara ndogo bado wanapata ugumu kuelewa matarajio ya taasisi za kifedha wanapoomba mikopo au uwekezaji.

“Kwa vijana wengi, biashara hukua kupitia faida ndogo na akiba binafsi kwa sababu mifumo ya kupata fedha huonekana kuwa migumu. Majadiliano kama haya yanarahisisha uelewa kuhusu namna taasisi za kifedha zinavyofanya kazi na hatua zinazohitajika ili biashara iwe tayari kupata ufadhili,” amesema.

Meshack Tweve, amesema kikao hicho kimemsaidia kuelewa kwa undani umuhimu wa nidhamu ya kifedha katika kuhakikisha biashara inadumu na kukua kwa muda mrefu.

“Wakati mwingine biashara ndogo hujikita zaidi kwenye mauzo ya kila siku bila kuweka mkazo kwenye utunzaji wa kumbukumbu, uwekaji wa akiba na usimamizi mzuri wa fedha. Mafunzo haya yameeleza kwa uwazi kwa nini maeneo hayo yana nafasi kubwa katika ukuaji wa biashara,” amesema.

Awali, akizungumza katika kikao hicho, Meneja wa Miradi wa CEOrt, Hawa Urungu, amesema mjadala huo umeendelea kujitokeza kupitia vikao vya awali vya TELS vilivyofanyika Dar es Salaam na Namanga, ambapo wajasiriamali wengi walieleza kuwa changamoto ya kupata fedha bado inaathiri ukuaji wa biashara zao licha ya kupata maarifa na mafunzo mbalimbali ya biashara.

Amesema uzoefu wa programu za maendeleo ya biashara unaonyesha mafanikio ya biashara nyingi hutegemea siyo maarifa pekee, bali pia uwepo wa mifumo imara ya kifedha na uwezo wa kutumia vizuri fursa za ufadhili zinazopatikana.

“Wajasiriamali vijana tayari wanatoa mchango mkubwa katika uchumi kupitia sekta mbalimbali. Hata hivyo, biashara nyingi bado zinakosa maandalizi muhimu ya kifedha yanayohitajika ili kuvutia uwekezaji na kupata mitaji ya kukuza shughuli zao. Kuongeza uelewa kuhusu nidhamu ya biashara na utayari wa kifedha ni hatua muhimu katika kujenga biashara endelevu,” amesema.

Majadiliano hayo yaligusia pia changamoto zinazowakabili vijana wengi wanapojaribu kuhamisha biashara zao kutoka mfumo usio rasmi kwenda biashara zenye mifumo ya ukuaji na usimamizi wa kisasa.

Washiriki walisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya taasisi za kifedha, mashirika ya maendeleo na sekta binafsi katika kuboresha upatikanaji wa taarifa, mitandao ya biashara na huduma za kifedha kwa vijana.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa TWCC, Naima Nyange, amesema vijana wengi bado wanakumbana na changamoto za dhamana, historia ndogo ya kifedha pamoja na uelewa mdogo wa fursa zilizopo za ufadhili, hali inayochangia biashara nyingi kushindwa kupanuka kwa wakati.

“Majadiliano ya vitendo kuhusu utayari wa kifedha yanasaidia kuongeza kujiamini kwa wajasiriamali na kuwajengea uwezo wa kuelewa maeneo wanayotakiwa kuyaimarisha kabla ya kutafuta mitaji ya biashara,” amesema.