Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Fursa kwa wazalishaji wa kaboni, Sh1.8 bilioni zatolewa

Balozi wa Norway nchini Tanzania, Tone Tinnes, Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya NCMC, Khamis Hamza Khamis, Mwakilishi Mkazi wa UNDP nchini, Shigeki Komatsubara, Ofisa Mtendaji Mkuu wa NCMC, Ngenda Kigaraba kwa pamoja wakionesha hati za mkataba wa makubaliano kati ya Norway, UNDP na Tanzania leo jijini Dar es Salaam.

Muktasari:

  • Makubaliano ya ufadhili huo yamesainiwa leo Alhamisi Julai 2, 2026 jijini Dar es Salaam kati ya Ubalozi wa Kifalme wa Norway nchini Tanzania na UNDP.

Dar es Salaam. Serikali ya Norway imetoa zaidi ya Sh1.8 bilioni kwa Tanzania ili kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji wa uzalishaji wa gesi ya kaboni na kuiwezesha nchi kushiriki kikamilifu katika soko la kimataifa la kaboni, hatua inayotarajiwa kuongeza fursa za uwekezaji na upatikanaji wa fedha za tabianchi.

Fedha hizo, ambazo ni Dola za Marekani 700,000 (sawa na Sh1.8 bilioni) zitatumika kutekeleza mradi wa mwaka mmoja unaojulikana kama MRV4Tanzania, utakaotekelezwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP) kwa kushirikiana na Kituo cha Kitaifa cha Kufuatilia Kaboni (NCMC).

Makubaliano ya ufadhili huo yamesainiwa leo Alhamisi Julai 2, 2026 jijini Dar es Salaam kati ya Ubalozi wa Kifalme wa Norway nchini Tanzania na UNDP.

Mradi huo unalenga kuijengea Tanzania mifumo madhubuti ya kitaasisi, kiufundi na kifedha katika ufuatiliaji, utoaji wa taarifa na uhakiki wa uzalishaji wa gesi hiyo, sambamba na kutekeleza matakwa ya Makubaliano ya Paris kuhusu mabadiliko ya tabianchi na mfumo wa uwazi ulioimarishwa.

Mbali na kuimarisha uwezo wa NCMC, mradi huo utaweka msingi wa kuanzishwa kwa Daftari la Kitaifa la Kaboni (National Carbon Registry), ambalo linatarajiwa kuongeza uaminifu wa Tanzania katika soko la kimataifa la kaboni na kuvutia uwekezaji wa fedha za tabianchi.

Mei 15, 2026, mkurugenzi wa masuala ya upimaji, uhakiki, usajili na tathmini ya gesi joto, kutoka Kituo cha Kuratibu Biashara ya Kaboni Tanzania (NCMC) akizungumza jijini Dar es Salaam alisema kampuni 99 nchini zimejisajili katika biashara ya uuzaji kaboni.

Biashara ya kaboni inalenga kutoa motisha kwa ajili ya shughuli zinazolenga kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi na kuweka ustahimilivu endelevu wa mazingira katika shughuli zote za kiuchumi.

"Miongoni mwa wilaya ambazo zimeanza utekelezaji wa biashara hiyo ipo Tanganyika ambayo mwaka 2024 ilipata Sh14 bilioni kwa jitihada walizozifanya katika uhifadhi wa misitu yao ambayo ni funzo kwa jamii nyingine kushiriki katika biashara hii," alisema mkurugenzi huyo.


Alichokisema Balozi

Akizungumza baada ya utiaji saini wa makubaliano hayo, Balozi wa Norway nchini Tanzania, Tone Tinnes, amesema mifumo imara ya uwazi ndiyo msingi wa mafanikio katika usimamizi wa masuala ya tabianchi.

"Kwa hiyo leo, tumesaini makubaliano ili kuendelea kuunga mkono Kituo cha NCMC. Lengo ni kukiwezesha kuanzisha mfumo thabiti ili waweze kufuatilia kikamilifu uzalishaji kaboni nchini Tanzania. Na kwa kufanya hivyo, Tanzania itaweza kupata mikopo ya kaboni (carbon credits) na ufadhili wa masuala ya kaboni."

"Tunaona kwamba tabianchi ni swala linalomgusa kila mtu duniani, na tunapaswa kufanya kazi pamoja. Hiyo ndiyo sababu pia tuna ushirikiano huu kati yetu na Tanzania kuhusu masuala ya tabianchi. Kuunga mkono NCMC ni sehemu muhimu sana ya ushirikiano huo," amesema.

"Utawala bora wa masuala ya hali ya hewa huanza na taasisi imara. Kupitia ushirikiano huu, Norway inaisaidia Tanzania kujenga mifumo inayohitajika ili kuimarisha uwazi wa masuala ya hali ya hewa na kufungua fursa za kifedha za tabianchi," amesema Tinnes.

Mwakilishi Mkazi wa UNDP nchini, Shigeki Komatsubara, amesema taasisi hiyo itaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania kuhakikisha mradi huo unatekelezwa kwa ufanisi na kuijengea nchi uwezo wa muda mrefu.

Amesema mradi huo utasaidia Tanzania kuwa na mfumo wa kisasa wa uwazi wa taarifa za tabianchi na kuiweka katika nafasi nzuri ya kunufaika na soko linayokua kwa kasi ya biashara ya kaboni duniani.

Katika kipindi cha mwaka mmoja wa awamu ya maandalizi, mradi huo utaweka mifumo ya usimamizi wa fedha, ununuzi na utawala bora ndani ya NCMC, kuimarisha ushirikiano kati ya kituo hicho na taasisi nyingine za Serikali pamoja na kujenga mifumo ya usimamizi wa rasilimali watu.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa NCMC, Ngenda Kigaraba amesema makubaliano hayo yana tija kiuchumi na mazingira katika kufikia soko la kaboni.

Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya NCMC, Khamis Hamza Khamis amesema   bodi hiyo itasimamia matumizi ya fedha hizo kwa uwazi na kuhakikisha mradi unaleta matokeo yaliyokusudiwa.